banner

Monday, November 9, 2020

WAZAZI WA MWANAFUNZI ALIYEPOTEA ST. MARY’S WAHOFIA KAUAWA

 

Labna Salim Said, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Bweni Wasichana ya St. Mary's iliyopo Mbezi Makonde ambaye amepotea kwa zaidi  ya mwezi mmoja sasa 

NA CHARLES  MULLINDA

WAZAZI wa mwanafunzi msichana, Labna Salim Said wa Shule ya Sekondari ya Bweni Wasichana ya St. Mary’s ambaye alitoroka shuleni usiku na kutokomea kusikojulikana wameeleza kuwa wanahofia mtoto wao kauawa.

Zephania Maduhu ambaye ni mjomba wa mwanafunzi huyo anayesoma kidato cha tatu na pia mlezi wake, ameieleza Tanzania PANORAMA kuwa mtoto wake alipotea tangu Oktoba 4, 2020 akiwa chini ya uangalizi wa shule na hadi sasa hajapatikana.

Alisema taarifa za kupotea kwa mwanafunzi huyo zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake aliyemtaja kwa jina la Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa mwanafunzi huyo akiulizia kama ameishafika nyumbani.

“Huyo mtoto ninamlea mimi, ninamlipia ada ya shule mimi, ni mtoto wa dada yangu, anasoma St. Mary’s Mbezi Makonde. Oktoba 8, mwaka huu, matron wake anaitwa Sarah Murra, alimpigia simu mama yake, yaani dada yangu akimuuliza kama Labna kafika nyumbani.

“Dada yangu ambaye wakati huo alikuwa mkoani Shinyanga akashangaa akamuuliza amefikaje nyumbani wakati yupo shule au shule zimefungwa ghafla tena? Yule matron akamjibu ametoroka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 hivyo alikuwa anataka kujua kama yupo nyumbani, dada akamwambia yeye yupo mkoani Shinyanga na anajua mtoto wake yupo shule.

“Aliporudi kutoka safari Shinyanga akakuta mtoto hajapatikana na shule haijatoa taarifa polisi yaani hata wasiwasi hawana. Ikabidi yeye aende kutoa ripoti Kituo cha Polisi cha Stakishari, waliniponipa taarifa mimi nikafunga safari mpaka shuleni.

“Pale shuleni nikamkuta mkuu wa shule anaitwa Reca Ntipoo, akanijibu mtoto alitoroka shule usiku hajarudi na hawajui alipokwenda. Nikauliza kama wamefanya jitihada zozote za kumtafuta na kama wameisha ripoti polisi akasema hilo ni jukumu letu wazazi.

“Sasa hapo nikakasirika nikamuuliza mtoto tumemkabidhi shule na ada tumelipa kumbe katoroka zaidi ya mwezi hata taarifa polisi hawajatoa, hapo akajibu labda tukamtafuta kwenye vijiwe vyao vya usiku wakitoroka huwa wanakwenda huko ambako wanafunzi wenzake wanavijua, akamuuita mwanafunzi mmoja kweli akatuelekeza huko wanakokwenda usiku.

“Nilikuwa na rafiki yangu alinisindikiza tukaenda kumtafuta huko hatukumpata, hatukuwa na jinsi ikatubidi sisi tukatoe taarifa nyingine kituo cha Polisi Goba na polisi tulipowaelezea nao walishangaa  kweli kweli.

“Sasa RB tunayo ni STK/RB/10714/2020 na mpelelezi wa shauri hilo ni Afande Gwake Mwakapande. Sidhani kama yupo hai sisi tunaamini ameishakufa lakini uongozi wa shule hii ndiyo umetuulia mtoto wetu. Polisi wanajua sasa sijui kama wameishawauliza au bado,” alisema Maduhu.

Alipoulizwakwa simu yake ya kiganjani, Afande Mwakapande kama analifahamu suala hilo alisema ni kweli faili la uchunguzi la kupotea kwa mtoto huyo analishughulikia yeye lakini yuko kwa kinyozi ananyoa nywele hivyo akimaliza atapiga simu  kuelezea alipofikia katika upelelezi wake, jambo ambalo hakulitekeleza.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment