banner

Friday, September 25, 2020

"VITAMBULISHO VYA WAMACHINGA VIMETUTUA MZIGO"



NA PIUS NTIGA, MOSHI

WAFANYABIASHARA wadogo, maarufu kwa jina la Machinga katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamesema vitambulisho wa wajasiriamali wadogo vimewatua mzigo hivyo wanawashangaa baadhi ya wanasiasa wanaopotosha kuhusu vitambulisho hivyo.

Wakizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM inayoangazia mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, wafanyabiashara hao wamesema utamu wa vitambulisho hivyo wanaujua wao.

Wamesema awali walikuwa wanalipa shilingi 500 kwa siku, sawa na shilingi 182,000 kwa mwaka, kiasi ambacho ni kikubwa ukilinganisha na shilingi 20,000 wanayolipa sasa kwa mwaka.



"Tulikua tukilipa shilingi 200 ya usafi kwa siku, sawa na shilingi 73,000 kwa mwaka, ambapo sasa mateso kama hayo hatuyapati. Tena tunashukuru sana Rais Magufuli kwa kutuona na tutampa zawadi mwaka huu" wamesema Machinga.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao wadogo, mkombozi wao ni Rais Magufuli ambaye amekuja na mpango wa sh  20,000 tu kwa mwaka na sasa kero za mgambo kuwafukuza hazipo tena.

"Nikwambie tu kuwa mabenki nayo yamesema kwa kuwa tuna vitambulisho, shughuli zetu zimerasimishwa hivyo tumeanza kupewa mikopo huku vitambulisho vikiwa ni dhamana yetu". wamesema

Wamesema hivi sasa hawasumbuliwi tena na askari wa jiji wala mgambo kama ilivyokuwa hapo awali.

"Vitambulisho vya wamachinga vimetusaidia sana, tunanunua kwa ridhaa yetu, hatulazimishwi". wamesema Machinga.

Aidha, wamefafanua kuwa uwepo wa vitambulisho hivyo umewaondolea kero na kwa sasa biashara yao imeimarika zaidi na kipato chao kimeongezeka na wamefanikiwa kununua ardhi na kujenga nyumba.

Kutokana na mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi, amesema tangu kuanza kwa utaratibu huo zaidi ya asilimia 70 ya wamachinga wamepatiwa vitambulisho katika Manispaa ya Moshi.

Mwandezi amesema fedha inayotokana na vitambulisho hivyo inakwenda Hazina na kisha kurudishwa katika Manispaa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo inawagusa moja kwa moja wananchi.



"Pia tumewasaidia hawa wajasiriamali kuwajengea uwezo wa kimtaji ambapo sasa wanakopesheka kupitia vitambulisho, hivyo vimewanufaisha kwa kukopa fedha benki," amesema Mkurugenzi huyo

Hivi karibuni baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakipotosha kuhusu vitambulisho hivyo vya wamachinga kuwa haviwanufaishi na badala yake wanaibiwa, kauli ambayo Rais John Magufuli ambaye ni mgombea wa urais kupitia CCM, amewataka wafanyabiashara hao kuwapuuza wanasiasa na badala yake waunge juhudi za serikali za kuwakomboa Wamachinga. 

MAJALIWA AAHIDI MAPITIO MAPYA TOZO SEKTA YA UVUVI


 

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa aseme serikali itaendelea kufanya upya mapitio ya tozo mbalimbali katika sekta ya uvuvi ili kuwapunguzia kero Watanzania wanaojishughulisha na uvuvi.

Majaliwa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mji wa Nansio Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza kumnadi mgombea urais wa CCM, Rais John Magufuli.

Amesema katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM, serikali iliondoa kodi katika zana na malighafi za uvuvi zikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio.

"Pia tumepunguza ada ya leseni ya kuuza samaki na mazao ya uvuvi yanayovuliwa kwenye maji baridi. Serikali itaendelea kufanya upya mapitio ya tozo mbalimbali katika sekta ya uvuvi ili kuwapunguzia kero wavuvi.

" Tumeweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa vifaa bora vya uvuvi, kuzuia uingizaji na uzalishaji wa zana haramu za uvuvi na kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa zana na vyakula vya samaki," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.


TRA YAUZA SHEHENA YA SABUNI ISIYOFAA

 



NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA)  imeuza kwa njia ya mnada shehena ya sabuni ya unga ambayo muda wake wa matumizi umeisha.

Shehena hiyo ya sabuni isiyofaa kutumika baada ya muda wake kuisha iliingizwa nchini kutoka nje na kukaa bandarini bila kulipiwa ushuru kwa muda mrefu kabla TRA haijaamua kuiuza.

Habari za uhakika zilizokusanywa na TANZANIA PANORAMA zimeonyesha kuwa shehena hiyo ilikuwa na mifuko 1,800' ya sabuni ya unga aina AKO na imeuzwa kwa njia ya mnada na maafisa wa TRA huku wakijua kuwa wanatenda kosa linaloweza kuwa na athari mbaya kwa watakaoitumia sabuni hiyo.

