banner

Saturday, October 17, 2020

UJENZI UBUNGO 'INTERCHANGE' KUKAMILIKA DISEMBA 30, 2020

 

NA MWANDISHI MAALUMU

UJENZI wa barabara za juu eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam, maarufu kama Ubungo Interchange unaozikutanisha barabara tatu za Mandela, Sam Nujoma na Morogoro unatarajiwa kukamilika Disemba 30, mwaka huu.

Ujenzi huo unaotekelezwa na serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), sasa umefikia asilimia 81.

Akizungumza katika mahojiano maalumu  meneja wa mradi huo, Mhandisi Barakaeli Mmari amesema ujenzi huo ulioanza Mei, 2017 unaendelea vizuri na hivi sasa barabara zote mbili za juu zimefunguliwa kwa majaribio.

“Kwa mara ya kwanza Mei 30, 2020 tuliifungua barabara ya ghorofa ya chini ya Morogoro kwa majaribio ambapo tuliruhusu magari kupita na Septemba 30, 2020 barabara ya ghorofa ya pili ya Nelson Mandela / Sam Nujoma ilifunguliwa kwa majaribio.

"Ni matarajio yetu kuwa ifikapo Disemba 30, 2020 ujenzi utakuwa umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wataendelea kufaidi barabara hiyo," amesema Mhandisi  Mmari.

Amesema lengo la ujenzi wa barabara za juu ni kuondoa msongamano katika makutano ya barabara hizo eneo la Ubungo uliokuwa ukisababisha watu kuchelewa kufika  kwenye kwenye shughuli zao kwa wakati na kupoteza muda mwingi ambao ungetumika kuwaongeza kipato.

Akizungumza kuhusu matumizi ya barabara hiyo kwa madereva amesema katika eneo hilo kuna barabara ngazi (ghorofa) tatu, ya chini, ya kati na ya juu, ambapo ngazi ya chini itatumiwa na magari yanayotoka Mjini kwenda Mwenge, Mwenge-Kimara, Kimara-Buguruni na Buguruni kwenda Mjini.

Amesema itatumiwa pia na magari yote yatakayokuwa yanapinda kushoto kwenye maungio hayo.

Mhandisi Mmari amesema ngazi ya kati  itatumiwa na magari yanayotoka Kimara kwenda mjini na yatokayo mjini kwenda Kimara na ngazi ya juu itatumiwa na magari yanayotoka  Mwenge kwenda Buguruni na  Buguruni kwenda Mwenge.

Aidha, Mhandisi Mmari amesema barabara za juu zimejumuisha njia maalumu kwa ajili ya mabasi ya mwendo kasi. 

Kuhusu ajira, Mhandisi Mmari amesema mradi huo umetoa ajira kwa watanzania wengi wakiwemo wananchi wa kawaida mpaka wahandisi ambao wanashughulika na kazi za kihandisi katika kutekeleza ujenzi kwa ufanisi.

“Tumeajiri wafanyakazi kati ya 800 hadi 900 kwa mwezi na kati ya hao Wafanyakazi wa nje ni asilimia 10 tu huku wafanyakazi wazawa wakiwa asilimia 90, kwa hiyo ujenzi huu umeleta faida kwa watanzania wengi hasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam," Amesema Mhandisi Mmari.

Kwa upande mwingine, Wananchi wa Ubungo waliozungumzia mradi huo hawakuficha furaha yao kwa kufunguliwa kwa majaribio barabara hizo.

“Tunaishukuru Serikali kwani foleni sasa hakuna, magari yanapita vizuri na sisi tunapita vizuri tu, naamini tunakoelekea tutafanya mambo mazuri zaidi ya haya,"  ameeleza Bakari Juma.

Naye Johnson Mwakalukwa amesema barabara hiyo imesaidia wasafiri kutoka mikoani kwani sasa wakifika Mbezi wanakutana na barabara ya njia nane na wanakuja kumalizia na Ubungo 'Interchange,' hivyo kuokoa muda mwingi waliokuwa wakiutumia kwenye foleni.

Thursday, October 15, 2020

TANROAD DAR ES SALAAM WALALAMIKA SHERIA ZA BARABARA KUPUUZWA

 

NA MWANDISHI WETU

UONGOZI wa Wakala wa Barabara (Tanroad) Mkoa wa Dar es Salaam, umesema maagizo ya kisiasa yanayotolewa na wanasiasa kuhusu matumizi na utunzaji wa miundombinu ya barabara yamekuwa yakikinzana na sheria na miongozo ya utunzaji barabara.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Mipango Tanroad Mkoa wa Dar es Salaam, Elisony Mweladzi alipofanya mahojiano na TANZANIA PANORAMA wiki iliyopita kuhusu malalamiko ya wafanyabiashara wa eneo la Kimara Mwisho kupangishwa vibanda vya biashara vilivyo katika eneo la Tanroad kwa bei kubwa.

Katika majibu yake, Mweladzi alisema sheria na miongozo iliyopo hairuhusu mtu yeyote kufanya biashara pembeni ya barabara hivyo Tanroad haijakodisha eneo lolote lililo pembezoni mwa barabara isipokuwa wafanyabiashara wamekuwa wakivamia maeneo yaliyo wazi na kuyatumia  kibiashara kwa kufuata maagizo ya kisiasa yanayotolewa na wanasiasa.

"Kwanza nataka ieleweke hakuna mwekezaji eneo la Kimara mwisho bali kuna wafanyabiashara pale. Kweli lile ni eneo la Tanroad na imelitoa kwa wafanyabiashara wapatao sita, Wanne upande wa kulia na wawili wapo upande wa kushoto wa barabara.

"Hawa tumewakodisha maeneo hayo na wanalipa kwa dola (fedha za marekani) lakini kwa ajili ya maegesho ya magari na siyo kuweka vibanda vidogo vidogo vya wafanyabiashara wa bidhaa za vyakula na nyinginezo.

" Sasa sisi tunatoa vibali vya kuegesha magari tu lakini hatuhusiki hata kidogo na vibali vya wafanyabiashara wadogo ndani ya hifadhi ya barabara. Na tulishachukua hatua hapo awali na kama wapo wengine basi tutawashughulikia.

"Tatizo linalotukwamisha kusimamia ipasavyo jambo hili ni matamko ya kisiasa yanayotolewa na viongozi wa kisiasa kwa sababu hawazingatia sheria, wanawaruhusu kufanya biashara pembezoni mwa barabara jambo ambalo ni kinyume kabisa cha sheria. Nadhani hata wewe mwandishi unaujua ugumu wa kusimamia sheria panapokuwa na upinzani kutoka kwa wanasiasa," alisema  Mweladzi.

Awali wafanyabiashara wadogo wa eneo Kimara Mwisho waliiambia TANZANIA PANORAMA kuwa mwekezaji aliyepewa eneo la pembezoni mwa barabara na Tanroad anawatoza fedha nyingi za kukodi vibanda vya biashara na hata wasiokuwa na vibanda nao wanatozwa bila kujali wana vitambulisho vya wamachinga.

Walisema vibanda vya mbogamboga na mama lishe vinatozwa kuanzia sh 50,000 hadi 300,000 na wapiga kiwi viatu ambao kikawaida hawana vibanda wao wanalipia eneo wanaloweka meza sh 45,000 hadi 50,000.

Akijibu hilo, Mweladzi alisema malalamiko hayo yanashagaza kwa sababu wafanyabiashara hao walipata kufika ofisini kwake wakimsifia na kumshukuru mfanyabiashara aliyewapa eneo hilo na kuwaruhusu kufanya biashara bila kuwatoza chochote na waliomba Tanroads inamruhusu awajengee choo.

TANZANIA PANORAMA lilifika ofisini kwa mfanyabiashara huyo eneo la Kimara Mwisho na kukutana na wasaidizi wake walioeleza kuwa bosi wao hayupo hivyo wapewe muda wawasiliane naye kabla ya kujibu maswali waliyoulizwa.

