banner

Thursday, November 19, 2020

FISI MADOA MNYAMA ANAYEWEKA MIPAKA YA HIMAYA YAKE KWA KINYESI CHAKE


 NA ERNEST SITTA

MAISHA ya mnyama Fisi yana mengi ya kuvutia kuyajua ambayo yanamsaidia binadamu kutambua umuhimu wa mnyama huyu katika uso wa dunia.

Fisi wamegawanyika katika makundi manne ambayo ni Fisi Madoa, Fisi Miraba, Fisi Kahawia na Fisi Aardwolf na asili yao ni familia inayofahamika kwa jina la kitaalamu la Hyenidae.

Taungalie kwanza maisha ya Fisi Madoa, mnyama anayetokea kwenye familia ya Hyenidae.

Kwa kawaida Fisi wote ni wanyama wanatokea katika kundi la wanyama walao nyama.

Fisi madoa ana urefu wa sentimita 77 kutoka mkiani hadi kwenye mabega akiwa amesimama.

Uzito wake ni kilo 63 kwa dume na jike ni kilo 68, hivyo jike ni mkubwa kuliko dume.



Fisi madoa anabeba mimba kwa muda wa miezi mitatu na nusu na huzaa watoto kuanzia mmoja mpaka wanne. Umri wake wa kuishi ni miaka 50.

Aina hii ya wanyama wanapendelea kukaa kwenye mashimo au mapango katika familia inayoongozwa na mtawala ambaye ni jike na kufuatiwa na majike daraja mbalimbali za utawala katika familia.

Sehemu hizo za mapangoni hutumika kuishi na kulea watoto wa rika mbalimbali. Jinsia ya kike hukaa katika himaya waliyozaliwa maisha yao yote lakini Fisi madume baada ya kufikia miaka minne huanza kujiandaa kuondoka kwenye familia.

Fisi madume baada ya kutimiza miaka minne hutoka na kujiunga na familia nyingine.

Fisi hawa huweka mipaka ya himaya yake kwa kutumia utomvu wenye harufu kali kutoka kwenye tezi lililomo ndani ya sehemu ya kujisaidia haja kubwa.



Mnyama huyu ni mahiri wa kuwinda, ana uvumilivu na nguvu nyingi za shingo. Umbo la fuvu la kichwa lina meno makali yenye uwezo wa kutafuna hata mifupa.

Kinyesi cha Fisi Madoa kina rangi nyeupe kama chaki au chokaa.

 Jike mtawala pamoja na watoto wake humiliki himaya na chochote kilichopo ndani ya eneo kama ni mnyama wameshirikiana kuua ndani ya himaya wa kwanza kula ni jike mtawala pamoja watoto wake, wakishatosheka ndipo Fisi wengine watafuatia kwa kuzingatia daraja mbalimbali au rika.

Chakula kisipotosha familia nzima ya Fisi wawindaji au wavizia mizoga husafiri kwenda mbali muda wa siku moja au mbili kutafuta chakula kingine cha kutosheleza kundi zima na kurudi kuwatapikia watoto wao.



Watoto wa Fisi Madoa waliozaliwa na jike mtawala wanakuwa na bahati ya kuendelea kutawala, vivyo hivyo wanaozaliwa na mama ambaye yupo daraja la chini huendelea  kutawaliwa na hawapewi kipaumbele hasa katika masuala ya chakula.

Katika jamii zetu za kiafrika hasa za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Fisi huhusishwa na imani za kishirikina na hasa wanaposikika kwa milio tofauti karibia na mazingira ya makazi ya watu.

Lakini kiuhalisia sauti za Fisi huashiria  kuomba msaada endapo mmoja ameona mawindo, mzoga au msaada kama kuna adui.

Fisi ni muhimu sana katika mapori tengefu na hifadhi za taifa. Mfano katika  mfumo wa kiikolojia wa Serengeti-Maasai Mara Kenya unajumuisha wanyama mbalimbali wakiwemo wanyama wahamiaji - Nyumbu zaidi ya milioni mbili ambao kila mwaka wanahama kutoka sehemu wanapozaa na kuenda sehemu wasipozaa kwa ajili ya mabadiliko ya hali ya hewa, kutafuta chakula, mazingira na maji.

