banner

Thursday, November 26, 2020

WAZABUNI WANAOIDAI TAMESA WAOMBA MSAADA WA WAZIRI MKUU


NA MWANDISHI WETU

WAZABUNI waliosambaza vipuli na kutengeneza magari ya Wizara na Idara za Serikali kupitia Karakana Kuu ya Temesa - MT Depot, wamemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aingilie kati kusaidia walipwe madeni wanayodai.

Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog, Mwenyekiti wa Umoja wa Gereji Tanzania (UGETA), Lumona Mkala, alisema wanachama wake wanaidai Temesa - MT. Depot zaidi ya shilingi Bilioni nne.

Mkala amesema kwa nyakati tofauti wamefuatilia kulipwa fedha zao bila mafanikio na wakati mwingine wanapewa  majibu yasiyoonyesha ushirikiano kutoka Ofisi ya Meneja wa MT Depot, Injinia Joseph Maronga.

"Unapofika ofisi ya meneja, unaambiwa nenda kwa mhasibu, ukifika kwa mhasibu anakwambia urudi kwa Meneja...Hivyo tunakuwa hatuna majibu ya lini pesa zetu tutalipwa," amesema Mkala.

Amezitaja baadhi ya gereji zinazodai kuwa ni Beka Investment shilingi 250,563,150, Moroturbo shilingi 80,256,197, Planet Busines link shilingi 175,312,570 na Ndeken shipingi 194,801,393

Nyingine ni Kigustar Enterprisess,  Leonardo Automotive Garage, Nedea Enterprisess, RaaR Investment, Kigoma Garage, Adam Motor na Point A.

Mkala amesema wamelazimika kumuomba Waziri Mkuu aingilie kati baada ya hatua alizozianza mwanzoni mwa mwaka huu,  kuzitaka wizara na idara za serikali ambazo ndizo zilizohudumiwa na gereji hizo!kulipa madeni yao wanayodaiwa kushindwa kufanikiwa.

"Hizi Idara na wizara tulizozihudumia tunazo taarifa kwamba baada ya agizo la Waziri Mkuu wamelipa fedha lakini Meneja wa MT Depot hataki kutulipa," amesema.

Alipotafutwa kuzungumzia madai hayo, Meneja wa MT Depot, Injinia Maronga, amesema yeye siyo msemaji wa taasisi hiyo na kumuelekeza mwandishi wa habari hizi kumtafuta Ofisa Habari ya Temesa, Theresia Mwami.

Mwami alipotafuta na kuulizwa kuhusu madai hayo, alisema hana majibu na kumtaka mwandishi awasiliane na Mtendaji Mkuu wa Temesa Dk. Stephen Masele.

Mtendaji wa Temesa alipotafutwa na kuulizwa kuhusu madeni hayo,  alikiri taasisi hiyo kudaiwa lakini alitaka mwandishi apate  nafasi ya kumfafanulia madeni hayo.

"Nipo Dodoma kuna vikao tunaendelea navyo, nitakupigia baadaye au njoo Dodoma," amrsema Masele.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana kutoka Ofisi za Mhasibu Mkuu wa MT Depot zimedai kuwa fedha zilizokusanywa hazizidi shilingi milioni 500 ambapo Temesa wameziweka  wakisubiri maelekezo ya Waziri Mkuu ili waweze kuwalipa wazabuni hao.

"Kiukweli hili suala ni dogo sana, lakini mtendaji wetu anasubiri kupata maelekezo ya nani  na nani alipwe, " alisema  na kuongeza,  "Temesa kama Temesa na sisi tunazidai hizo Idara na Wizara za serikali karibu Shilingi billion 5.

Wazabuni hao, wanalalamika kuwa kutolipwa madeni yao tangu  2016 kunasababisha washindwe kujiendesha kwa vile nao wanadaiwa fedha nyingi  na taasisi za fedha.

ANAYETUHUMIWA KUMTOROSHA MWANAFUNZI ST MARY'S MBARONI

NA MWANDISHI WETU

MAKACHERO wa Jeshi la Polisi wamemkamata Rahim Nyamka kwa tuhuma za kumtorosha na kumuachisha masomo, mwanafunzi Labna Said Salim anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary's iliyoko Mbezi Makonde.

Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania PANORAMA kutosha ndani ya timu ya maafisa wanne waandamizi wa serikali Wilaya ya Kinondoni inayomsaka Labna zimeeleza kuwa Nyamka alikamatwa Juzi, Novemba 24 na kuhojiwa kabla ya kupendekezwa na timu hiyo kuwa asipewe dhamana.

Timu inayomsaka Labna ambaye alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 inaundwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kinondoni, Afisa wa Usalama wa Wilaya, Afisa Elimu Sekondari na Mthibiti Elimu Kanda.

Taarifa kutoka ndani ya timu ya uchunguzi zimeeleza kushangazwa na uamuzi wa polisi kutozingatia maelekezo ya timu ya uchunguzi ya kutompatia dhamana mtuhumiwa huyo.

"Tumemsaka huyo mtuhumiwa mpaka tumempata, tulimkamata tukiwa na askari wapelelezi tukampeleka kituo cha Polisi Goba ambako ndiko kesi ilikofunguliwa, huko tulimuhoji kisha tukawaachia polisi lakini tuliwaambia wasimwachie kulingana na mwenendo wa uchunguzi wa shauri hili.

" Ajabu tulipoondoka wakampa dhamana. Hili jambo limetushangaza hata sisi kwani tumeshindwa kujua kuna nini kinaendelea pale Polisi Goba lakini wapo wenzangu wa vyombo vya ulinzi na usalama ndani ya timu nao wameliona hili na limewashangaza pia naamini watalifanyia kazi, alisema mmoja wa wajumbe wa timu hiyo.

Akizungumzia mwenendo wa uchunguzi ulipofikia alisema Labna bado hajapatikana na baada ya kuhojiwa kwa Nyamka alikana kumtorosha au kuwa naye.

"Bado aisee, yule mtuhumiwa Nyamka amekana tuhuma zote lakini vijana sita tuliowakamata wakivuta bangi ndani ya nyumba ya baba yake Nyamka ambaye Kamishna Mstaafu Magereza wamekiri katika mahojiano kuwa Labna alifika kwenye hiyo Nyumba na alikuwa anawapikia na walipata kumvutisha bangi.

" Mbali na hao, wale vijana waliomsadia kuruka ukuta nao wamekiri kuwa ni kweli walitenda tukio hilo. Tatizo kuna mambo ambayo timu inapigana kuyabaini lakini huko chini kuna watu wanavuruga," alisema.

Jitahidi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuwa inaita  bila kupokelewa.

Labna alitoweka shuleni Oktoba 4, mwaka huu lakini uongozi wa shule ya St Mary's alificha taarifa za kutoweka kwake hadi Oktoba 8, 2020 ambapo Matroni wake anayefamika kwa jina la Sarah Murra alipompigia simu yake mama yake kumuiliza kama yupo nyumbani.

Mkuu wa Shule ya St. Mary's Sekondari, Reca Ntipoo amekaririwa na timu ya uchunguzi akiungama kuwa uongozi wa shule ulifanya makosa kutotoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mtoto huyo.

Ntipoo pia alieleza timu hiyo kuwa alipohamishiwa shuleni hapo alikuta wanafunzi hao wakitoroka usiku na kurudi alfajili jambo lilimjanisha kuwa hata Labna baada ya kutoroka angerudi kwa sababu kitendo hicho ni kawaida shuleni hapo.

Aidha uchunguzi wa awali wa timu umebaini kuwa shule hiyo imepungukiwa sifa kwa sababu ni chafu, haina ulinzi wa kutosha na uzio wake (ukuta) siyo imara.

Timu hiyo pia ilibaini vijana saba waliokuwa wakivuta bangi nyumbani kwa Kamishna Mstaafu wa Jeshi Magereza na pia ndani ya ua wa nyumba kulikuwa na shamba la bangi. Nyumba hiyo ndiyo anayoishi Rahim na ndugu yake.

Tuesday, November 24, 2020

WALIOFICHA SARUJI KUSAKWA MKOA KWA MKOA



*Waziri Mkuu Majaliwa awaagiza MA RC kuwakagua mawakala, wauzaji wa kati na wadogo

NA MWANDISHI MAALUM

SERIKALI sasa imeanza kuchukua hatua mahususi za kupambana na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu walioficha saruji kwa lengo la kuleta taharuki katika nchi.