Wakijibu kwa niaba ya bosi wao walisema, Biashara yote inayoendelea katika eneo hilo la pembezoni mwa barabara inatambuliwa na kusimamiwa na Meneja wa Tanroads wa Mkoa wa Dar es Salaam hivyo kuna jambo lolote linalohitaji ufafanuzi basi aulizwe yeye.

WEZI WAJA NA MBINU MPYA DAR ES SALAAM

 



NA MWANDISHI WETU

MAGENGE ya uhalifu wa kutumia silaha jijini Dar es Salaam yamebuni mbinu mpya ya kutekeleza vitendo vya kihalifu pasipo watu walio karibu na eneo la tukio kubaini chochote.

Mbinu hiyo ni kuwateka abiria wanaokuwa wamepanda kwenye daladala kisha wahalifu hao huanza kupiga kelele kwa namna ya kushangalia na muziki ndani ya daladala hiyo hufunguliwa kwa sauti ya juu sana.

Katikati ya kelele hizo za muziki na ushagiliaji ndipo wahalifu huanza kushambuliwa abiria waliowapakia kwa visu na bisibisi kabla ya kuwapora fedha na mali wanazokuwa nazo kisha kuwatupa njiani.

Moja ya matukio hayo ya kuogofya lililoshuhudiwa na TANZANIA PANORAMA, limetokea Jumamosi, Oktoba 10, 2020 eneo la kunduchi njia panda ya kwenda Hoteli ya Bahari Beach, ambako daladala lililokuwa na genge wahalifu zaidi ya 20 lilisimama na mmoja wa wahalifu hao akatangaza kuwa linakwenda Makumbusho.

Katika kituo hicho, walipanda abiria watatu akiwemo Mwandishi wa TANZANIA PANORAMA na baada ya kupanda na daladala kuondoka, dereva alifungua muziki kwa sauti ya juu na wahalifu wakaanza kushangilia kwa nguvu kwa staili ya ushangiliaji wa mashabiki wa soka.

"Baada ya kufungua muziki kwa sauti ya juu na wao kuanza kupiga kelele ndiyo wakatoa mapanga na bisibisi wakaanza kutushambulia. Abiria ya kwanza mwanamke ambaye alikuwa ameng'ang’ania pochi yake alikatwa panga mkononi, mkononi ukaning'inia akaachia pochi akaanguka chini wakabembe hadi nyuma ya gari wakaanza kumsachi.

"Mimi nikajaribu kumwambia dreva asimamishe gari kumbe ni mwenzao maana alichomoa upanga mkali akanielekezea huku akinitaka nitulie. Wezi wale wakanivamia na sikuwa mbishi wakanipora na kunichakaza kwa ngumi za kutosha bila kujali kuwa sikutoa upinzani wowote kwao," alisema mwandishi wa TANZANIA PANORAMA.

Alisema gari hilo lilikuwa linaendeshwa kwa mwendo mkali na kabla ya kufika njiapanda ya mbuyuni abiria mmoja ambaye alikuwa amekatwa mapanga mara mbili  mwilini na kuporwa kila kitu alitupwa nje na kuachwa hapo kisha gari likaondoka kwa kasi tena.

"Baada tu ya kukata kona ya mbuyuni gari likashika mwelekeo wa Mwenge lilipunguza mwendo na mimi nikasukumwa nikatupwa hapo lakini nilifanikiwa kukariri namba na rangi za hiyo daladala, kwahiyo kwenye gari wakabaki na mateka mmoja mwanamke waliyekuwa wamemkata mkono" alisema.

Alisema alichukua bodaboda hadi kituo kidogo cha Polisi Mtongoni na kutoa taarifa ya kushambuliwa na kuporwa fedha na mali na kwamba gari hilo likifukuzwa na pikipiki litakamatwa kwa sababu amekariri namba zake na kwamba kuna abiria ndani amekatwa mkono lakini polisi walisema hawana uwezo wa kulifuatilia isipokiwa afunguliwe faili na suala lake litaanza kushughulikiwa Jumatatu.

