banner

Tuesday, November 24, 2020

WALIOFICHA SARUJI KUSAKWA MKOA KWA MKOA



*Waziri Mkuu Majaliwa awaagiza MA RC kuwakagua mawakala, wauzaji wa kati na wadogo

NA MWANDISHI MAALUM

SERIKALI sasa imeanza kuchukua hatua mahususi za kupambana na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu walioficha saruji kwa lengo la kuleta taharuki katika nchi.

Hatua hizo zimetangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kuwaagiza wakuu wa mikoa yote nchini kufanya ukaguzi kwenye viwanda vya kuzalisha saruji, kwa mawakala na wauzaji wa kati na wadogo.

Waziri Mkuu Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa kuwachukulia hatua stahiki wale wote watakaobainika kuficha saruji katika msako watakaoufanya.

Agizo hilo alilitoa alippkuwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa yote nchini kuhusu tatizo la kupanda kwa bei ya saruji, kwenye kikao alichokiendesha kwa njia ya video (video conferencing) kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

"Wakuu wa Mikoa na Kamati zenu za Ulinzi na Usalama fanyeni ukaguzi kwa mawakala, ukikuta wamerundika saruji kamata na kuwashtaki. Nendeni pia kwa wauzaji wa kati, nao pia chekini maghala yao.

“Piteni kwa maafisa biashara na muwasimamie iwe ni kwenye Sekretarieti za Mikoa au katika Halmashauri zenu, tunataka bei irudi kama ilivyokuwa mwezi Septemba kwa sababu hakuna badiliko lolote kwenye tozo ya kodi,” alisisitiza.

Agizo hili la kupambana na walanguzi wa saruji limetolewa na Waziri Mkuu Majaliwa katika kikao chake cha kwanza na Wakuu wa Mikoa tangu alipoapishwa kushika wadhfa huo kwa mara pili.

"Wakati wa uapisho, Novemba 16, mwaka huu nilitambulisha tatizo la kupatikana saruji kwa bei ya juu sana. Niliagiza kila Mkuu wa Mkoa afuatilie ni kwa nini bei imepanda kiasi hicho.

"Nimepokea taarifa zenu na kuona hali halisi iliyoko kwenye mikoa yenu. Hali si nzuri, akiba iliyopo ni ndogo na bei ni ya juu sana. Nasema bei ni ya juu sababu tunaangalia bei ya mlaji kwa sasa. Awali ilikuwa kati ya sh. 14,000 hadi 15,000 lakini sasa hivi imefikia sh. 24,000 kwa mfuko mmoja,” alisema.



Waziri Mkuu Majaliwa alisema hiyo ni tofauti ya sh. 9,000 hadi 10,000 lakini kwa sasa ni lazima bei ishuke kwa sababu hakuna tozo za kodi zilizoongezeka.

“Kuna watu wanatumia kigezo cha gharama za usafirishaji, hii si kweli kwani hata Septemba, walikuwa wakisafirisha bidhaa hiyo kwa njia zetu zile zile," alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali ya awamu ya tano imekuwa ikihimiza ujenzi wa viwanda ili bidhaa zinazozalishwa nchini zipatikane kwa wingi. “Kwenye saruji malighafi ziko nchini, hazitoki nje, kwa hiyo tunataraji upatikanaji wake uwe rahisi na bei ingekuwa nafuu," alisema.

Aidha, aliwaagiza wakurugenzi wa Wizara ya Viwanda na Biashara wakutane na wenye viwanda na kuweka ratiba ya mwaka ili kuepuka viwanda vingi kufungwa kwa matengenezo ya mwaka kwa wakati mmoja na kufanya saruji iadimike na kupandisha ghafla bei ya saruji.

Vilevile, aliwaagiza viongozi wa Tume ya Ushindani (FCC) wafuatilie wamiliki wenye viwanda vya saruji na wafanye uchunguzi kubaini uhalali wa bei zinazopangwa na mawakala na wafanyabiashara wa saruji nchini.  Pia akawataka wawasisitizie wazingatie sheria za nchi.

Kwa upande wao, wakuu wa mikoa walisema wamepokea maelekezo na watayatekeleza.

Mkutano huo uliwashirikisha pia Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara za Viwanda na Biashara; Uchukuzi na watendaji kutoka Tume ya Ushindani.

No comments:

Post a Comment