banner

Friday, September 25, 2020

DK. TULIA- SAFARI HII TUNALALA TUNAPOKULA

 



NA MWANDISHI WETU

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk.Tulia Ackson jana amepiga hodi katika Kata ya Sinde kuomba kura huku akiwa amebeba ujumbe unawaotaka wananchi wa jimbo hilo kulala wanapokula.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi, Dk Tulia amesema watu waliozowea kula kwa dada na kulala kusikojulikana waanze kujiandaa kwenda kulala wanakokula.

Dk Tulia amewaomba wananchi wa Kata ya Sinde kukipa ridhaa ya uongozi CCM kwa kipindi kingine cha miaka mitano kwa kumchagua Rais John Pombe Magufuli kuwa Rais, kumchagua yeye kuwa Mbunge na pia kuwachagua madiwani wa CCM.

Amesema  wananchi wa Kata ya Sinde wana kila sababu ya kumchagua Rais Magufuli katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu ili apate fursa ya kukamilisha kazi kubwa na ya kutukuka anayolifanyia taifa.

"Ninapokuja hapa kwenu ndugu zangu mimi siyo mgeni, kuna watu wanasikika huko wakisema kwamba tunakula kwa dada halafu tutalala sijui wapi… safari hii tunalala tulipokula. Kura yetu safari hii tutaipeleka kwenye maendeleo na maendeleo safari hii hapa Mbeya ni CCM tu.

“Mpaka hapa ninapozungumza na nyie baada ya kushuhudia mafuriko ya watu waliojitokeza kuungana nasi katika maeneo ya Kata za Nzovwe, Isyesye, Igawilo, Sinde na mahali kwengineko mimi mbunge wa kujiongeza nilishafanya 'connection'.

"Hapa ninapozungumza, mipango kazi ipo tayari, watu wanafanya usanifu ili miundombinu yetu ikae sawa.

“Watu wa Mbeya safari hii tunaenda kwa kasi ya kujiongeza na kasi hii inatoka Chama Cha Mapinduzi pekee, pigieni kura zote CCM mjionee maendeleo yatakavyoinuka kwa kasi ya ajabu. Mtu akija kwenu kuwapiga propaganda muulizeni umetufanyia nini kabla ya kuja hapa kuomba kura?” Dk. Tulia.

IRUGWA KUPATA KITUO CHA AFYA

 



NA MWANDISHI WETU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itajenga kituo kipya cha afya katika Kata ya Irugwa, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza ili kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu wananchi wa kata hiyo kufuata huduma za kitabibu

Akizungumza leo na wakazi wa Kata ya Irugwa wakati wa mkutano wa kumuombea kura mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais John Magufuli, amesema uamuzi huo unakwenda sambamba na ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya 2020 - 2025.

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, amesema  katika ilani ya uchaguzi ya 2020-2025, ukurasa wa 186 unasomeka, "hadi  kufikia 2025 serikali itaongeza vituo vya kutolea huduma za afya kwa asimilia 20 ya vituo 8,446 vilivyopo sasa; vipaumbele vitawekwa  katika ujenzi wa vituo vya afya na ukamilishwaji wa maboma kwa kuzingatia uwiano wa kijiografia, idadi ya watu na wingi wa wagonjwa."

Amesema Serikali ya Rais Magufuli imekwishatoa sh milioni 49.2 kwa ajili ya ujenzi wa jengo moja la kujifungilia  katika zahanati Irugwa.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi, alisema ilani imeweka mipango imara ya kushughulikia upatikanaji wa maji vijijini kama hatua ya kutekeleza azma ya Rais Magufuli  ya kumtua mama ndoo kichwani.

Kuhusu usafiri wa majini, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ya CCM ikiingia madarakani inakusudia kujenga vivuko mbalimbali kikiwemo kivuko cha Irugwa, Murtanga, Gana, Kakakuru na Lugezi hadi Kisorya.

" Kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya CCM, ukurasa wa 83 hadi 84, Chama Cha Mapinduzi kimeielekeza serikali ikamilishe ujenzi wa vivuko vipya nane kikiwemo cha Irugwa - Murutanga wilayani Ukerewe.

"Pia ilani imeelekeza serikali ianze kutekeleza mradi wa ujenzi wa maegesho ya Lugezi - Kisorya mkoani Mwanza, Kome na Nyakalilo mkoani Mwanza, Utete huko Pwani, Chato- Nkome huko Geita, Iramba na Majita mkoani Mwanza na Irugwa," alisema.

 

DMO MANYONI ASEMA UJENZI ZAHANATI YA NTOPE HAUJAKAMILIKA TANGU 2012

 

Jengo la Zahanati ya Kijiji cha Ntope  kilichopo Kata ya Sanza, Wilaya ya Manyoni, Mkoa wa Singida ambalo ujenzi wake ulianza 2013. Mradi huu unadaiwa kughubikwa na vitendo vya ufisadi

NA MWANDISHI WETU

MGANGA Mkuu wa Wilaya ya Manyoni (DMO) Furaha Mwakafula amesema ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ntope kilichopo Kata ya Sanza, Wilaya  ya Manyoni mkoani Singida haujakamilika kwa miaka minane sasa kutokana na ukosefu wa fedha.

Mwakafula ameyasema hayo leo wakati wa mahojiano na TANZANIA PANORAMA kuhusu kukwama kwa ujenzi wa zahanati hiyo na madai ya ufisadi dhidi ya fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi huo.

Amesema mbali na zahanati hiyo, ujenzi wa nyumba ya daktari wa kijiji ulikamilika na ilianza kutumiwa na mtumishi ambaye hakuwa wa kada ya afya aliyepewa na uongozi wa kijiji.

"Taarifa nilizonazo mimi ni kwamba ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwaka 2012, katika bajeti ya mwaka 2012/2013 zilitolewa sh milioni 20 zikatumika kujenga sehemu ya boma ambalo halikukamilika na tangu wakati huo haijatolewa fedha nyingine. Kwa hiyo ujenzi umekwama kwa miaka yote hiyo kwa sababu ya ukosefu wa fedha," alisema Mwakafula.

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa zilitolewa sh milioni 60 ila zilizoelekezwa kwenye ujenzi ni sh milioni 20 huku sh milioni 40 zikihamishiwa kwenye fungu lisilojulikana na hazijapata kurejeshwa hadi sasa alisema hizo zinaweza kuwa hisia za watu au upotoshaji wa makusudi.

"Kuna mambo mawili hapo ambayo ni vizuri yaeleweke, moja ni kwamba kuna fungu la fedha kutengwa kwenye bajeti na kuna fungu la fedha husika kupelekwa na kupokelewa kwenye mradi. Sasa mimi nimethibitishiwa na wataalamu wa mipango kuwa fedha iliyotolewa na kutumika kwenye mradi huo ni sh milioni 20 tu," alisema Mwakafula.



Aidha mganga mkuu huyo alisema mradi mwingine wa ujenzi wa nyumba ya daktari ulioanza sambamba na zahanati ya Ntope ulikamilika na uongozi wa Kijiji cha Ntope uliitoa nyumba hiyo itumiwe na mtumishi wa serikali ambaye hakuwa wa kada wa afya hadi ilipoharika paa.

"Kuhusu nyumba ya daktari yenyewe ilikamilika na uongozi wa kijiji uliitoa kwa mtumishi ambaye hakuwa wa kada ya afya. Huyo aliitumia hadi ilipoezuka paa lake. Hivi sasa ndiyo tunafikiria kuitengeza ili ianze kutumika kama zahanati ya kijiji," alisema.

Aidha, Mwakafula alisema taarifa kuwa zahanati ya Kijiji cha Ntope ambayo haijawahi kutoa huduma hupewa mgao wa dawa kutoka MSD ni za kweli na dawa hizo huwa zinaelekezwa zahanati za jirani ambazo zinawahudumia wananchi wa Kijiji cha Ntope.

" Hilo kweli fungu la fedha za dawa katika zahanati ya Ntope huwa linatoka kila mwaka lakini kwa sababu haipo fedha hizo huwa zinaelekezwa zahanati za jirani ambazo zinatoa huduma kwa wananchi wa Kijiji cha Ntope," alisema.

Daktari Mwakafula amefanya mahojiano na TANZANIA PANORAMA na kutoa ufafanuzi huo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Jackson kueleza kuanza kuwa anafuatilia madai ya ufisadi katika mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ntope.

SERIKALI YATUMIA BIL 3.29 KUKARABATI SHULE ZA MSINGI


 

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imetumia shilingi bilioni 3.29 kukarabati na kugharamia shughuli za utawala, michezo, mitihani na posho kwa maafisa elimu kata na walimu wakuu kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2019/2020.

Fedha hizo zimetolewa na serikali kupitia mpango wa elimu bila malipo unaotekelezwa na Serikali ya Rais John Pombe Magufuli ambao hadi sasa umezinufaisha pia shule za sekondari 23.

