NA MWANDISHI WETU
MAGENGE ya uhalifu wa kutumia silaha jijini Dar es
Salaam yamebuni mbinu mpya ya kutekeleza vitendo vya kihalifu pasipo watu walio
karibu na eneo la tukio kubaini chochote.
Mbinu hiyo ni kuwateka abiria wanaokuwa wamepanda
kwenye daladala kisha wahalifu hao huanza kupiga kelele kwa namna ya
kushangalia na muziki ndani ya daladala hiyo hufunguliwa kwa sauti ya juu sana.
Katikati ya kelele hizo za muziki na ushagiliaji
ndipo wahalifu huanza kushambuliwa abiria waliowapakia kwa visu na bisibisi
kabla ya kuwapora fedha na mali wanazokuwa nazo kisha kuwatupa njiani.
Moja ya matukio hayo ya kuogofya lililoshuhudiwa na
TANZANIA PANORAMA, limetokea Jumamosi, Oktoba 10, 2020 eneo la kunduchi njia panda
ya kwenda Hoteli ya Bahari Beach, ambako daladala lililokuwa na genge wahalifu
zaidi ya 20 lilisimama na mmoja wa wahalifu hao akatangaza kuwa linakwenda
Makumbusho.
Katika kituo hicho, walipanda abiria watatu akiwemo
Mwandishi wa TANZANIA PANORAMA na baada ya kupanda na daladala kuondoka, dereva
alifungua muziki kwa sauti ya juu na wahalifu wakaanza kushangilia kwa nguvu
kwa staili ya ushangiliaji wa mashabiki wa soka.
"Baada ya kufungua muziki kwa sauti ya juu na
wao kuanza kupiga kelele ndiyo wakatoa mapanga na bisibisi wakaanza
kutushambulia. Abiria ya kwanza mwanamke ambaye alikuwa ameng'ang’ania pochi
yake alikatwa panga mkononi, mkononi ukaning'inia akaachia pochi akaanguka
chini wakabembe hadi nyuma ya gari wakaanza kumsachi.
"Mimi nikajaribu kumwambia dreva asimamishe
gari kumbe ni mwenzao maana alichomoa upanga mkali akanielekezea huku akinitaka
nitulie. Wezi wale wakanivamia na sikuwa mbishi wakanipora na kunichakaza kwa
ngumi za kutosha bila kujali kuwa sikutoa upinzani wowote kwao," alisema
mwandishi wa TANZANIA PANORAMA.
Alisema gari hilo lilikuwa linaendeshwa kwa mwendo
mkali na kabla ya kufika njiapanda ya mbuyuni abiria mmoja ambaye alikuwa
amekatwa mapanga mara mbili mwilini na kuporwa kila kitu alitupwa nje na kuachwa
hapo kisha gari likaondoka kwa kasi tena.
"Baada tu ya kukata kona ya mbuyuni gari likashika
mwelekeo wa Mwenge lilipunguza mwendo na mimi nikasukumwa nikatupwa hapo lakini
nilifanikiwa kukariri namba na rangi za hiyo daladala, kwahiyo kwenye gari
wakabaki na mateka mmoja mwanamke waliyekuwa wamemkata mkono" alisema.
Alisema alichukua bodaboda hadi kituo kidogo cha
Polisi Mtongoni na kutoa taarifa ya kushambuliwa na kuporwa fedha na mali na
kwamba gari hilo likifukuzwa na pikipiki litakamatwa kwa sababu amekariri namba
zake na kwamba kuna abiria ndani amekatwa mkono lakini polisi walisema hawana
uwezo wa kulifuatilia isipokiwa afunguliwe faili na suala lake litaanza
kushughulikiwa Jumatatu.
Alisema alipewa RB namba KMT/RB/2428/2020 pamoja na
PF3 kwa ajili ya kwenda kutibiwa na kuelekezwa kufika Kituo cha Polisi Kawe
Jumatatu ya Oktoba 12, 2020, asubuhi ambako ataonana na mpelelezi wa kesi na
taratibu nyingine kuendelea.