Alisema alipewa RB namba KMT/RB/2428/2020 pamoja na PF3 kwa ajili ya kwenda kutibiwa na kuelekezwa kufika Kituo cha Polisi Kawe Jumatatu ya Oktoba 12, 2020, asubuhi ambako ataonana na mpelelezi wa kesi na taratibu nyingine kuendelea.

DK. MAGUFULI KUIMARISHA MUUNGANO, DK. MWINYI KUPAMBANA NA UDHALILISHAJI




NA MWANDISHI WETU

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Zanzibar wamchague Dk. John Pombe Magufuli kuwa rais kwa sababu ndiye mgombea pekee mwenye uwezo wa kudumisha Muungano.

"Nawaletea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefanya makubwa kwenye uongozi wake uliopita. Hata kwenye wizara alizowahi kuongoza, pia amefanya makubwa. Ndiye mgombea pekee mwenye uwezo wa kutuunganisha Wazanzibari na Watanzania Bara,” alisema.

Wito huo aliutoa Jumatatu, Oktoba 12, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa Kairo, Kiwengwa, Wilaya ya Kaskazini B.

Alisema wako baadhi ya wagombea wanaotangaza kuuvunja muungano pindi wakichaguliwa na amewataka wananchi wa Zanzibar wawaepuke.

Alisisitiza kuwa kazi ya rais si ya mchezo na inataka mtu makini, kwa hiyo akawaomba wakazi hao wamchangue mtu ambaye ana uwezo wa kupambana na wala rushwa.

Majaliwa yuko Zanzibar kuwaombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli, mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Mwinyi, wagombea ubunge wa majimbo, wawakilishi na wagombea udiwani.

Akimuombea kura Dk. Mwinyi, Majaliwa alisema Chama Cha Mapinduzi kina benki ya kutosha ya makada wenye uwezo wa kuongoza. “Chama Cha Mapinduzi kina nafasi nyingi za uongozi na katika nafasi hii ya kuongoza Zanzibar, tumemleta Dk. Hussein Mwinyi.”

Alisema yapo mambo mengi mazuri yamefanywa na Dk. Ali Mohammed Shein na yaliyobakia yatakamilishwa na Dk. Mwinyi. “Masuala yote ya kipaumbele yamewekwa kwenye ilani ya uchaguzi yenye kurasa 303. Pia kitabu hiki kimesambazwa hadi kwenye shehia zenu. Kitafuteni mkisome ili muone mambo yaliyopangwa kufanyika kwa ajili ya Zanzibar.

“Maendeleo ya mifugo yamo humu, maendeleo ya uvuvi yamo humu, maendeleo ya ajira yamo, kuwezesha sekta binafsi yamo humu, kuwezesha viwanda yamo humu, kuwezesha wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa nayo pia yamo humu,” alieleza.

Mapema, akinadi sera zake, Dk. Mwinyi alisema serikali yake itaimarisha uvuvi wa bahari kuu pamoja na bandari za uvuvi pamoja na ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki ili kuongeza ajira na masoko kwa bidhaa za baharini.

Alisema ataimarisha ufugaji wa samaki ikiwa ni njia mojawapo ya kulinda mazingira. “Nitasimamia hilo la ufugaji wa samaki hasa kwenye maeneo ya mikoko kwa sababu tutakuwa pia tunalinda mazingira yetu,” alisema.

Alisisitiza kuwa atashughulikia tatizo la mmomonyoko wa maadili na hasa tatizo la matumizi ya dawa za kulevya na udhalilishaji wa wanawake na watoto. “Ninawaomba mtoe ushirikiano kwa sababu wanaofanya hivi vitendo mnawajua. Tusaidieni ili tuweze kudhibiti hivi vitendo vya udhalilishaji na dawa za kulevya,” alisema.

