NA MWANDISHI WETU
VIBARUA wa Kampuni ya One World Company Limited ya
jijijni Dar es Salaam wamelalamika kuwa wananyanyaswa na kutishiwa maisha na
mwajiri wao.
Wamesema mwajiri wao anakiuka makubaliano
waliyoingia kufanya kazi, kutowapa mikataba ya ajira, kuwapunja malipo ya kazi
wanazofanya kwa kampuni anazowapeleka kufanya kazi anazoingia nazo mikataba ya
kumkodishia vibarua na kutopeleka fedha za makato katika mifuko ya pensheni.
Malalamiko hayo wameyatoa mwishoni mwa wiki
jijini Dar es Salaam katika mahojiano yao na TANZANIA PANORAMA.
"Tumeamua kuwatafuta nyie watu wa TANZANIA
PANORAMA baada ya kuona nyie mko tofauti na wengine kwa sababu mnagusa matatizo
ya Watanzania na kuyaweka hadhani. Ukiangalia kwenye mitandao unaona mnaandika
habari ambazo haziandikwi na wengine ambazo zinagusa maisha ya watu wanyonge
moja kwa moja.
" Sasa sisi tuna malalamiko yetu, tunaomba
yafike serikalini na tunaomba serikali ije itusikilize sisi wananchi wake.
Tunaomba kwanza kuiambia serikali kuwa huyu mwajiri wetu Kampuni ya One World
Company Limited anatunyanyasa na kututishia maisha kila tunapojaribu kudai hata
kile kidogo anachotudhulumu.
"Huyu mwajiri wetu anatufanyisha kazi kwa saa
nyingi kuliko tulivyokubaliana, baadhi yetu wana miaka mingi sana kwenye
kampuni lakini kila wakiomba ajira anasema anayetaka ajira aache kazi. Sasa
tunashagaa huyu bwana mbona anakiuka sheria kwa sababu sheria inaelekeza mtu
akifanya kazi kwa kipindi fulani anapaswa kuajiriwa.
"Jambo jingine ni pensheni, hapeleki pesa yetu
kwenye mifuko ya jamii, na huko mahakama ya kazi wamemshindwa maana amekataa
kupokea barua za mahakama baada ya wenzetu kumfungulia shauri kwenye
mahakama hiyo lakini kinachotuuma zaidi, huyu ana mikataba ya siri na baadhi ya
makampuni hapa nchini ambayo huwa anayatafutia vibarua anawapeleka kufanya kazi
huko na hayo makampuni yanamlipa ili alipe vibarua aliowapeleka.
" Kibaya hapo ni kwamba zile pesa zetu huwa
anatulipa kidogo sana kiasi kikubwa anachukua yeye bila kujali kampuni hizo
zinakuwa zimeishamlipa hela yake ya udalali. Tukimlalamikia kuwa anatuonea
anasema ambaye amechoka kuishi aendelee kuhoji na ole wake atakayebainika kutoa
siri za kampuni nje," alisema mmoja wa vibarua hao ambaye jina lake
tunalihifadhi kwa sababu ya kulinda kibarua chake.
Akizungumzia malalamiko hayo. Mwanasheria wa vibarua
hao, Saulo Kusakala alieleza kushangazwa na uongozi wa kampuni hiyo kwa
kuonyesha kiburi hata kwa Mahakama.
"Kweli mimi ni mwanasheria wao, nimeamua
kuwasaidia kwa sababu ukisikia mateso yao kwa kweli unawahurumia. Kama
mwanasheria wao nilimuandikia barua huyo mwajiri ili nipate maelezo yake kuhusu
malalamiko ya wafanyakazi wake alichojibu ni kwamba hawatambui. Yaani hana
ushirikiano kabisa," alisema.
Alipoulizwa Mkurugenzi wa One World, Kelvin Tegwa
kuhusu malalamiko hayo alisema hao waliokuja kwa waandishi wa habari
wanajisumbua na alijigamba kuwa ana mkono mrefu hivyo atawabaini na
atawashughulikia.
"Unasema wewe ni mwandishi wa habari, kwa hiyo
wamekuja kwako ili utuchafue. Kwahiyo kwako ndiyo wanadhani watapata msaada?
Labda nikuulize sasa wamekuja kalalamika kwako wewe utafanya nini? Wewe njoo
tuongee ofisini hao waache niko nao mahakamani.
" Na ninakwambia tu mimi nafanya kazi na
serikali, nina mkono mrefu hivyo hata hao waliokuja kwako nakuhakikishia ntajua
na nitawashughulikia. Hii siyo kampuni ya kuchezea, alisema.
Muda mfupi baadaye TANZANIA PANORAMA lilipigiwa simu
na mtu ambaye hakujitambulisha jina lakini uchunguzi wa namba aliyotumia
umebaini kuwa imesajiliwa kwa jina la Dismas Damas ambaye alionya kuwa kitu
chochote kinachohusu kampuni hiyo kisiandikwe.
Damas alisema iwapo maelekezo hayo yatakiukwa
asiwepo wa kulalamika na kabla hajakata simu alisema yeye ni meneja wa Kampuni
ya One World Company Ltd na milango yake ipo wazi kwa mazungumzo.