NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala kimesema hakina
shaka na maelezo yaliyotolewa na Diwani wake wa Kata Kivukoni, Sharik Choughule
kuhusu uraia wake.
Kimesema kabla ya wagombea wa chama hicho kupitishwa kupeperusha
bendera ya chama katika uchaguzi,
kilijiridhisha kuwa wote wana sifa stahiki.
CCM kimesema watu wanaoibuka sasa kudai uraia wa Choughule
una utata wanapaswa kupuuzwa kwa sababu CCM huteua wagombea wake kwa umakini na
baada ya kujiridhisha hivyo wenye shaka na uteuzi huo wafuate taratibu za
kimahakama kuthibitisha madai yao.
Hayo yameelezwa jana na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Ilala Iddi
Mkowa katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA kuhusu madai ya utata wa uraia
wa Choughule na kwamba alitoa taarifa zisizokuwa sahihi kwa chama
zilizomuwezesha kuteuliwa.
Mkowa alisema CCM hakina muda wa kuanza kuchunguza tuhuma
za udanganyifu au utata wa uraia wa kada wake huyo kwa sababu kina uhakika na
taarifa alizotoa hivyo wenye wasiwasi wana wajibu wa kuthibitisha madai yao
kisheria ndipo chama kiweze kuchukua hatua.
Kauli hii ya Mkowa inafuatia taarifa iliyoripotiwa juzi na
Tanzania PANORAMA kuwa Choughule anadaiwa kutoa taarifa zisizokuwa sahihi
kuhusu uraia wake ili kufanikisha azma yake ya kuwa kiongozi katika chama
hicho.
Madai hayo yalianza kusambaa mapema mwezi uliopita lakini
jitahada za Tanzania PANORAMA kumfikia kuyazungumzia hazikuweza kufanikiwa
kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kutingwa na shughuli nyingi za kisiasa.
Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa kata hiyo aliyefikiwa na
Tanzania PANORAMA na kukubali kuzungumza kwa sharti la jina lake kuhifadhiwa
kwa vile hataki aonekane ana nia mbaya dhidi ya mbio za kusaka uongozi wa
kisiasa za Choughule, alisema awali kulikuwa na utata huo lakini ulitatuliwa.
Taarifa zilizokusanywa Tanzania PANORAMA zimeonyesha kuwa
Choughule aliingia nchini kwa kutumia hati ya kusafiria ya India akiwa
ameambata na ndugu yake wa kiume, ambao walikuja kumtembelea mjomba wao
anayefanya biashara jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi umeonyesha kuwa Choughule na ndugu yake walikuja
nchini kuonana na mjomba wao aliyekuwa ametwaa mali za baba yao baada ya
kufariki dunia.
Washirika wa karibu wa Choughule wamekaririwa kuwa vijana
hao wawili walishindwa kuafikiana na mjomba wao ndipo walipogoma kuondoka
nchini kurejea India walikokuwa wakiishi na mama yao.
Kwamba ili kuzika mzozo baina yao, mjomba wao aliwaingiza
katika moja ya kampuni zake kufanya kazi huku akiwataka wawe na subira ya
kutatua utata wa umiliki wa mali hizo.
Taarifa zaidi zimeeleza kuwa vijana hao walilia na kupiga
magoti mbele ya mjomba wao wakimuomba azungumze na maofisa wa Uhamiaji ili
wasirejeshwe India kwa sababu walikuwa wakiishi maisha ya shida na mama yao
baada ya baba yao kufariki na kwamba mjomba wao alikuwa hawatumii fedha kama
alivyokuwa akifanya baba yao licha ya kujimilikisha mali zote.
Inadaiwa mjomba wao aliwapa sharti la kutomuuliza tena
kuhusu mali alizotwaa kwa marehemu kama wanataka kiendelea kuwepo Tanzania,
amri ambayo waliiafiki na yalifanyika mazungumzo wakaachiwa.
"Ni kweli Choughule alikuja nchini akiwa na mwenzake.
Walikuja kwa mjomba wao lakini baadaye kulitoka mtafaruku wakakamatwa na
uhamiaji wakapandishwa ndege wakarejeshwa India ambako hawakupokelewa
walirudishiwa uwanja wa ndege, wakarejea Tanzania.
"Hakukuwa na namna ikabidi wapokelewe hapa nchini
wakarudi tena kuishi na mjomba wao ndipo zikaanza kufanyika taratibu za uraia
na uhamiaji iliwasafisha kwa kuwapa uraia wakawa huru kujihusisha na shughuli
za kisiasa na mpaka sasa Choughule anaendelea na siasa," alisema.
Choughule amekuwa akikwepa kulizungumzia suala hilo kwa
zaidi ya wiki tatu sasa kwani licha ya Tanzania PANORAMA kufika ofisi za CCM
Kata ya Kivukoni ambako hakupatikani na kisha kutafutwa kwa simu yake ya
kiganjani na kuomba apewe muda kabla ya kuzungumza, hajatekeleza ahadi yake
hiyo wala kujibu maswali aliyotumiwa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphery Polepole
ambaye alitafutwa kwa simu yake ya kiganjani kuzungumzia suala hilo, simu yake
imekuwa ikiita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi kwenye simu
yake hakuujibu.
Kwa mujibu wa taratibu za Idara ya Uhamiaji, raia wa kigeni
anaweza kupewa uraia kabla ya kuwa na sifa za kugombea nafasi za uongozi wa
kisiasa isipokuwa urais wa Tanzania akiishi nchini kuanzia miaka nane na
kufuata taratibu za kuomba uraia ikiwemo muda wote wa kuishi nchini kuwa na
kibali.
Tanzania PANORAMA limeperuzi sifa zinazotakiwa kwa
wanachama wa CCM kugombea uongozi wa kisiasa ambapo ya kwanza inasomeka awe
raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment