NA MWANDISHI WETU
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewaasa Watanzania kuchagua
kiongozi ambaye atakuza uhusiano wa kidiplomasia na nchi jirani.
“Tanzania inazungukwa na nchi tisa ambazo baadhi
yake ziko kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na nyingine hazimo. Tunahitaji
kiongozi ambaye ataweza kuhakikisha nchi hii inakuwa na uhusiano mwema na nchi
jirani na nchi nyingine duniani kote lakini pia anayeweza kuilinda heshima ya
nchi yetu,” amesema.
Majaliwa ameyasema hayo Alhamisi, Oktoba Mosi, 2020
wakati akizungumza na wakazi wa Kata za Nyakahura na Nyakanazi, wilayani
Biharamulo, mkoani Kagera akiwa njiani kuelekea Wilaya za Bukombe na Mbogwe
mkoani Geita.
Majaliwa ambaye amemaliza ziara yake mkoani Kagera
ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli
alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi,
Injinia Ezra Chiwelesa na wagombea udiwani wa CCM wa kata hizo, Apolinary
Mgalula na Amos Madegwa.
Akielezea suala la vitambulisho vya uraia, amesema
kote alikopita mkoani humo wananchi wanauliza kuhusu kuchelewa kutolewa kwa
vitambulisho hivyo.
"Ucheleweshaji huu hauko hapa mkoani Kagera tu
bali hata kwenye mikoa ya pembezoni ya Kigoma, Songwe, Katavi, Ruvuma, Mtwara,
Lindi, Pwani, Arusha na Mara.
"Hii ni kwa sababu tunataka tujiridhishe na uraia
wa waombaji kwani hili suala ni kwa usalama wa nchi yetu. Wale walioko jirani
umbali wa km. 10 wanaruhusiwa kuja kutembea au kufanya biashara na kurudi kwao.
Hawaruhusiwi kupata vitambulisho, hivi ni kwa Watanzania tu," amesema
Majaliwa.
Kiongozi huyo amewahakikishia wakazi hao kwamba kila
Mtanzania mwenye sifa atapata kitambulisho cha Taifa kwa kuwa ndiyo mkakati wa
Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Magufuli.
Majaliwa amesema Idara ya Uhamiaji inatakiwa kuwa
makini kusimamia mchakato huo kwa sababu wapo baadhi ya raia wa nchi jirani
wanatamani kupata kitambulisho cha Taifa kutokana na amani iliyopo nchini.
"Uhamiaji iwe makini haitapendeza kuona
Mtanzania anakosa kitambulisho cha Taifa halafu mgeni kutoka nchi jirani
anapata," amesema.
Hata hivyo, amewataka wakazi hao wasikubali
kutoa rushwa kwa sababu hiyo ni haki yao na kwamba endapo itatokea wameombwa
rushwa watoe taarifa.
"Mtu wa uhamiaji akidai rushwa ili akupatie
kitambulisho toa taarifa mara moja ili tumshughulikie," amesisitiza.

