NA MWANDISHI WETU
TIMU ya maafisa wanne waandamizi wa serikali iliyoundwa na
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo kumsaka mwanafunzi wa kidato cha
tatu wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St Mary's, aliyepotea tangu Oktoba 4,
2020 imebaini kuwa shule hiyo imepungukiwa sifa zinazostahili kisheria.
Afisa Elimu Sekondari ya Wilaya ya Kinondoni, Joseph Kapere
ameyasema hayo alipokuwa akielezea mwenendo wa msako na uchunguzi wa mazingira
ya kutoweka kwa mwanafunzi Labna unaofanywa na timu iliyoundwa na Chongolo.
Kapere alisema katika uchunguzi huo ulioanza jana kwa kumuhoji Mkuu wa Shule ambaye alieleza
kuwa Labna aliwaambia walimu hataki shule na alitoroka akaenda kwa rafiki yake
ya kiume wakawa wanaishi pamoja.
"Tunafanya uchunguzi kwa umakini sana. Tumeishamuhoji
Mkuu wa Shule na yeye ametueleza kuwa huyo mtoto alikwishawambia walimu kuwa
hataki shule na aliondoka shuleni kwa kutoroka.
"Mkuu wa Shule alituambia kuwa motto alitoroka shuleni
kwa kuruka ukuta usiku akisaidiwa na wanafunzi wenzake wavulana wawili, akaenda
kwa boy friend wake wakaanza kuishi pamoja huko,” Kapere alimkariri mkuu wa
shule.
Alisema mkuu huyo wa shule aliipeleka timu ya serikali
nyumba aliyokuwa akiishi Labna na mpenzi wake baada ya kutoroka shule lakini
waliwakosa na badala yake walikuta wavulana saba wakiwa wanavuta bangi.
"Mkuu wa shule anapajua alipotorokea mtoto huyo na
alitupeleka kwenye hiyo nyumba. Ni nyumba ya Kamishna Mstaafu wa Magereza
ambayo wanaishi watoto wake wawili lakini hapo hatukumta Labna wala boy friend
wake, tulikuta vijana saba waliokuwa wanavuta bangi na nyumba nzima ilikuwa
imetapakaa misokoto ya bangi.
"Kwa kweli ni hali ya kutisha sana kwa vijana wetu.
Walituambia ni kweli Labna alipotoroka shule alikuwa akiishi hapo na boy friend
wake na alikuwa mama wa nyumbani kwani alikuwa akiwapikia na kufanya usafi wa
nyumba lakini baada ya muda kidogo aliondoka.
"Boy friend wake naye hatukumkuta, wale vijana wavuta
bangi walisema anasoma chuo CBE na anaishi hostel sasa tumepeleka makachero
akakamatwe huko.
“Lakini hiyo nyumba baada ya kuichunguza kwa sababu ina
uzio mkubwa sana tulikuta shamba la bangi humo ndani. Yaani bangi inalimwa humo
humo nyumbani kwa Kamishna wa Magereza wanavuna wanavuta hao vijana.
"Basi wale vijana tuliwachukua hadi polisi wamelala
huko kwa ajili ya uchunguzi zaidi na taratibu nyingine zitafuata," alisema
Kapere.
Alipoulizwa iwapo timu hiyo imebaini ni kwanini Mkuu wa
Shule baada ya kuambiwa na Labna kuwa hataki shule hakuwapa taarifa wazazi na
hata alipotoroka uongozi wa shule ulikaa kimywa wala haukutoa ripoti polisi,
alisema mwalimu huyo amekiri kuwa yeye na wenzake walikosea.
Tanzania PANORAMA lilimuuliza pia Kapere kama timu ya
serikali imebaini ni kwanini Mkuu wa Shule baada ya kubaini mwanafunzi wake
ametoroka na alikuwa akiishi na mwanaume nje ya shule hakuchukua hatua za kutoa
taarifa kwa wazazi na polisi ili wote wawili wakamatwe kwa kuzingatia
mwanafunzi huyo wazazi wake walimkabidhi kwa uongozi wa shule, Kapere alisema
swali hilo ni zuri na watamuuliza Mkuu wa Shule.
"Timu yetu ina
polisi, hata nyumba ya kamishna tuliivamia tukiwa na polisi. Polisi waliizingira
kisha wakaingia ndani ndiyo wakakuta lile shamba la bangi na ile misokoto.
Lakini Mwalimu anajitetea yeye ni mgemi na tabia ya watoto kutoroka usiku
wakarudi alfajili aliikuta. Lakini pia mkuu wa shule alituambia kuwa awali
yeye, polisi na wajomba wa huyo wa mtoto walikwenda hadi kwenye hiyo nyumba
kumsaka lakini polisi na wajombe hawakuingia ndani, waliishia nje.
"Sasa hata Labna
alipotoroka Mwalimu amesema mwenyewe alijua ndiyo kawaida yao atarudu lakini
kwa bahati mbaya yeye hakurudi, akahamia kabisa kwa huyo boy friend wake.
"Uchunguzi wetu sasa
pale shuleni imebaini kuwa ile shule haifai, imepungukiwa sifa stahiki za
kuitwa shule. Kwanza ni chafu sana, haina walinzi wa kutosha na hata ukuta wake
haufai," alisema Kapere.
Alisema anaamini mtoto
huyo yupo hai na atapatikana katika msako unaoendelea.
Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni, Daniel Chongolo alipoulizwa jana alisema yupo msibani hivyo hayupo
katika nafasi kuzungumza.
Labna, mwanafunzi wa Shule
ya Sekondari ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde Jijini Dar es Salaam alitoweka
shuleni tangu Oktoba 4, 2020 lakini tukio la kutoweka kwake halikuripotiwa polisi na
uongozi wa shule.
No comments:
Post a Comment