Akielezea kuhusu sekta ya maji, Dk. Mwinyi alisema upatikanaji wa maji safi na salama umefikia asilimia 72 na kwamba asilimia 28 iliyobakia ni ya kutoa maji kutoka barabara kuu hadi kwenye makazi ya watu. “Serikali yetu itakamilisha hiyo sehemu ndogo iliyobakia,” alisema.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuomba kura za Dk. Magufuli, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani wa CCM.

Saturday, October 3, 2020

RAIS DK. MAGUFULI AUZWA KWA REKODI YAKE YA KUTUKUKA

 

NA MWANDISHI WETU

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapunduzi (CCM), Kassim Majaliwa jana amemuuza mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Pombe Magufuli kwa rekodi yake ya kupigiwa mfano ya utendaji kazi.

Majaliwa ameutangazia umma wa Watanzania kuwa mgombea hiyo wa CCM ana rekodi ya kutukuka ya utendaji kazi katika kipindi cha miaka 20 alipokuwa Waziri katika wizara mbalimbali.

Akiwahutubia wakazi wa Ushirombo, Okotoba Mosi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Igulwa, wilayani Bukombe mkoani Geita, amesema Dt. Magufuli ana rekodi nzuri ya utendaji kazi.

"Dk. Magufuli tunamjua. Alikuwa Waziri katika nchi hii kwa miaka 20. Alikuwa Waziri wa Ujenzi akajenga barabara ambazo sote leo tunaziona. Alipoenda Wizara ya Ardhi, akapiga marufuku watumishi wa wizara hiyo kujilimbikizia viwanja vinne vinne.

"Nimekuja kuwaomba kura zenu. Ni lazima tumpe kura mtu ambaye tunaijua historia yake ya kwamba aliwahi kuwa kiongozi na ameweka historia," amesema.

Majaliwa amewataka wananchi wamchague kiongozi ambaye anaweza kuisimamia Serikali yake.

"Usipokuwa makini unaweza kumpa mtu nchi halafu akashindwa kuisimamia. Kiongozi anayefaa, mwenye uwezo wa kuratibu rasilimali zetu na kuzisimamia, si mwingine bali ni Dk. Magufuli," amesema.

Amehimiza watanzania wawachague wagombea wa CCM ili waweze kuzungumza lugha moja. "Ni muhimu tuwe na madiwani ili waunde baraza lao la madiwani, waongee lugha moja na wapeleke hoja zao kwa mbunge wao," amesema.

Majaliwa ambaye yuko kwenye ziara ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe, Dotto Biteko na mgombea udiwani wa Kata ya Igulwa, Richard Mabenga.

"Dk. Magufuli amekuwa rais kwa miaka mitano, aliyoyafanya katika kipindi kifupi tunayaona. Dk. Magufuli huyu, wala rushwa ndiye kiboko yao. Leo niko mbele yako, bila kujali chama chako cha siasa, ninakuomba umpigie kura Dk. Magufuli. Niko mbele yenu, ninawaomba kura za wagombea wa CCM," amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema Wilaya ya Mbogwe imetengewa sh. bilioni 3.9 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Makao Makuu ya Wilaya hiyo.

Akielezea kuhusu sekta ya maji, amesema serikali imetoa fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miradi ya maji ikiwemo mradi wa maji Kabanga – Nhomolwa ambao ulipatiwa sh. bilioni 1.2. “Fedha nyingine zilizotolewa ni shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji Mbogwe ambao utanufaisha maeneo ya Kasosobe, Bwelwa na Iboya.”

Amesema upanuzi wa mradi wa maji Nyakafuru umepatiwa sh. milioni 633 ambao utanufaisha maeneo ya Lulembela na Nyakafuru, Shinyanga A & B pamoja na usimikaji wa nguzo za umeme huko Nyakafuru, Shenda na Masumbwe.

Majaliwa amemaliza ziara yake mkoani Geita na anaendelea kutafuta kura katika Mkoa wa Shinyanga.