Hatua hizo zimetangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kuwaagiza wakuu wa mikoa yote nchini kufanya ukaguzi kwenye viwanda vya kuzalisha saruji, kwa mawakala na wauzaji wa kati na wadogo.

Waziri Mkuu Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa kuwachukulia hatua stahiki wale wote watakaobainika kuficha saruji katika msako watakaoufanya.

Agizo hilo alilitoa alippkuwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa yote nchini kuhusu tatizo la kupanda kwa bei ya saruji, kwenye kikao alichokiendesha kwa njia ya video (video conferencing) kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

"Wakuu wa Mikoa na Kamati zenu za Ulinzi na Usalama fanyeni ukaguzi kwa mawakala, ukikuta wamerundika saruji kamata na kuwashtaki. Nendeni pia kwa wauzaji wa kati, nao pia chekini maghala yao.

“Piteni kwa maafisa biashara na muwasimamie iwe ni kwenye Sekretarieti za Mikoa au katika Halmashauri zenu, tunataka bei irudi kama ilivyokuwa mwezi Septemba kwa sababu hakuna badiliko lolote kwenye tozo ya kodi,” alisisitiza.

Agizo hili la kupambana na walanguzi wa saruji limetolewa na Waziri Mkuu Majaliwa katika kikao chake cha kwanza na Wakuu wa Mikoa tangu alipoapishwa kushika wadhfa huo kwa mara pili.

"Wakati wa uapisho, Novemba 16, mwaka huu nilitambulisha tatizo la kupatikana saruji kwa bei ya juu sana. Niliagiza kila Mkuu wa Mkoa afuatilie ni kwa nini bei imepanda kiasi hicho.

"Nimepokea taarifa zenu na kuona hali halisi iliyoko kwenye mikoa yenu. Hali si nzuri, akiba iliyopo ni ndogo na bei ni ya juu sana. Nasema bei ni ya juu sababu tunaangalia bei ya mlaji kwa sasa. Awali ilikuwa kati ya sh. 14,000 hadi 15,000 lakini sasa hivi imefikia sh. 24,000 kwa mfuko mmoja,” alisema.



Waziri Mkuu Majaliwa alisema hiyo ni tofauti ya sh. 9,000 hadi 10,000 lakini kwa sasa ni lazima bei ishuke kwa sababu hakuna tozo za kodi zilizoongezeka.

“Kuna watu wanatumia kigezo cha gharama za usafirishaji, hii si kweli kwani hata Septemba, walikuwa wakisafirisha bidhaa hiyo kwa njia zetu zile zile," alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali ya awamu ya tano imekuwa ikihimiza ujenzi wa viwanda ili bidhaa zinazozalishwa nchini zipatikane kwa wingi. “Kwenye saruji malighafi ziko nchini, hazitoki nje, kwa hiyo tunataraji upatikanaji wake uwe rahisi na bei ingekuwa nafuu," alisema.

Aidha, aliwaagiza wakurugenzi wa Wizara ya Viwanda na Biashara wakutane na wenye viwanda na kuweka ratiba ya mwaka ili kuepuka viwanda vingi kufungwa kwa matengenezo ya mwaka kwa wakati mmoja na kufanya saruji iadimike na kupandisha ghafla bei ya saruji.

Vilevile, aliwaagiza viongozi wa Tume ya Ushindani (FCC) wafuatilie wamiliki wenye viwanda vya saruji na wafanye uchunguzi kubaini uhalali wa bei zinazopangwa na mawakala na wafanyabiashara wa saruji nchini.  Pia akawataka wawasisitizie wazingatie sheria za nchi.

Kwa upande wao, wakuu wa mikoa walisema wamepokea maelekezo na watayatekeleza.

Mkutano huo uliwashirikisha pia Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara za Viwanda na Biashara; Uchukuzi na watendaji kutoka Tume ya Ushindani.

Friday, November 20, 2020

MSAKO WA LABNA WA ST MARY'S WAIBUA MADUDU YA KUTISHA, SHAMBA LA BANGI LABAINIKA NYUMBANI KWA KAMISHNA

 


NA MWANDISHI WETU

TIMU ya maafisa wanne waandamizi wa serikali iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo kumsaka mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St Mary's, aliyepotea tangu Oktoba 4, 2020 imebaini kuwa shule hiyo imepungukiwa sifa zinazostahili kisheria.