Fisi Madoa na jamii nyingine za Fisi huitwa bwana afya katika hifadhi kwa sababu ya kula idadi kubwa ya mizoga ingawa kuna wanyama wengine kama Simba, Chui, Mbweha na ndege aina ya Tumbusi ambao nao hula mizoga hiyo.

Hivyo bila Fsi kula mizoga hiyo kwa idadi kubwa, hifadhi zingekuwa zinanuka na kukatisha wageni kuzitembelea jambo ambalo lingechangia kupoteza mapato yatokanayo na utalii.

ERNEST SITTA NI MTAALAMU WA ELIMU YA WANYAMA NA MIMEA AMBAYE AMEFANYA KAZI NA TAFITI MBALIMBALI KATIKA HIFADHI TOFAUTI TOFAUTI HAPA NCHINI KWA ZAIDI YA MIAKA 10

DSTV YAJA NA OFA KABAMBE YA MSIMU WA SIKUKUU

 



NA MWANDISHI MAALUM

KATIKA kunogesha zaidi msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka na mwaka mpya, Kampuni ya MultiChoice Tanzania imetangaza ofa kabambe kwa wateja wapya wa DStv yenye lengo la kuhakikisha Watanzania wengi wanapata huduma hiyo ili waweze kufurahia burudani, elimu na habari wao na familia zao msimu huu wa sikukuu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya DStv ya msimu wa sikukuu iliyopewa jina la ‘Vibe la sikukuu na DStv kama DStv’, Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania, Ronald Shelukindo amesema kama ilivyo ada kwa DStv, kila unapofika msimu wa sikukuu hutoa ofa maalum kwa wateja wake ili kuwapa uhakika wa kupata huduma za DStv kipindi cha sikukuu na watu wengi wakiwemo watoto huwa likizo hivyo kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa burudani nyumbani.

Akifafanua, Shelukindo amesema kampeni ya msimu wa sikukuu DStv hutoa ofa maalum kwa wateja wake.

“Kwa wale ambao bado hawajajiunga na DStv, huu ndio wakati muafaka kwani kuna ofa maalum ya kujiunga ambapo mteja ataunganishwa na DStv kwa Sh,79,000 tu na zawadi ya kifurushi cha Family mwezi mmoja bila malipo” alisema Shelukindo.

Alisema ofa hii inawapa uhakika wateja wapya kufurahia maudhui motomoto ndani ya DStv na itadumu hadi mwisho wa mwezi Desemba 2020.


Mkuu wa Mauzo wa MultiChoice Tanzania, Salum Salum akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya msimu wa sikukuu ambapo DStv imetangaza ofa kabambe kwa wateja wake


Akifafanua zaidi kuhusu ofa hiyo alisema inapatikana nchi nzima kwa mawakala wa DStv hivyo mteja atapata ofa hii na huduma ya kufungiwa DStv popote alipo kwa urahisi na haraka.

“Tunafahamu kuwa kipindi hiki cha sikukuu watu wengi husafiri kuungana na familia zao maeneo mbalimbali mijini na vijijini na kwa kulitambua hili tumejipanga kuhakikisha huduma zetu zinapatikana kirahisi kila mahali”

Amewashauri wateja wote ambao wanahitaji huduma za DStv, mbali na kwenda kwenye vituo au mawakala wa DStv, wanaweza pia kupata huduma hiyo kwa kupiga simu 0659070707 au kwa kutembelea kurasa za DStv Tanzania za mitandao ya kijamii Instagram @dstvtanzania, Twitter @DStv_Tz na Facebook @DStv(tz) ambapo wanaweza kupata huduma mbalimbali za DStv kama vile kuunganishwa, kulipia vifurushi, kubadili kifurushi na huduma nyinginezo.

Kwa wateja wa DStv, Salum amesema wataendelea kupata maudhui kemkem kuanzia michezo, burudani, vipindi vya elimu, chaneli za watoto, sinema na tamthilia za ndani na nje bila kusahau chaneli za habari zitakazowahakikishia taarifa mbalimbali kutoka pande zote za dunia.

