NA MWANDISHI MAALUMU
UJENZI wa barabara za juu eneo la Ubungo jijini Dar
es Salaam, maarufu kama Ubungo Interchange unaozikutanisha barabara tatu za
Mandela, Sam Nujoma na Morogoro unatarajiwa kukamilika Disemba 30, mwaka huu.
Ujenzi huo unaotekelezwa na serikali kupitia Wakala
wa Barabara (TANROADS), sasa umefikia asilimia 81.
Akizungumza katika mahojiano maalumu meneja wa
mradi huo, Mhandisi Barakaeli Mmari amesema ujenzi huo ulioanza Mei, 2017
unaendelea vizuri na hivi sasa barabara zote mbili za juu zimefunguliwa kwa
majaribio.
“Kwa mara ya kwanza Mei 30, 2020 tuliifungua
barabara ya ghorofa ya chini ya Morogoro kwa majaribio ambapo tuliruhusu magari
kupita na Septemba 30, 2020 barabara ya ghorofa ya pili ya Nelson Mandela / Sam
Nujoma ilifunguliwa kwa majaribio.
"Ni matarajio yetu kuwa ifikapo Disemba 30,
2020 ujenzi utakuwa umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wataendelea
kufaidi barabara hiyo," amesema Mhandisi Mmari.
Amesema lengo la ujenzi wa barabara za juu ni
kuondoa msongamano katika makutano ya barabara hizo eneo la Ubungo uliokuwa
ukisababisha watu kuchelewa kufika kwenye kwenye shughuli zao kwa wakati
na kupoteza muda mwingi ambao ungetumika kuwaongeza kipato.
Akizungumza kuhusu matumizi ya barabara hiyo kwa
madereva amesema katika eneo hilo kuna barabara ngazi (ghorofa) tatu, ya chini,
ya kati na ya juu, ambapo ngazi ya chini itatumiwa na magari yanayotoka Mjini
kwenda Mwenge, Mwenge-Kimara, Kimara-Buguruni na Buguruni kwenda Mjini.
Amesema itatumiwa pia na magari yote yatakayokuwa
yanapinda kushoto kwenye maungio hayo.
Mhandisi Mmari amesema ngazi ya kati itatumiwa
na magari yanayotoka Kimara kwenda mjini na yatokayo mjini kwenda Kimara na
ngazi ya juu itatumiwa na magari yanayotoka Mwenge kwenda Buguruni
na Buguruni kwenda Mwenge.
Aidha, Mhandisi Mmari amesema barabara za juu
zimejumuisha njia maalumu kwa ajili ya mabasi ya mwendo kasi.
Kuhusu ajira, Mhandisi Mmari amesema mradi huo
umetoa ajira kwa watanzania wengi wakiwemo wananchi wa kawaida mpaka wahandisi
ambao wanashughulika na kazi za kihandisi katika kutekeleza ujenzi kwa ufanisi.
“Tumeajiri wafanyakazi kati ya 800 hadi 900 kwa
mwezi na kati ya hao Wafanyakazi wa nje ni asilimia 10 tu huku wafanyakazi
wazawa wakiwa asilimia 90, kwa hiyo ujenzi huu umeleta faida kwa watanzania
wengi hasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam," Amesema Mhandisi Mmari.
Kwa upande mwingine, Wananchi wa Ubungo
waliozungumzia mradi huo hawakuficha furaha yao kwa kufunguliwa kwa majaribio
barabara hizo.
“Tunaishukuru Serikali kwani foleni sasa hakuna,
magari yanapita vizuri na sisi tunapita vizuri tu, naamini tunakoelekea
tutafanya mambo mazuri zaidi ya haya," ameeleza Bakari Juma.
Naye Johnson Mwakalukwa amesema barabara hiyo
imesaidia wasafiri kutoka mikoani kwani sasa wakifika Mbezi wanakutana na
barabara ya njia nane na wanakuja kumalizia na Ubungo 'Interchange,' hivyo
kuokoa muda mwingi waliokuwa wakiutumia kwenye foleni.

