banner

Monday, November 30, 2020

JWTZ, TISS KUOMBWA KUMSAKA MWANAFUNZI ALIYEPOTEA ST MARY’S

 


NA MWANDISHI WETU

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) wataombwa kumsaka mwanafunzi aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde, Labna Said Salim ambaye ametoweka tangu Oktoba 4, 2020.

Taarifa iliyotolewa na Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kinondoni, Joseph Kapere kwa Tanzania PANORAMA Blog leo, imeeleza kuwa taasisi hizo zitaombwa kusaidia kumsaka mwanafunzi huyo popote alipo baada ya jitihada za Jeshi la Polisi kumsaka kushindwa kuzaa matunda.

Kapere ambaye alikuwa akizungumzia mwenendo wa uchunguzi wa timu ya maafisa wanne wa serikali iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo kuchunguza mazingira ya kutoweka kwa mwanafunzi huyo na kumsaka mahali alipo, ameeleza kuwa tume hiyo imekwishamkamata kijana anayedaiwa kuishi na mwanafunzi huyo baada ya kutoroka shuleni na sasa inasubiri wanafunzi wa kidato cha nne wamalize mitihani ya taifa ili iweze kuchukua hatua zaidi.

Timu hiyo inayomsaka mwanafunzi huyo inaundwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kinondoni, Afisa Usdalama wa Wilaya ya Kinondoni, Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kinondoni na Mdhibiti Ubora wa Elimu Kanda.

“Uchunguzi wetu unaendelea lakini hatufanikiwa kumpata huyo mtoto. Tiumekwishamkamata na kumuhoji kijana ambaye inadaiwa kuwa yule mtoto alitorokea kwake, anakiri kwamba ni kweli alikwenda chumbani kwake lakini huwa anakwenda mara kwa mara na marafiki zake na kwamba aliondoka akamuacha hapo chumbani akiwa na marafiki zake.

“Lakini wale marafiki zake saba tuliowakuta nyumbani kwa baba yake mahali ambako anaishi huyo kijana wakiwa wanavuta bangi wameeleza kuwa ni kweli huyo mtoto alipotoroka shule ule usiku alikwenda kwa huyo kijana wakawa wote kabla ya kutoweka kusikojulikana,

“Na wale waliomsindikiza kwenda kwenye hiyo nyumba ambao ni wanafunzi wenzake nao tuimewahoji na wanakiri kuwa mtoto Labna alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na huyo kijana na kwamba siku hiyo walimsindikiza akaenda kwake.

“Sasa unajua wanafunzi wengi wa kidato cha nne wako kwenye mitahani, tunasubiri jumatano wamalize ili tuiwakutanishe pamoja wote tuliowahoji watueleze kwa pamoja ndipo tuchukua hatua zaidi,” alisema Kapere.

Alipoulizwa hatua zitakazochikuliwa na timu hiyo baada ya kukamilisha uchunguzi wake alisema itaandika taarifa itakayoipeleka kwa Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi lakini itaomba Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) vialikwe kusaidia kumsaka mwanafunzi huyo kutokana na jeshi la polisi kutopata mafanikio.

“Sisi tutaandika taarifa yetu na tumeishaanza kuandika, tutaeleza upungufu wote tulioubaini kwenye hiyo shule na tutatoa mapendekezo tutapeleka kwa mkuu wa wilaya ambaye ndiye aliyeunda timu hii. Lakini niseme tu moja kwa moja katika mapendekezo yetu tutashauri TISS na JWTZ waalikwe kumsaka huyu mtoto kwasababu nadhani polisi wanahitaji msaada maana mpaka sasa hawajafanikiwa,” alisema Kapere.



Mwanafunzi Labna alitoweka shuleni Oktoba 4, 2020 na taarifa za awali zilieleza kuwa alitoroka akiwa na wafunzi wanzake kwenda kwenye maeneo ya starehe na kutokomea moja kwa moja.

Zephania Maduhu ambaye ni mjomba wa mwanafunzi huyo aliyekuwa akimlipia ada ya shule aliieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa ana wasiwasi mtoto wake ameuawa kwani tangu Oktoba 4, 2020 alipopotea akiwa chini ya uangalizi wa shule, taarifa za kupotea kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake, Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa mwanafunzi huyo akiulizia kama ameishafika nyumbani jambo ambalo limekuwa liibua hisia zinazotia shaka kuhusu usalama wa mtoto huyo.

“Huyo mtoto ninamlea mimi, ninamlipia ada ya shule mimi, ni mtoto wa dada yangu, anasoma St. Mary’s, Mbezi Makonde. Oktoba 8, mwaka huu, matron wake anaitwa Sarah Murra, alimpigia simu mama yake, yaani dada yangu akimuuliza kama Labna kafika nyumbani.

 “Dada yangu ambaye wakati huo alikuwa mkoani Shinyanga akashangaa akamuuliza amefikaje nyumbani wakati yupo shule au shule zimefungwa ghafla tena? Yule matron akamjibu ametoroka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 hivyo alikuwa anataka kujua kama yupo nyumbani, dada akamwambia yeye yupo mkoani Shinyanga na anajua mtoto wake yupo shule.

 “Aliporudi kutoka safari Shinyanga akakuta mtoto hajapatikana na shule haijatoa taarifa polisi yaani hata wasiwasi hawana. Ikabidi yeye aende kutoa ripoti Kituo cha Polisi cha Stakishari, waliponipa taarifa mimi nikafunga safari mpaka shuleni.

 “Pale shuleni nikamkuta mkuu wa shule anaitwa Reca Ntipoo, akanijibu mtoto alitoroka shule usiku hajarudi na hawajui alipokwenda. Nikauliza kama wamefanya jitihada zozote za kumtafuta na kama wameisha ripoti polisi akasema hilo ni jukumu letu wazazi.

 “Sasa hapo nikakasirika nikamuuliza mtoto tumemkabidhi shule na ada tumelipa kumbe katoroka zaidi ya mwezi hata taarifa polisi hawajatoa, hapo akajibu labda tukamtafute kwenye vijiwe vyao vya usiku wakitoroka huwa wanakwenda huko ambako wanafunzi wenzake wanavijua, akamuita mwanafunzi mmoja kweli akatuelekeza huko wanakokwenda usiku.

 “Nilikuwa na rafiki yangu alinisindikiza tukaenda kumtafuta huko hatukumpata, hatukuwa na jinsi ikatubidi sisi tukatoe taarifa nyingine kituo cha Polisi Goba na polisi tulipowaelezea nao walishangaa  kweli kweli.

 “Sasa RB tunayo ni STK/RB/10714/2020 na mpelelezi wa shauri hilo ni Afande Gwake Mwakapande. Sidhani kama yupo hai sisi tunaamini ameishakufa lakini uongozi wa shule hii ndiyo umetuulia mtoto wetu. Polisi wanajua sasa sijui kama wameishawauliza au bado,” alisema Maduhu.

 Kapere amekwishaieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa Mkuu wa Shule ya St. Mary’s, Ntipoo alikiri kufanya uzembe kutotoa taarifa polisi na kwa wazazi kuhusu kupotea kwa mwanafunzi Labna na kwamba kutoroka kwa wanafunzi usiku na kwenda kwenye maeneo ya starehe ni jambo alilolikuta shuleni hapo hivyo hata baada ya kutoonekana kwa Labna aliamini kuwa alitoroka usiku kwenda kwenye mambo yake lakini angerudi.

 Aidha Kapere amwishaeleza kuwa timu imebaini kuwa Shule ya Sekondari ya St Mary’s ni chafu, haina ulinzi wa kutosha na ukuta wake haufai.

 

 

 

KAMANDA BUKOMBE AONDOLEWA KINONDONI, APELEKWA MAKAO MAKUU


NA MWANDISHI WETU

ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni (RPC), Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Edward Bukombe, amehamishwa kituo chake cha kazi na kupelekwa makao makuu.   

Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog kutoka vyanzo vyake vya habari zimeeleza kuwa Kamanda Bukombe sasa anakwenda kuongoza kitengo cha picha na matukio na kwamba uhamisho huo ni wa kawaida.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, nafasi ya Kamanda Bukombe imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ramadhani Kingai ambaye katika mahojiano yake leo na Tanzania PANORAMA Blog amethibitisha kurithi wadhfa huo akitokea mkoani Arusha.  

