NA MWANDISHI WETU
HATIMAYE serikali imeanzisha msako mkali wa mwanafunzi Labna
Salim Said wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Bweni ya St Mary's
ambaye amepotea tangu Oktoba 4, 2020 akiwa shuleni.
Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog
zimeeeza kuwa, msako huo umeanza jana baada ya kufanyika kwa kikao cha ulinzi
na usalama cha Wilaya ya Kinondoni kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo,
Daniel Chongolo.
Chongolo ameithibitishia Tanzania PANORAMA kuitisha na kuongoza kikao hicho na kueleza
kuwa serikali imeanza kuchunguza mazingira ya tukio la kupotea kwa mwanafunzi
huyo akiwa shuleni kwa kuunda kikosi maalumu kinachojumuisha vyombo vya ulinzi
na usalama.
Hata hivyo, Chongolo alisema hayuko katika nafasi nzuri ya
kulizunguzia suala hilo kwa sababu kuhofia kuharibu mwenendo wa uchunguzi
wa timu yake aliyoiunda.
Akizungumzia hatua hiyo ya serikali kujitosa rasmi kwenye
sakata la kupotea kwa mwanafunz Labna, Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya
Kinondoni, Joseph Kapere Chongolo aliitisha kikao cha kamati ya ulinzi na
usalama ofisini kwake jana mchana baada ya kupokea malalamiko ya wazazi wa
mtoto huyo kupotea akiwa shuleni.
Kapere alisema katika kikao hicho kilichohudhuliwa pia na
wazazi wa mtoto huyo, Chongolo aliunda kamati ya watu wanne kumsaka mtoto
Labna popote alipo na kuchunguza mwenendo mzima wa tukio la kupotea kwake.
"Hili tukio ni la aina yake lakini tunasikitika kuwa
limechelewa kutufikia, hata mkuu wa wilaya kafahamu jana baada ya wazazi
kumfikishia kesi hiyo. Hizo shule zipo chini yangu mimi ndiyo nashughulika
nazo.
"Sasa mkuu wa wilaya aliitisha kamati ya ulinzi ya
usalama na ameteua kikosi cha watu wanne kumsaka mtoto huyo.
"Walioteuliwa kwenye kikosi hicho ni viongozi
waandamizi wakiwemo kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa
Kinondoni, ofisi ya Afisa Usalama wa Wilaya ya Kinondoni, mimi mwenyewe Afisa
Elimu Sekondari Wilaya ya Kinondoni," alisema Kapere.
Mwanafunzi msichana, Labna wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya
St. Mary’s alitoroka shuleni usiku na kutokomea kusikojulikana na hadi sasa
hajapatikana.
Labna alitoroka Oktoba 4, 2020 akiwa chini ya uangalizi wa
shule lakini taarifa za kupotea kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake Sarah
Murra aliyempigia simu mama mzazi wa Labna akiulizia kama ameishafika nyumbani.
Katika hatua ya kushangaza, uongozi wa Shule ya Sekondari
ya St Mary’s haukutoa taarifa polisi kuhusu kupotea kwa mwanafunzi huyo na
badala yake wazazi ndiyo walioripoti tukio la mtoto wao kupotea akiwa shuleni.
No comments:
Post a Comment