TANZANIA PANORAMA limedokezwa na vyanzo vyake vya habari kuwa shehena hiyo ambayo thamani yake ni sh milioni 300, ili kuwa imehifadhiwa katika bandari kavu (ICD) ya Kampuni ya Azam na imepigwa mnada mapema mwezi huu kwa sh milioni 20

"Watanzania tunaumizana wenyewe kwa wenyewe. Sabuni iliyopigwa mnada na TRA imekwisha muda wake wa matumizi na TRA walilijua hilo. Sasa wameiingiza mtaani bila kujali kama itasababisha magonjwa kwa watakaoitumia,  wewe waulize uone kama watajibu, watababaisha tu maana wanajua siku hizi hakuna watu wa kichumbua mambo," alisema mmoja wa watoa habari wa TANZANIA PANORAMA.

Alipoulizwa juzi, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo  haraka haraka alikanusha kuwa taarifa hizo hazina ukweli na kutaka atumiwe ushahidi wa uwepo wa shehena hiyo na alipotumiwa sehemu ndogo ya ushahidi aliotaka aliomba apewe muda kidogo afuatilie.

Hadi juzi jioni Kayombo alishindwa kutoa majibu kwani kila alipopigiwa alisema maafisa wanaohusika na minada na wale wa forodha wote wametoka ofisini hivyo anaendelea kuwasubiri na alipoombwa namba zao za simu alikataa kutoa.

Jana asubuhi,  TANZANIA PANORAMA lilimtafuta tena Kayombo ili kuzungumzia tuhuma hizo lakini hakupokea simu na alipotumiwa ujumbe mfupi kwenye simu yake ya kiganjani akikumbushwa ahadi yake ya kutoa kauli kuhusu tuhuma hizo na pia kutimiza wajibu wake alijibu kuwa kuna taarifa moja anaisubiri kutoka kwa wahusika wa mnada.

TANZANIA PANORAMA lilimtumia ujumbe mwingine likimshauri awe anapokea simu yake na kutoa taarifa hata kama hajafanikiwa kupata majibu husika na yeye alijibu kuwa akiwa kwenye kikao huwa hapokei simu kwa sababu siyo nidhami nzuri.

Baadaye mchana, Kayombo alitafutwa tena lakini hakujibu chochote na majira ya jioni alipiga simu na kueleza kuwa ni kweli shehena hiyo ya sabuni ilikuwepo TRA na imeishauzwa lakini haweza kusema kama muda wake wa matumizi umeishaisha au bado.



"Sasa bwana ni hivi. Ni kweli huo mzigo unaousema ni kweli ulikuwepo TRA. Ni kweli kabisa. Na mnada wake wa kwanza ulikuwa Agosti 24, 2020 lakini aliyeshinda hakuja kulipa hivyo ikabidi ufanyike mnada mwingine ndiyo ukauzika

" Ni kama kulikuwa na pande mbili zilizokuwa zikiushindania kwa sababu yule mnunuzi wa kwanza hakuja kulipa hivyo ikabidi ufanyike mnada mwingine ndipo shehena ile ikachukuliwa kwa sh. milioni 21.5 ," alisema Kayombo.

Alipoulizwa mnada wa pili uliofanyika lini na kukumbushwa kujibu swali aliloulizwa kuwa TRA inadaiwa kuuza shehena ya sabuni iliyokwisha muda wa matumizi huku ikijua kuwa inaweza kuwa na athari mbaya kwa watumiaji alisema maswali hayo hawezi kuyajibu.

"Hivi unaandikia chombo gani siku hizi........  Sasa hayo maswali mengine mimi siwezi kuyajibu we fahamu tu mnada umefanyika mara mbili," alisema Kayombo.

Thursday, September 24, 2020

SERIKALI YATUMIA BILIONI 58 KUKAMILISHA MIRADI YA MAJI UKEREWE

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imekamilisha ukarabati na upanuzi wa miradi ya maji katika Wilaya ya Nansio mkoani Mwanza kwa gharama ya sh bilioni 58.

Hayo yameelezwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa Nansio jana katika uwanja wa Getrude Mongela.

Majaliwa ambaye yuko katika ziara ya kisiasa nchi nzima ya kumnadi mgombea urais wa CCM, Rais John Pombe Magufuli, amesema kati ya fedha hizo, sh bilioni 13 zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maji ikiwemo sh bilioni 10.9 za uboreshaji wa huduma ya maji safi mjini Nansio utakaonufaisha wananchi 108,653.

Amesema sh bilioni 2.1 zimetumika kwa ajili ya kuboresha huduma ya usafi wa mazingira  mjini Nansio.

Ameitaja miradi mingine ya maji iliyokamilishwa na Serikali ya Rais Magufuli kwa gharama ya sh bilioni 1.3 kuwa ni ukarabati wa mradi wa maji wa Irugwa,  mradi wa maji ya bomba ya Nansore, mradi wa maji wa Muriti/ Ihebo, upanuzi wa mradi wa maji wa Chabilungo na upanuzi na ukarabati wa mradi wa maji Kazilankanda.