Thursday, November 26, 2020

WAZABUNI WANAOIDAI TAMESA WAOMBA MSAADA WA WAZIRI MKUU


NA MWANDISHI WETU

WAZABUNI waliosambaza vipuli na kutengeneza magari ya Wizara na Idara za Serikali kupitia Karakana Kuu ya Temesa - MT Depot, wamemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aingilie kati kusaidia walipwe madeni wanayodai.

Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog, Mwenyekiti wa Umoja wa Gereji Tanzania (UGETA), Lumona Mkala, alisema wanachama wake wanaidai Temesa - MT. Depot zaidi ya shilingi Bilioni nne.

Mkala amesema kwa nyakati tofauti wamefuatilia kulipwa fedha zao bila mafanikio na wakati mwingine wanapewa  majibu yasiyoonyesha ushirikiano kutoka Ofisi ya Meneja wa MT Depot, Injinia Joseph Maronga.

"Unapofika ofisi ya meneja, unaambiwa nenda kwa mhasibu, ukifika kwa mhasibu anakwambia urudi kwa Meneja...Hivyo tunakuwa hatuna majibu ya lini pesa zetu tutalipwa," amesema Mkala.

Amezitaja baadhi ya gereji zinazodai kuwa ni Beka Investment shilingi 250,563,150, Moroturbo shilingi 80,256,197, Planet Busines link shilingi 175,312,570 na Ndeken shipingi 194,801,393

Nyingine ni Kigustar Enterprisess,  Leonardo Automotive Garage, Nedea Enterprisess, RaaR Investment, Kigoma Garage, Adam Motor na Point A.

Mkala amesema wamelazimika kumuomba Waziri Mkuu aingilie kati baada ya hatua alizozianza mwanzoni mwa mwaka huu,  kuzitaka wizara na idara za serikali ambazo ndizo zilizohudumiwa na gereji hizo!kulipa madeni yao wanayodaiwa kushindwa kufanikiwa.

"Hizi Idara na wizara tulizozihudumia tunazo taarifa kwamba baada ya agizo la Waziri Mkuu wamelipa fedha lakini Meneja wa MT Depot hataki kutulipa," amesema.

Alipotafutwa kuzungumzia madai hayo, Meneja wa MT Depot, Injinia Maronga, amesema yeye siyo msemaji wa taasisi hiyo na kumuelekeza mwandishi wa habari hizi kumtafuta Ofisa Habari ya Temesa, Theresia Mwami.

Mwami alipotafuta na kuulizwa kuhusu madai hayo, alisema hana majibu na kumtaka mwandishi awasiliane na Mtendaji Mkuu wa Temesa Dk. Stephen Masele.

Mtendaji wa Temesa alipotafutwa na kuulizwa kuhusu madeni hayo,  alikiri taasisi hiyo kudaiwa lakini alitaka mwandishi apate  nafasi ya kumfafanulia madeni hayo.

"Nipo Dodoma kuna vikao tunaendelea navyo, nitakupigia baadaye au njoo Dodoma," amrsema Masele.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana kutoka Ofisi za Mhasibu Mkuu wa MT Depot zimedai kuwa fedha zilizokusanywa hazizidi shilingi milioni 500 ambapo Temesa wameziweka  wakisubiri maelekezo ya Waziri Mkuu ili waweze kuwalipa wazabuni hao.

"Kiukweli hili suala ni dogo sana, lakini mtendaji wetu anasubiri kupata maelekezo ya nani  na nani alipwe, " alisema  na kuongeza,  "Temesa kama Temesa na sisi tunazidai hizo Idara na Wizara za serikali karibu Shilingi billion 5.

Wazabuni hao, wanalalamika kuwa kutolipwa madeni yao tangu  2016 kunasababisha washindwe kujiendesha kwa vile nao wanadaiwa fedha nyingi  na taasisi za fedha.

ANAYETUHUMIWA KUMTOROSHA MWANAFUNZI ST MARY'S MBARONI

NA MWANDISHI WETU

MAKACHERO wa Jeshi la Polisi wamemkamata Rahim Nyamka kwa tuhuma za kumtorosha na kumuachisha masomo, mwanafunzi Labna Said Salim anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary's iliyoko Mbezi Makonde.

Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania PANORAMA kutosha ndani ya timu ya maafisa wanne waandamizi wa serikali Wilaya ya Kinondoni inayomsaka Labna zimeeleza kuwa Nyamka alikamatwa Juzi, Novemba 24 na kuhojiwa kabla ya kupendekezwa na timu hiyo kuwa asipewe dhamana.

Timu inayomsaka Labna ambaye alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 inaundwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kinondoni, Afisa wa Usalama wa Wilaya, Afisa Elimu Sekondari na Mthibiti Elimu Kanda.

Taarifa kutoka ndani ya timu ya uchunguzi zimeeleza kushangazwa na uamuzi wa polisi kutozingatia maelekezo ya timu ya uchunguzi ya kutompatia dhamana mtuhumiwa huyo.

"Tumemsaka huyo mtuhumiwa mpaka tumempata, tulimkamata tukiwa na askari wapelelezi tukampeleka kituo cha Polisi Goba ambako ndiko kesi ilikofunguliwa, huko tulimuhoji kisha tukawaachia polisi lakini tuliwaambia wasimwachie kulingana na mwenendo wa uchunguzi wa shauri hili.

" Ajabu tulipoondoka wakampa dhamana. Hili jambo limetushangaza hata sisi kwani tumeshindwa kujua kuna nini kinaendelea pale Polisi Goba lakini wapo wenzangu wa vyombo vya ulinzi na usalama ndani ya timu nao wameliona hili na limewashangaza pia naamini watalifanyia kazi, alisema mmoja wa wajumbe wa timu hiyo.

Akizungumzia mwenendo wa uchunguzi ulipofikia alisema Labna bado hajapatikana na baada ya kuhojiwa kwa Nyamka alikana kumtorosha au kuwa naye.

"Bado aisee, yule mtuhumiwa Nyamka amekana tuhuma zote lakini vijana sita tuliowakamata wakivuta bangi ndani ya nyumba ya baba yake Nyamka ambaye Kamishna Mstaafu Magereza wamekiri katika mahojiano kuwa Labna alifika kwenye hiyo Nyumba na alikuwa anawapikia na walipata kumvutisha bangi.

" Mbali na hao, wale vijana waliomsadia kuruka ukuta nao wamekiri kuwa ni kweli walitenda tukio hilo. Tatizo kuna mambo ambayo timu inapigana kuyabaini lakini huko chini kuna watu wanavuruga," alisema.

Jitahidi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuwa inaita  bila kupokelewa.

Labna alitoweka shuleni Oktoba 4, mwaka huu lakini uongozi wa shule ya St Mary's alificha taarifa za kutoweka kwake hadi Oktoba 8, 2020 ambapo Matroni wake anayefamika kwa jina la Sarah Murra alipompigia simu yake mama yake kumuiliza kama yupo nyumbani.

Mkuu wa Shule ya St. Mary's Sekondari, Reca Ntipoo amekaririwa na timu ya uchunguzi akiungama kuwa uongozi wa shule ulifanya makosa kutotoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mtoto huyo.

Ntipoo pia alieleza timu hiyo kuwa alipohamishiwa shuleni hapo alikuta wanafunzi hao wakitoroka usiku na kurudi alfajili jambo lilimjanisha kuwa hata Labna baada ya kutoroka angerudi kwa sababu kitendo hicho ni kawaida shuleni hapo.

Aidha uchunguzi wa awali wa timu umebaini kuwa shule hiyo imepungukiwa sifa kwa sababu ni chafu, haina ulinzi wa kutosha na uzio wake (ukuta) siyo imara.

Timu hiyo pia ilibaini vijana saba waliokuwa wakivuta bangi nyumbani kwa Kamishna Mstaafu wa Jeshi Magereza na pia ndani ya ua wa nyumba kulikuwa na shamba la bangi. Nyumba hiyo ndiyo anayoishi Rahim na ndugu yake.