Afisa Elimu Sekondari ya Wilaya ya Kinondoni, Joseph Kapere ameyasema hayo alipokuwa akielezea mwenendo wa msako na uchunguzi wa mazingira ya kutoweka kwa mwanafunzi Labna unaofanywa na timu iliyoundwa na Chongolo.



Kapere alisema katika uchunguzi huo ulioanza jana  kwa kumuhoji Mkuu wa Shule ambaye alieleza kuwa Labna aliwaambia walimu hataki shule na alitoroka akaenda kwa rafiki yake ya kiume wakawa wanaishi pamoja.

"Tunafanya uchunguzi kwa umakini sana. Tumeishamuhoji Mkuu wa Shule na yeye ametueleza kuwa huyo mtoto alikwishawambia walimu kuwa hataki shule na aliondoka shuleni kwa kutoroka.

"Mkuu wa Shule alituambia kuwa motto alitoroka shuleni kwa kuruka ukuta usiku akisaidiwa na wanafunzi wenzake wavulana wawili, akaenda kwa boy friend wake wakaanza kuishi pamoja huko,” Kapere alimkariri mkuu wa shule.

Alisema mkuu huyo wa shule aliipeleka timu ya serikali nyumba aliyokuwa akiishi Labna na mpenzi wake baada ya kutoroka shule lakini waliwakosa na badala yake walikuta wavulana saba wakiwa wanavuta bangi.

"Mkuu wa shule anapajua alipotorokea mtoto huyo na alitupeleka kwenye hiyo nyumba. Ni nyumba ya Kamishna Mstaafu wa Magereza ambayo wanaishi watoto wake wawili lakini hapo hatukumta Labna wala boy friend wake, tulikuta vijana saba waliokuwa wanavuta bangi na nyumba nzima ilikuwa imetapakaa misokoto ya bangi.

"Kwa kweli ni hali ya kutisha sana kwa vijana wetu. Walituambia ni kweli Labna alipotoroka shule alikuwa akiishi hapo na boy friend wake na alikuwa mama wa nyumbani kwani alikuwa akiwapikia na kufanya usafi wa nyumba lakini baada ya muda kidogo aliondoka.

"Boy friend wake naye hatukumkuta, wale vijana wavuta bangi walisema anasoma chuo CBE na anaishi hostel sasa tumepeleka makachero akakamatwe huko.

“Lakini hiyo nyumba baada ya kuichunguza kwa sababu ina uzio mkubwa sana tulikuta shamba la bangi humo ndani. Yaani bangi inalimwa humo humo nyumbani kwa Kamishna wa Magereza wanavuna wanavuta hao vijana.

"Basi wale vijana tuliwachukua hadi polisi wamelala huko kwa ajili ya uchunguzi zaidi na taratibu nyingine zitafuata," alisema Kapere.

Alipoulizwa iwapo timu hiyo imebaini ni kwanini Mkuu wa Shule baada ya kuambiwa na Labna kuwa hataki shule hakuwapa taarifa wazazi na hata alipotoroka uongozi wa shule ulikaa kimywa wala haukutoa ripoti polisi, alisema mwalimu huyo amekiri kuwa yeye na wenzake walikosea.

Tanzania PANORAMA lilimuuliza pia Kapere kama timu ya serikali imebaini ni kwanini Mkuu wa Shule baada ya kubaini mwanafunzi wake ametoroka na alikuwa akiishi na mwanaume nje ya shule hakuchukua hatua za kutoa taarifa kwa wazazi na polisi ili wote wawili wakamatwe kwa kuzingatia mwanafunzi huyo wazazi wake walimkabidhi kwa uongozi wa shule, Kapere alisema swali hilo ni zuri na watamuuliza Mkuu wa Shule.

