NA PIUS NTIGA, SAME
KIWANDA cha kuchakata zao la Tangawizi kilichopo
Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kitaanza kuchakata zao Novemba mwaka huu
baada ya kupata mwekezaji.
Kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2012 kikimilikiwa
na Chama cha Ushirika cha Tangawizi Mamba, Miamba lakini kiliharibika muda
mfupi baadaye na hivyo kusikitisha shughuli zake.
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa (PSSSF), Fortunatus
Magambo ambao ndiyo mwekezaji mpya wa kiwanda hicho jana amekabidhi kwa
menejimenti mashine za kuchakata Tangawizi zilizotolewa na mfuko huo mbele ya
Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule
Katika mkutano na wananchi wa Mamba, Miamba ambao
ulihudhuriwa pia na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM kijijini hapo, Magambo amesema
mashine hizo za kisasa zimenunuliwa nchini China kwa gharama ya sh bilioni
1.83 na zinafanya kazi bila kutoa sauti.
Kwa mujibu wa ubia huo, PSSSF ina hisa ya asilimia
60 huku 40 zikiwa za wananchi wa Wilaya ya Same ambao zao lao kuu la Biashara
ukiachia Mkonge ni Tangawizi.
Aidha, amesema kiasi cha sh milioni 800 zitatumika
kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya kiwanda, ofisi, hospitali,
Karakana na miundombinu pamoja na matumizi ya awali ya kiwanda hicho.
"Tunataka kuona mradi huu unakamilika na
kusaidia kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Same na utakamilika kwa wakati
"Wataalamu kutoka China wanatarajiwa kuwasili
nchini mwezi Oktoba mwaka huu kwa ajili ya kufunga mashine hizi tayari kwa
kuanza uzalishaji," alsema Magambo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule,
amewaambia wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa serikali ya awamu tano
imejipambanua kuwa ni ya Tanzania ya viwanda, hivyo uwepo wa kiwanda hicho
utachochea kukuza vipato vyao na taifa kwa ujumla.
Amesema tani 5,000 kwa mwaka zinahitajika kiwandani
hapo, hivyo akawataka wakulima kuongeza uzalishaji wa Tangawizi ambayo itakuwa
inasindikwa hapa hapa nchini kwa matumizi ya hapa nchini na nje ya nchi.
Aidha, DC Rosemary amesema soko la Tangawizi
litakuwa kubwa baada ya uzalishaji kuanza.
Pia amewataka wananchi kuwapuuza Wanasiasa wakiwemo
wa upinzani wanaojipitisha kwao wakidai kuwa mashine za kiwanda hicho
wamezileta wao wakati zimeletwa na serikali ya awamu ya tano.
"Wananchi wangu wa Same hasa hapa Mamba,
Miamba, Corona ilichelewesha ufungaji wa mashine hizo lakini sasa
zipo hapa na nyie leo mmeshuhudia, hivyo muda wowote zitaanza kufanya kazi,
endeleeni kuiunga mkono serikali yenu" alisema DC Rosemary

Wakizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM, baadhi
ya wananchi akiwemo Mzee Ndimangwa Manento, aliyetoa shamba lake kwa ajili ya
kujengwa kiwanda hicho cha Tangawizi, wameishukuru serikali kwa kusikiliza
kilio chao cha kuleta mashine za kisasa zisizo na sauti na akawaomba wananchi
wenzake mwaka huu wasifanye makosa katika uchaguzi mkuu wakampigie kura nyingi
Rais Magufuli, wabunge na madiwani wa CCM.
Wakati huo huo, zaidi ya sh milioni 400 zimetumika
kujenga majengo mapya ya kituo cha afya cha Ndungu ikiwemo maabara, chumba cha
kuhifadhi maiti, jengo la upasuaji, pamoja na wodi ya akina mama
wajawazito.
Hayo yamesema na Afisa Mipango wa Halmashauri ya
Same, Simion Mzee wakati akizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM.
Nao baadhi ya wananchi wa Ndungu akiwemo Hatibu
Mlindoko, wamepongeza serikali kwa kuwajengea kituo hicho cha afya na wakaiomba
kupandisha hadhi kituo hicho ili kiwe Hospitali.
Kaimu Mganga Mkuu kituo hicho, Hamis Waziri Juma
amesema kabla ya majengo hayo walikuwa wanatoka rufaa nyingi kwenda Hospitali
ya Wilaya ya Same kwa ajili ya matibabu lakini sasa wajawazito wanajifungua
katika kituo hichi na hivyo kupunguza gharama ya wanachi kuwapeleka Same.
Katika hatua nyingine, zaidi ya sh milioni 60
zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa shule Kongwe ya Sekondari ya Same katika
miaka mitano ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli.
Mkuu wa Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1954 Mwalimu
Hoza Mgonja, amesema Majengo 24 yamekarabatiwa yakiwemo Mabweni, Jiko,
Madarasa, Maabara, Zahanati, Ofisi na kujenga Tenki la Maji kwa ajili ya
matumizi ya Shule hiyo ambayo sasa ni ya Kidato cha Tano na Sita.
Wakizungumzia mafanikio hayo baadhi ya Wanafunzi
wamesema Shule hiyo sasa imekuwa ya kisasa baada ya Majengo ya zamani
kubadilishwa na kujengwa mapya imesaidia pia kuongeza ufaulu na walimu
kufundisha katika mazingira mazuri na wameipongeza Serikali.

Aidha, shilingi Milioni-25 zimepelekwa na serikali
kukarabati na kujenga Ofisi na Madarasa Mawili katika Shule ya Sekondari
Mamba, iliyopo Kata ya Mamba, Miamba Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.
Kiasi hicho cha fedha
kimetajwa na Mkuu wa Shule hiyo Elizabet Irira, ambaye pia ameipongeza serikali
kwa kupeleka kiasi hicho cha fedha Shuleni hapo, hatua ambayo pia imepongezwa
na Wanafunzi wa Shule hiyo iliyopo Milimani Kilometa 90 kutoka Mjini Same hadi
Mamba, Miamba.