Kwa wale wanaosafiri, amewakumbusha kupakua App ya DStv Now inayowawezesha kuendelea kufurahia huduma za DStv kwenye vifaa mbalimbali kama simu janja bila gharama yaziada.

“Kwa wale wanaosafiri na wangehitaji kuendelea kuburudika na DStv, ni vyema wakatumua huduma yetu ya DStv Now kwa kupakua app yetu na hivyo kuweza kutumia akaunti zao katika vifaa zaidi ya vine popote walipo nchini bila kulazimika kulipia malipo yoyote ya ziada” alisisitiza Salum



Waigizaji maarufu katika tamthilia ya Karma Ford (kulia) na Misa (Katikati) wakiwa pamoja na maafisa wa DStv Tanzania – Mkuu wa Masoko Ronald Shelukindo (wa pili kulia), Mkuu wa Mauzo Salum Salum (wa pili kushoto) na Afisa Uhusiano wa kampuni hiyo Grace Mgaya (kushoto) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya msimu wa sikukuu

 Hafla ya kuzindua kampeni hiyo ya DStv ilihudhuriwa na baadhi ya wasanii maarufu wa Bongo Movie wanaoigiza katika tamthilia na filamu mbalimbali zinazoonyeshwa kwenye chaneli ya Maisha Magic Bongo ndani ya DStv akiwemo kinara wa tamthilia maarufu ya Karma Wema Sepetu.

 

 

Wednesday, November 18, 2020

WAFANYAKAZI MR CLEAN WAMLILIA JPM

 


NA MWANDISHI WETU

WAFANYAKAZI wa Kampuni ya udobi ya Mr Clean ya jijini Dar es Salaam wamemuomba Rais John Magufuli atakapoteua Baraza la Mawaziri, amuelekeze Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira kutafuta suluhu ya kudumu kwa watanzania wanaofanyishwa kazi muda mrefu bila kupewa mikataba ya kazi.

Wakizungumza na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni kuhusu kutopatiwa mikataba ya kazi na mwajiri wao kwa muda mrefu, walisema wao ni sehemu tu ya watanzania wengi wanaonyanyasika sehemu za kazi na wameamua kupaza sauti zao ili Rais ambaye amekuwa akiwatetea wanyonge awasikie.

"Tunaamini Rais akisikia kilio chetu atatusidia kutatua hii kero yetu. Sisi tumefanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa katika Kampuni ya Udobi ya Mr Clean lakini mwajiri wetu hajatupa mikataba ya kazi. Kila tukiomba anatishia kutufukuza kazi.

"Tunapenda kufanya kazi kwa sababu bila kazi kwa maisha ya sasa mtu unakufa njaa na tunafurahi wanapojitokeza wawekezaji na wafanyabiashara wenye makampuni wanaotoa nafasi za kazi lakini mazingira ya kazi ni magumu mno.

"Mtu unakuwa kibarua mwaka mzima, miaka miwili, kazi yenyewe ngumu maana tunafua nguo kwa madawa ambayo hatujui yana kemikali za aina gani. Matokeo yake ukiugua unaondolewa kazini.

"Hatuna pensheni ya aina yoyote, hatuna Bima ya Afya, tunafua nguo kwa kutumia madawa, tunalipwa mkononi kama vibarua serikali haipati kodi yoyote ambayo ingetokana na mishahara yetu. Tunaomba kilio chetu kimfikie rais atuletee waziri wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yetu wafanyakazi wa sekta binafsi," alisema mmoja wa wafanyakazi hao.

Alipoulizwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mr Clean, Ravi Shankar kuhusu malalamiko ya wafanyakazi hao alisema suala hilo aulizwe msemaji wa Kampuni yake aliyemtaja kwa jina la Morris Ngonyani.

 

Alipoulizwa Ngonyani alisema yeye siyo msemaji wa kampuni ya Mr Clean bali mwenye Kampuni akiwa na hisa asilimia 90 na huyo alielekeza aulizwe ni mfanyakazi wake ambaye hana ruhusa ya kuzungumza lolote kwa sababu amemuweka kiwandani hapo kama msimamizi wa wafanyakazi tu.