TANZANIA YASIFIWA KWA SERA BORA ZA UWEKEZAJI

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaji Rajab Kundya (mwenye suti nyeusi) akifanya mahoajino na waandishi wa Uhuru FM - Amsha Amsha 2020, Suti katika Shamba la Maua la Mwekezaji raia wa Uholanzi.

NA PIUS NTIGA, MOSHI

TANZANIA imesifiwa kuwa ina sera nzuri ya uwekezaji ambayo imekuwa kichocheo cha upatikanaji wa ajira na ukuaji wa uchumi.

Hayo yameelezwa leo na mwekezaji Fons Nijenhuis katika mahojiano na Amzha Amsha 2020 ya Uhuru FM shambani kwake Dakau, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Ameema zaidi ya ekari 250 zinatumika katika uwekezaji wa sh bilioni 6  tangu mwaka 2003 na kufanikiwa kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 1,000 katika shamba la maua la Vasso.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka  2015/2020 iliyoahidi kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kama njia moja wapo ya kuongeza ajira kwa Watanzania

Fons Nijenhuis, amesema uwekezaji huo umetoa ajira kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo na pia umesaidia kuchangamsha eneo hilo kibiashara na hivyo kuinua Uchumi.



Aidha, amesema amefanikiwa kuwajengea uwezo wananchi wanozunguka shamba hilo ambao miongoni mwao wameanzisha kilimo cha maua wanayoyauza kwake.

"Ngoja nikwambie hapa mimi nimefanikiwa kufundisha ujuzi wananchi wapo kama 40 hivi hawa wote wana mashamba hapo nje na maua yao huwa wananiuzia mimi na huwalipa kiasi cha shilingi milioni kama moja hivi kila wiki wanaponiuzia" anasema Mwekezaji.

Kwa mujibu wa mwekezaji huyo kila wiki husafirisha zaidi ya tani 250 za miche ya maua nje ya nchi na sehemu ya fedha zake hutumika pia kufanya ukarabati wa huduma katika vijiji vitatu vinavyozunguka shamba hilo.

Amesema katika shamba hilo anatumia tani 500 za udongo ambazo huziagiza kutoka nchini Uholanzi na kwamba udongo wa hapa nchini hautoshelezi.



Aidha, amesema anaendelea kufanya mazungumzo na serikali ili kuangalia uwezekano wa kuwa anatumia udongo wa hapa nchini ambao unapatikana Wilaya ya Pangani, Mkoa waTanga ili pesa anayotumia kuagiza nje udongo ibaki hapa hapa nchini.

"Sehemu kubwa ya wateja wangu wapo nchini China na Uholanzi ambako huuza hii Miche ya Maua," alisema

Kwa upande wake, Afisa Kilimo Halmashauri ya Moshi Vijijini, Mercy Urio amesema uwekezaji huo umeleta manufaa makubwa kwa jamii na Halmashauri ya Moshi vijijini na wananchi kwa ujumla wanajivunia uwepo wa mwekezaji huyo.

Nao wanufaika wa uwekezaji huo, Agnes Shofa, Justina Mushi pamoja na Benard Erasto wamesema kwa sasa maisha yao yamebadilika ukilinganisha na awali walivyokuwa kwani wamefanikiwa kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba mpya.

Naye meneja wa shamba hilo, Alany Njau, amevitaja vijiji vitatu vinavyonufaika na uwekezaji huo kuwa ni pamoja na kijiji cha Umbwe, Ucharo pamoja na Dakau na wamekuwa wakifundisha ujuzi kwa wananchi wa namna ya kupandikiza pia Vikonyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaj Rajab Kundya, aliambatana na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru Fm, katika shamba hilo amesema mafanikio yote yamepatikana kutoka na uongozi thabiti wa Rais Dk. John Magufuli na kusisitiza kuwa chanda chema huvikwa Pete.


Aidha, mkuu huyo wa Wilaya ya Moshi, amesema shamba hilo la maua ni moja ya mashamba 11 yaliyopo katika wilaya hiyo na  yameendelezwa vizuri kupitia vyama vya ushirika.

"Kuna changamoto kadhaa ambazo hujitokeza kwa mwekezaji huyo lakini tumekuwa tukikaa pamoja kuzitafutia ufumbuzi wa kina"Amesema DC wa Moshi.

Amesema wanafarijika kuona maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji na kilimo cha kutumia mvua kinapitwa na wakati na serikali inahakikisha kuwa vyanzo vya maji vinatunzwa vizuri ili kuleta chachu katika kilimo cha Umwagiliaji.

Chama Cha Mapinduzi katika Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020 /2025 imeahidi kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika kilimo cha Kisasa cha biashara hususani ujenzi wa miundombinu ya Umwagiliaji.

Kutokana na mafanikio hayo na ahadi zinazotolewa na CCM, Amsha Amsha kazi yake kubwa ni kumkumbusha  mtanzania  Oktoba 28 mwaka huu asifanye makosa akachaguze viongozi wakaowaletea maendeleo ya haraka wanaotokana na CCM.