Hayo yameelezwa jana na Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika majukwaa ya kisiasa wilayani Ukerewe ambako amefika akiwa katika mfululizo wa ziara zake nchi nzima za kumnadi mgombea urais wa CCM, Rais John Magufuli.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema katika utekelezaji wa mfumo wa uboreshaji wa miundombinu ya shule wa lipa kutokana matokeo (EP4R) ulioanza kutekelezwa 2015 hadi 2020, sh milioni 309 zilitolewa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya madarasa, vyoo na ofisi kwa shule mbalimbali zikiwemo Kalandero, Murutunguru na Kakerege.

Alisema kiasi kingine cha sh milioni 873 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa, vyoo na maabara kwa shule za sekondari mbalimbali nchini zikiwemo Bukongo, Pius Msekwa, Bwisya, Muruti na Lugongo.

Ziara hiyo ya Waziri Mkuu Majaliwa ilimfikisha katika Kisiwa cha Bwisya kilichoko Kisiwa cha Ukara ambako alitembelea Kituo cha Afya cha Bwisya na kukagua wodi ya wanaume na ya Wazazi.

Kabla ya kukagua kituo hicho, Waziri Mkuu Majaliwa alifika kwenye mnara wa kumbukumbu ya watu waliokufa kwenye ajali ya kivuko cha MV Nyerere, Septemba 20, 201  ilikofanyika ibada fupi ya kuwaombea marehemu ikiongozwa na Padre Peter Paul wa Parokia ya Nyamwaga, Ukere na Sheikh Mudhakiru Maguza wa Msikiti wa Bwisya

ACT WAZALENDO CHAMKINGIA KIFUA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD

 



NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo) kimemwandikia barua msajili wa vyama vya siasa, kikijibu barua yake iliyotaka kujieleza kwa kukiuka masharti ya kifungu cha 11 A cha sheria ya vyama vya siasa kikimtaka arejee na kufahamu tafasiri sahihi ya kifungu hicho.

Barua hiyo ya Septemba 24, 2020 yenye kumbukumbu namba ACT/HQ/MSJ/023/Vol.III/248 inamtaka msajili afahamu maana,  tafasiri sahihi na tofauti ya vyama kuungana chini ya kifungu hicho na mgombea mmoja kuonyesha imani yake kwa mgombea mwingine katika uchaguzi mkuu.

Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo imesainiwa na Jaran Bashange kwa niaba ya katibu mkuu, mgombea mmoja kuonyesha imani kwa mgombea mwingine ni jambo la kupigiwa mfano kwa siasa za Tanzania kuwa licha ya ushindani wa kisiasa, umoja na mshikamano kama Watanzania unadumishwa.

Sehemu ya barua hiyo ambayo TANZANIA PANORAMA imeoina inasomeka; 'nakiri kupokea barua yako ya tarehe 22 Septemba, 2020 yenye kumbukumbu namba HA.322/362/21/90 inayotutaka tuwasilishe maelezo juu ya mgombea wetu wa urais wa Zanzibar, Mheshimiwa Seif Sharif Hamad kumuombea kura mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tundu Antipas Lissu

'Katika barua yako umetukumbusha uwepo wa kifungu cha 11 A cha sheria ya vyama vya siasa kinachoweka utaratibu wa vyama "kushirikiana" na ukaenda mbali kuwa  kwa vyama kushirikiana bila kufuata utaratibu uliowekwa ni kukiuka sheria.



'Tunapenda kueleza kuwa mgombea wetu wa urais wa Zanzibar, mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad hajakiuka kifungu cha 11 A cha sheria ya vyama kinachoweka utaratibu wa vyama kuungana au vinavyokusudia kuungana kabla au baada ya uchaguzi.

'Aidha, mheshimiwa Seif Sharif Hamad hakumuombea kura ndugu Tundu Antipas Lissu kama inavyodaiwa na ofisi yako. Video clip uliyotutumia haina maneno hayo na nikuombe urejee kuisikiliza upya kwa makini .

'Alichokisema mgombea wetu ni imani yake kuwa ndugu Tundu Antipas Lissu atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jambo ambalo liko wazi sana kutokana na mwelekeo wake wa kuungwa mkono na Watanzania walio wengi.

'Hii inathibitishwa na namna wananchi wengi na kwa hamasa kubwa wanavyojitokeza katika mikutano yake ya kampeni inayoendelea. Hilo si kosa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa.

'Kauli na imani hiyo haina tafasiri ya kuungana kwa vyama vyetu vya Alliance for Change and Transparent (ACT Wazalendo) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ila chama chetu kina Imani kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Chama Cha Mapinduzi, Ndugu John Pomne Magufuli hatakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya uchaguzi wa tarehe 28 Oktoba, 2020.'

Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa ilikiandikia ACT ikikitaka kitoe Maelezo kuhusu hatua ya Maalim Seif kumuombea kura mgombea urais wa Chadema, Lissu.