Akijibu malalamiko ya wafanyakazi hao alisema walikuwa vibarua ambao kwa sasa wameishaondolewa kazini na kwamba Kampuni ya Mr Clean imebaki na wafanyakazi saba tu nchi nzima kutokana na mwenendo mgumu wa biashara.

CCM ILALA YATOA MSIMAMO MADAI YA DIWANI WAKE KUDANGANYA URAIA




NA MWANDISHI WETU

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala kimesema hakina shaka na maelezo yaliyotolewa na Diwani wake wa Kata Kivukoni, Sharik Choughule kuhusu uraia wake.

Kimesema kabla ya wagombea wa chama hicho kupitishwa kupeperusha bendera  ya chama katika uchaguzi, kilijiridhisha kuwa wote wana sifa stahiki.

CCM kimesema watu wanaoibuka sasa kudai uraia wa Choughule una utata wanapaswa kupuuzwa kwa sababu CCM huteua wagombea wake kwa umakini na baada ya kujiridhisha hivyo wenye shaka na uteuzi huo wafuate taratibu za kimahakama kuthibitisha madai yao.

Hayo yameelezwa jana na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Ilala Iddi Mkowa katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA kuhusu madai ya utata wa uraia wa Choughule na kwamba alitoa taarifa zisizokuwa sahihi kwa chama zilizomuwezesha kuteuliwa.

Mkowa alisema CCM hakina muda wa kuanza kuchunguza tuhuma za udanganyifu au utata wa uraia wa kada wake huyo kwa sababu kina uhakika na taarifa alizotoa hivyo wenye wasiwasi wana wajibu wa kuthibitisha madai yao kisheria ndipo chama kiweze kuchukua hatua.

Kauli hii ya Mkowa inafuatia taarifa iliyoripotiwa juzi na Tanzania PANORAMA kuwa Choughule anadaiwa kutoa taarifa zisizokuwa sahihi kuhusu uraia wake ili kufanikisha azma yake ya kuwa kiongozi katika chama hicho.

Madai hayo yalianza kusambaa mapema mwezi uliopita lakini jitahada za Tanzania PANORAMA kumfikia kuyazungumzia hazikuweza kufanikiwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kutingwa na shughuli nyingi za kisiasa.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa kata hiyo aliyefikiwa na Tanzania PANORAMA na kukubali kuzungumza kwa sharti la jina lake kuhifadhiwa kwa vile hataki aonekane ana nia mbaya dhidi ya mbio za kusaka uongozi wa kisiasa za Choughule, alisema awali kulikuwa na utata huo lakini ulitatuliwa.

Taarifa zilizokusanywa Tanzania PANORAMA zimeonyesha kuwa Choughule aliingia nchini kwa kutumia hati ya kusafiria ya India akiwa ameambata na ndugu yake wa kiume, ambao walikuja kumtembelea mjomba wao anayefanya biashara jijini Dar es Salaam.

Uchunguzi umeonyesha kuwa Choughule na ndugu yake walikuja nchini kuonana na mjomba wao aliyekuwa ametwaa mali za baba yao baada ya kufariki dunia.

Washirika wa karibu wa Choughule wamekaririwa kuwa vijana hao wawili walishindwa kuafikiana na mjomba wao ndipo walipogoma kuondoka nchini kurejea India walikokuwa wakiishi na mama yao.

Kwamba ili kuzika mzozo baina yao, mjomba wao aliwaingiza katika moja ya kampuni zake kufanya kazi huku akiwataka wawe na subira ya kutatua utata wa umiliki wa mali hizo.

 Imeelezwa kuwa mjomba (jina limehifadhiwa kwa sababu hajapatikana kuzungumza) alitoa taarifa ofisi za uhamiaji kuhusu uwepo wa vijana hao waliokuwa wakiishi nchini na kufanya kazi kinyume cha sheria na walikamatwa na taratibu za kuwarudisha India zilianza kufanyika.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa vijana hao walilia na kupiga magoti mbele ya mjomba wao wakimuomba azungumze na maofisa wa Uhamiaji ili wasirejeshwe India kwa sababu walikuwa wakiishi maisha ya shida na mama yao baada ya baba yao kufariki na kwamba mjomba wao alikuwa hawatumii fedha kama alivyokuwa akifanya baba yao licha ya kujimilikisha mali zote.