Tuesday, November 24, 2020

WALIOFICHA SARUJI KUSAKWA MKOA KWA MKOA



*Waziri Mkuu Majaliwa awaagiza MA RC kuwakagua mawakala, wauzaji wa kati na wadogo

NA MWANDISHI MAALUM

SERIKALI sasa imeanza kuchukua hatua mahususi za kupambana na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu walioficha saruji kwa lengo la kuleta taharuki katika nchi.

Hatua hizo zimetangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kuwaagiza wakuu wa mikoa yote nchini kufanya ukaguzi kwenye viwanda vya kuzalisha saruji, kwa mawakala na wauzaji wa kati na wadogo.

Waziri Mkuu Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa kuwachukulia hatua stahiki wale wote watakaobainika kuficha saruji katika msako watakaoufanya.

Agizo hilo alilitoa alippkuwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa yote nchini kuhusu tatizo la kupanda kwa bei ya saruji, kwenye kikao alichokiendesha kwa njia ya video (video conferencing) kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

"Wakuu wa Mikoa na Kamati zenu za Ulinzi na Usalama fanyeni ukaguzi kwa mawakala, ukikuta wamerundika saruji kamata na kuwashtaki. Nendeni pia kwa wauzaji wa kati, nao pia chekini maghala yao.

“Piteni kwa maafisa biashara na muwasimamie iwe ni kwenye Sekretarieti za Mikoa au katika Halmashauri zenu, tunataka bei irudi kama ilivyokuwa mwezi Septemba kwa sababu hakuna badiliko lolote kwenye tozo ya kodi,” alisisitiza.

Agizo hili la kupambana na walanguzi wa saruji limetolewa na Waziri Mkuu Majaliwa katika kikao chake cha kwanza na Wakuu wa Mikoa tangu alipoapishwa kushika wadhfa huo kwa mara pili.

"Wakati wa uapisho, Novemba 16, mwaka huu nilitambulisha tatizo la kupatikana saruji kwa bei ya juu sana. Niliagiza kila Mkuu wa Mkoa afuatilie ni kwa nini bei imepanda kiasi hicho.

"Nimepokea taarifa zenu na kuona hali halisi iliyoko kwenye mikoa yenu. Hali si nzuri, akiba iliyopo ni ndogo na bei ni ya juu sana. Nasema bei ni ya juu sababu tunaangalia bei ya mlaji kwa sasa. Awali ilikuwa kati ya sh. 14,000 hadi 15,000 lakini sasa hivi imefikia sh. 24,000 kwa mfuko mmoja,” alisema.



Waziri Mkuu Majaliwa alisema hiyo ni tofauti ya sh. 9,000 hadi 10,000 lakini kwa sasa ni lazima bei ishuke kwa sababu hakuna tozo za kodi zilizoongezeka.

“Kuna watu wanatumia kigezo cha gharama za usafirishaji, hii si kweli kwani hata Septemba, walikuwa wakisafirisha bidhaa hiyo kwa njia zetu zile zile," alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali ya awamu ya tano imekuwa ikihimiza ujenzi wa viwanda ili bidhaa zinazozalishwa nchini zipatikane kwa wingi. “Kwenye saruji malighafi ziko nchini, hazitoki nje, kwa hiyo tunataraji upatikanaji wake uwe rahisi na bei ingekuwa nafuu," alisema.

Aidha, aliwaagiza wakurugenzi wa Wizara ya Viwanda na Biashara wakutane na wenye viwanda na kuweka ratiba ya mwaka ili kuepuka viwanda vingi kufungwa kwa matengenezo ya mwaka kwa wakati mmoja na kufanya saruji iadimike na kupandisha ghafla bei ya saruji.

Vilevile, aliwaagiza viongozi wa Tume ya Ushindani (FCC) wafuatilie wamiliki wenye viwanda vya saruji na wafanye uchunguzi kubaini uhalali wa bei zinazopangwa na mawakala na wafanyabiashara wa saruji nchini.  Pia akawataka wawasisitizie wazingatie sheria za nchi.

Kwa upande wao, wakuu wa mikoa walisema wamepokea maelekezo na watayatekeleza.

Mkutano huo uliwashirikisha pia Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara za Viwanda na Biashara; Uchukuzi na watendaji kutoka Tume ya Ushindani.