"Timu yetu ina polisi, hata nyumba ya  kamishna tuliivamia tukiwa na polisi. Polisi waliizingira kisha wakaingia ndani ndiyo wakakuta lile shamba la bangi na ile misokoto. Lakini Mwalimu anajitetea yeye ni mgemi na tabia ya watoto kutoroka usiku wakarudi alfajili aliikuta. Lakini pia mkuu wa shule alituambia kuwa awali yeye, polisi na wajomba wa huyo wa mtoto walikwenda hadi kwenye hiyo nyumba kumsaka lakini polisi na wajombe hawakuingia ndani, waliishia nje.  

"Sasa hata Labna alipotoroka Mwalimu amesema mwenyewe alijua ndiyo kawaida yao atarudu lakini kwa bahati mbaya yeye hakurudi, akahamia kabisa kwa huyo boy friend wake.

"Uchunguzi wetu sasa pale shuleni imebaini kuwa ile shule haifai, imepungukiwa sifa stahiki za kuitwa shule. Kwanza ni chafu sana, haina walinzi wa kutosha na hata ukuta wake haufai," alisema Kapere.

Alisema anaamini mtoto huyo yupo hai na atapatikana katika msako unaoendelea.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo alipoulizwa jana alisema yupo msibani hivyo hayupo katika nafasi kuzungumza.

Labna, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde Jijini Dar es Salaam alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 lakini tukio  la kutoweka kwake halikuripotiwa polisi na uongozi wa shule.

SERIKALI YAANZA MSAKO MKALI MWANAFUNZI ALIYEPOTEA ST MARY'S

 

NA MWANDISHI WETU

HATIMAYE serikali imeanzisha msako mkali wa mwanafunzi Labna Salim Said wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Bweni ya St Mary's ambaye amepotea tangu Oktoba 4, 2020 akiwa shuleni.

Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimeeeza kuwa, msako huo umeanza jana baada ya kufanyika kwa kikao cha ulinzi na usalama cha Wilaya ya Kinondoni kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Daniel Chongolo.

Chongolo ameithibitishia Tanzania PANORAMA  kuitisha na kuongoza kikao hicho na kueleza kuwa serikali imeanza kuchunguza mazingira ya tukio la kupotea kwa mwanafunzi huyo akiwa shuleni kwa kuunda kikosi maalumu kinachojumuisha vyombo vya ulinzi na usalama.

Hata hivyo, Chongolo alisema hayuko katika nafasi nzuri ya kulizunguzia suala hilo kwa sababu kuhofia kuharibu mwenendo wa uchunguzi wa timu yake aliyoiunda.

Akizungumzia hatua hiyo ya serikali kujitosa rasmi kwenye sakata la kupotea kwa mwanafunz Labna, Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kinondoni, Joseph Kapere Chongolo aliitisha kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ofisini kwake jana mchana baada ya kupokea malalamiko ya wazazi wa mtoto huyo kupotea akiwa shuleni.

Kapere alisema katika kikao hicho kilichohudhuliwa pia na wazazi wa mtoto huyo, Chongolo aliunda kamati ya watu  wanne kumsaka mtoto Labna popote alipo na kuchunguza mwenendo mzima wa tukio la  kupotea kwake.

"Hili tukio ni la aina yake lakini tunasikitika kuwa limechelewa kutufikia, hata mkuu wa wilaya kafahamu jana baada ya wazazi kumfikishia kesi hiyo. Hizo shule zipo chini yangu mimi ndiyo nashughulika nazo.

"Sasa mkuu wa wilaya aliitisha kamati ya ulinzi ya usalama na ameteua kikosi cha watu wanne kumsaka mtoto huyo.

"Walioteuliwa kwenye kikosi hicho ni viongozi waandamizi wakiwemo kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ofisi ya Afisa Usalama wa Wilaya ya Kinondoni, mimi mwenyewe Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Kinondoni," alisema Kapere.

Mwanafunzi msichana, Labna wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s alitoroka shuleni usiku na kutokomea kusikojulikana na hadi sasa hajapatikana.

Labna alitoroka Oktoba 4, 2020 akiwa chini ya uangalizi wa shule lakini taarifa za kupotea kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa Labna akiulizia kama ameishafika nyumbani.

Katika hatua ya kushangaza, uongozi wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s haukutoa taarifa polisi kuhusu kupotea kwa mwanafunzi huyo na badala yake wazazi ndiyo walioripoti tukio la mtoto wao kupotea akiwa shuleni.