Inadaiwa mjomba wao aliwapa sharti la kutomuuliza tena kuhusu mali alizotwaa kwa marehemu kama wanataka kiendelea kuwepo Tanzania, amri ambayo waliiafiki na yalifanyika mazungumzo wakaachiwa.

 Afisa mmoja wa CCM wa Kata ya Kivukoni ambaye jina lake limehifadhiwa ameeleza kuwa ni kweli vijana hao waliingia nchini wakitokea India na kufikia kwa mjomba wao kabla ya kukamatwa na maofisa uhamiaji ambao waliwapakia kwenye ndege na kuwarudisha India ambako walikataliwa kuingia na kurudishwa hapa nchini.

"Ni kweli Choughule alikuja nchini akiwa na mwenzake. Walikuja kwa mjomba wao lakini baadaye kulitoka mtafaruku wakakamatwa na uhamiaji wakapandishwa ndege wakarejeshwa India ambako hawakupokelewa walirudishiwa uwanja wa ndege, wakarejea Tanzania.

"Hakukuwa na namna ikabidi wapokelewe hapa nchini wakarudi tena kuishi na mjomba wao ndipo zikaanza kufanyika taratibu za uraia na uhamiaji iliwasafisha kwa kuwapa uraia wakawa huru kujihusisha na shughuli za kisiasa na mpaka sasa Choughule anaendelea na siasa," alisema.

Choughule amekuwa akikwepa kulizungumzia suala hilo kwa zaidi ya wiki tatu sasa kwani licha ya Tanzania PANORAMA kufika ofisi za CCM Kata ya Kivukoni ambako hakupatikani na kisha kutafutwa kwa simu yake ya kiganjani na kuomba apewe muda kabla ya kuzungumza, hajatekeleza ahadi yake hiyo wala kujibu maswali aliyotumiwa.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphery Polepole ambaye alitafutwa kwa simu yake ya kiganjani kuzungumzia suala hilo, simu yake imekuwa ikiita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi kwenye simu yake hakuujibu.

Kwa mujibu wa taratibu za Idara ya Uhamiaji, raia wa kigeni anaweza kupewa uraia kabla ya kuwa na sifa za kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa isipokuwa urais wa Tanzania akiishi nchini kuanzia miaka nane na kufuata taratibu za kuomba uraia ikiwemo muda wote wa kuishi nchini kuwa na kibali.

Tanzania PANORAMA limeperuzi sifa zinazotakiwa kwa wanachama wa CCM kugombea uongozi wa kisiasa ambapo ya kwanza inasomeka awe raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

 


WAZIRI MKUU AZINDUA UCHEPUSHAJI MAJI MTO RUFIJI

 


Misri yaahidi kufundisha Watanzania 25 kwa miaka mitatu mfululizo

NA MWANDISHI MAALUMU

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezindua kazi ya uchepushaji maji ya Mto Rufiji kwenda kwenye handaki ili kupisha ujenzi wa tuta kuu la bwawa la kufua umeme wa megawati 2115.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, alisema mradi huo utawezesha nchi kuwa na umeme mwingi na wa kutosha lakini pia utawezesha kufanya biashara ya umeme na nchi za jirani.

Uzinduzi huo ambao ulifanyika jana Novemba 18, 2020 kwenye eneo la mradi, mkoani Pwani, ulimpa fursa Waziri Mkuu kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa uzalishaji umeme kwa kutumia maporomoko ya Mto Rufiji.

"Upatikanaji wa *umeme wa bei nafuu na uhakika nchini kwetu utachochea ukuaji na mapinduzi katika sekta ya viwanda nchini kwa kushusha gharama za uendeshaji viwandani, kukabiliana na mfumuko wa bei, kuwezesha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya Afrika Mashariki, Afrika na duniani,” alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema hatua hiyo itaenda sambamba na kuvutia uwekezaji mkubwa, wa kati na mdogo katika sekta mbalimbali nchini kutokana kupungua kwa gharama za umeme za uzalishaji pamoja na kuwawezesha Watanzania wote kumudu gharama za umeme mijini hadi vijijini.



