NA MWANDISHI WETU
MAKACHERO wa Jeshi la Polisi wamemkamata Rahim Nyamka kwa tuhuma za kumtorosha na kumuachisha masomo, mwanafunzi Labna Said Salim anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary's iliyoko Mbezi Makonde.
Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania PANORAMA kutosha ndani ya timu ya maafisa wanne waandamizi wa serikali Wilaya ya Kinondoni inayomsaka Labna zimeeleza kuwa Nyamka alikamatwa Juzi, Novemba 24 na kuhojiwa kabla ya kupendekezwa na timu hiyo kuwa asipewe dhamana.
Timu inayomsaka Labna ambaye alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 inaundwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kinondoni, Afisa wa Usalama wa Wilaya, Afisa Elimu Sekondari na Mthibiti Elimu Kanda.
Taarifa kutoka ndani ya timu ya uchunguzi zimeeleza kushangazwa na uamuzi wa polisi kutozingatia maelekezo ya timu ya uchunguzi ya kutompatia dhamana mtuhumiwa huyo.
"Tumemsaka huyo mtuhumiwa mpaka tumempata, tulimkamata tukiwa na askari wapelelezi tukampeleka kituo cha Polisi Goba ambako ndiko kesi ilikofunguliwa, huko tulimuhoji kisha tukawaachia polisi lakini tuliwaambia wasimwachie kulingana na mwenendo wa uchunguzi wa shauri hili.
" Ajabu tulipoondoka wakampa dhamana. Hili jambo limetushangaza hata sisi kwani tumeshindwa kujua kuna nini kinaendelea pale Polisi Goba lakini wapo wenzangu wa vyombo vya ulinzi na usalama ndani ya timu nao wameliona hili na limewashangaza pia naamini watalifanyia kazi, alisema mmoja wa wajumbe wa timu hiyo.
Akizungumzia mwenendo wa uchunguzi ulipofikia alisema Labna bado hajapatikana na baada ya kuhojiwa kwa Nyamka alikana kumtorosha au kuwa naye.
"Bado aisee, yule mtuhumiwa Nyamka amekana tuhuma zote lakini vijana sita tuliowakamata wakivuta bangi ndani ya nyumba ya baba yake Nyamka ambaye Kamishna Mstaafu Magereza wamekiri katika mahojiano kuwa Labna alifika kwenye hiyo Nyumba na alikuwa anawapikia na walipata kumvutisha bangi.
" Mbali na hao, wale vijana waliomsadia kuruka ukuta nao wamekiri kuwa ni kweli walitenda tukio hilo. Tatizo kuna mambo ambayo timu inapigana kuyabaini lakini huko chini kuna watu wanavuruga," alisema.
Jitahidi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuwa inaita bila kupokelewa.
Labna alitoweka shuleni Oktoba 4, mwaka huu lakini uongozi wa shule ya St Mary's alificha taarifa za kutoweka kwake hadi Oktoba 8, 2020 ambapo Matroni wake anayefamika kwa jina la Sarah Murra alipompigia simu yake mama yake kumuiliza kama yupo nyumbani.
Mkuu wa Shule ya St. Mary's Sekondari, Reca Ntipoo amekaririwa na timu ya uchunguzi akiungama kuwa uongozi wa shule ulifanya makosa kutotoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mtoto huyo.
Ntipoo pia alieleza timu hiyo kuwa alipohamishiwa shuleni hapo alikuta wanafunzi hao wakitoroka usiku na kurudi alfajili jambo lilimjanisha kuwa hata Labna baada ya kutoroka angerudi kwa sababu kitendo hicho ni kawaida shuleni hapo.
Aidha uchunguzi wa awali wa timu umebaini kuwa shule hiyo imepungukiwa sifa kwa sababu ni chafu, haina ulinzi wa kutosha na uzio wake (ukuta) siyo imara.
Timu hiyo pia ilibaini vijana saba waliokuwa wakivuta bangi nyumbani kwa Kamishna Mstaafu wa Jeshi Magereza na pia ndani ya ua wa nyumba kulikuwa na shamba la bangi. Nyumba hiyo ndiyo anayoishi Rahim na ndugu yake.
ReplyForward |
No comments:
Post a Comment