Alisema mradi huo ambao unafadhiliwa na serikali kwa asilimia 100 kwa gharama ya sh. trilioni 6.557, unasimamiwa na Mhandisi Mshauri wa Kitanzania kwa asilimia 100.

“Serikali imeendelea kuwaamini na kuwatumia wataalamu wa Kitanzania katika kusimamia miradi mikubwa, na kwa kutambua hilo mradi huu unasimamiwa na Mhandisi Mshauri wa Kitanzania kwa asilimia 100,” alisema.

Alisema mradi huo wa kufua umeme kwa kutumia maji wa Julius Nyerere ni mkubwa, wa kimkakati na wa aina yake katika ukanda wa Afrika, ukiwa ni wa kwanza kwa ukubwa kwa Afrika Mashariki na wa nne barani Afrika na akasisitiza kuwe na usimamizi makini na wa viwango ili kuhakikisha unakamilika katika muda uliopangwa.

“Nimeambiwa kwamba, mradi huu unaenda sambamba na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka eneo la mradi hadi Chalinze, yote hii ni kuhakikisha umeme unaotoka hapa unaingizwa kwenye gridi ya Taifa.”

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said alisema hadi kufikia Oktoba 31, mwaka huu, mradi huo ulikuwa umeshatoa ajira za moja kwa moja 6,364 ambapo kati ya hizo, ajira 5,728 zikiwa ni za Watanzania.

Akielezea hatua iliyofikiwa kwenye usambazaji wa umeme nchini, Katibu Mkuu huyo alisema hadi sasa vijiji 9,884 kati ya 12,264 vilivyopo nchini vimekwishapatiwa umeme.

“Tuna mpango wa kukamilisha vijiji vyote vilivyobakia ndani ya miaka miwili ijayo,” alisema.

Wakati huohuo, Waziri wa Nyumba na Huduma za Mijini wa Misri, Dkt. Assem el Gazzar alisema Rais wa nchi hiyo, Abdel Fattah al-Sisi anafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ambao unajengwa kwa ubia na kampuni za Arab Contractors and El Sewedy Electric kutoka Misri.

“Rais wetu anafuatilia kwa karibu maendeleo ya mradi huu na tunatarajia utaisha ndani ya muda uliopangwa. Kukamilika kwa mardi huu kutahakikisha nishati ya umeme inakuwa ya uhakika katika kuleta maendeleo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Misri, Dkt. Mohamed Shaker El-Markabi alisema Serikali ya nchi hiyo iko tayari kubadilishana uzoefu na Wizara ya Nishati ya Tanzania na kwamba itatoa mafunzo kwa Watanzania 25 kwa miaka mitatu ijayo.

“Tunawapongeza Watanzania kwa hatua hii ya kihistoria. Wizara yetu iko tayari kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo na Wizara ya Nishati ya Tanzania, na katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, tutatoa mafunzo (full training) kwa Watanzania 25,” alisema.

Alisema upatikanaji wa umeme wa uhakika ni suala la muhimu kwa wananchi kama ilivyo kwa maji na huduma nyingine muhimu.

“Uzalishaji wa megawati 2,115 utaiwezesha Tanzania kuwa na umeme wa uhakika, itaongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme na kutengeneza fursa za ajira na za kibiashara.

 “Ndani ya miaka mitatu ijayo, Tanzania itakuwa kinara wa uzalishaji nishati ya umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakapokamilika, unatarajiwa kutoa ziada ya kuuza kwenye nchi za jirani,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka alisema ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 75.76 na kwamba uchepushaji wa maji ya mto uliofanyika sasa ni wa muda tu ili kupisha ujenzi wa tuta kuu.

“Tumekwepesha umbali wa mita 700 tu, na tukimaliza ujenzi wa tuta, tutarudisha maji ya mto kwenye njia yake ya awali,” alisema.