banner

Tuesday, December 1, 2020

TEMESA KUANZA KULIPA MADENI YA WAZABUNI

 


NA MWANDISHI WETU

WAKALA wa Ufundi na Umeme (TEMESA), itaanza kulipa sehemu ya madeni ya shilingi bilioni nne wanayodai wazabuni kutokana na fedha zilizolipwa na wizara na idara za serikali zilizotokana na agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wazabuni mbalimbali wanaidai TEMESA fedha za kusambaza vipuli na vilainishi pamoja na kutengeneza magari ya wizara na idara za serikali, madeni yanayofikia shilingi bilioni nne ya tangu 2012.

Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Dk. Stephen Massele alisema baada ya malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wazabuni,  sasa wataanza kulipa baada ya kukamilisha upitiaji wa madeni kwa kila mzabuni.

Dk. Massele alisema baadhi ya wazabuni ikiwemo kampuni ya Planet mawakili wao,  wamekwishapewa taarifa kwamba TEMESA inafanya mapitio ya madeni na itaanza kulipa  baada ya wiki moja.

Alisema fedha zitakazolipwa zimetokana na madeni wanayodai wizara na idara za serikali zilizopata huduma ya wazabuni hao na zitalipwa kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu mapema mwanzoni mwa mwaka huu.

Dk. Masele alisema madeni mengine ya wazabuni hao, yataendelea kulipwa kulingana na upatikanaji wa fedha kutoka kwa wadeni wao. TEMESA inazidai wizara na idara za serikali kiasi cha shilingi bilioni tano.

"Baadhi ya wazabuni tumewapa maelekezo kupitia mawakili wao,  wapo waliotuelewa kuwa tunakamilisha 'Reconciliation' ya fedha zilizolipwa kwa agizo la Waziri Mkuu nani ana fedha ya madeni yake na ndani ya wiki moja tutakamilisha malipo yake, " alisema Dk. Massele na kuongeza.

"Ambayo hayajalipwa hiyo watapewa taarifa na mameneja husika mengine yatasubiri kadiri tunavyolipwa. "

Kauli hiyo ya Dk. Masele imetolewa baada ya kuwepo malalamiko ya muda mrefu ya wazabuni kupitia viongozi wao wa Umoja wa Gereji Tanzania (UGETA).

Akizungumza na Tanzania PANORAMA, Mwenyekiti wa Umoja wa Gereji Tanzania (UGETA), Lumona Mkala, alisema wanachama wake wanaidai TEMESA MT Depot zaidi ya shilingi Bilioni nne za kusambaza vipuli na vilainishi vya mafuta ya magari.

Alitaja wazabuni wanaodai ni Beka investment shilingi  250,563,150, Moroturbo shilingi 80,256,197, Planet Busines link shilingi 175,312,570 na Ndeken shilingi 194,801,393

Wengine ni Kigustar Enterprisess,  Leonardo Automotive Garage, Nedea Enterprisess, RaaR Investment, Kigoma Garage, Adam Motor na Point A.

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWATUMIA SALAMU ZA ONYO WAHUJUMU USHIRIKA

 


NA MWANDISHI MAALUMU - OFISI YA WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa vyama vya ushirika wabadilike na wawe weledi ili warejesha heshima ya ushirika nchini.

Akizungumza jana katika ukumbi wa mikutano wa Hazina jijini Dodoma na wakuu wa mikoa sita, makatibu wakuu, Mrajisi wa Ushirika Taifa, warajisi wasaidizi wa mikoa,  Menejimenti ya Tume ya Ushirika,  wajumbe wa Bodi za NCU (1984) Ltd, KNCU (1984) Ltd, SHIRECU na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mkonge, Waziri Mkuu Majaliwa alisema viongozi wa vyama vya ushirika wanapaswa kubadilika kwa sababu wamepewa dhamana ya kuwasaidia Watanzania wanyonge.

"Viongozi wa ushirika ni lazima tubadilike. Nyie mliopewa dhamana kwenye vyama vikuu hivi vitatu vya KNCU, NYANZA na SHIRECU lazima mbadilike. Nyie mmepewa dhamana ya kuwasaidia Watanzania wenzetu wanyonge wanaolima ekari moja, mbili au tatu,” alisema.

Katika mkutano huo maalumu ambao Waziri Mkuu Majaliwa alipokea taarifa ya ufuatiliaji wa mwenendo wa vyama vya ushirika vya NCU (1984) Ltd, KNCU (1984) Ltd na SHIRECU (1984) Ltd kutoka kwa timu maalumu ya uchunguzi , alisema viongozi wa ushirika bado hawajabadilika kwa sababu hata kazi ya usambazaji mbolea kwa wakulima bado ni changamoto.

Uwasilishwaji wa taarifa hiyo ulishuhudiwa na Wakuu wa Mikoa ya Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Tanga, Geita na Simiyu. Pia Makatibu Wakuu wa Wizara za Fedha, Ardhi, Kilimo, Viwanda na Biashara.

Wengine walioshuhudia ni Mrajisi wa Ushirika Taifa, Warajisi Wasaidizi wa Mikoa, Menejimenti ya Tume ya Ushirika, Wajumbe wa Bodi za KNCU, NYANZA na SHIRECU na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania.

"Ninasema viongozi bado hatujabadilika kwa sababu hata suala la usambazaji wa mbegu kwa wakulima ni changamoto. Wengine wamekuja kujifunza ushirika hapa nchini na wamesonga mbele lakini sisi hatuendi mbali kwa sababu ya kukosa weledi, uaminifu na uwajibikaji katika majukumu tuliyowakabidhi.

"Nendeni mkasimamie ushirika ili heshima ya ushirika wa zamani irejee, hali ya ushirika ule ambao uliacha mali za ushirika. Bado kazi hizo mali haijakamilika. Tunataka tuzisimamie na tuwakabidhi kitu ambacho kimekamilika," alisema.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alisema anasikitika kuona makosa ya ushirika yanafanyika wakati warajisi wasaidizi wapo na hata kwenye halmashauri kuna maafisa ushirika.

“Haya madudu yanafanyika lakini warajisi wa mikoa mpo na nyie ndiyo wasimamizi wa ushirika. Je mnafanya nini?”

“Lazima uhakikishe vyama vya msingi vinasimamiwa na vinakwenda kama ambavyo sheria yetu ya ushirika inasema. Warajisi wasaidizi wapo kila mkoa na kila wilaya kuna afisa ushirika. Ni kwa nini mambo hayaendi?

"Hatutasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu anayehujumu mali za ushirika. Tulianza na tutaendelea kusimamia mali za ushirika," alisema.

Mapema, akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa, kiongozi wa timu hiyo maalumu, Asangye Bangu alisema imefanikiwa kurejesha mali 60 za ushirika zenye thamani ya sh. bilioni 68.98.

“Mali hizo zinajumuisha majengo, viwanja, magari na mitambo ya mashine, hazikuwa mikononi mwa vyama hivi vitatu lakini sasa zimerudishwa kwenye vyama," alisema Bangu.

Alisema kati ya hizo, NYANZA ilikuwa na mali 37 zenye thamani ya sh. bilioni 61.36, SHIRECU ilikuwa na mali saba zenye thamani ya sh. bilioni 3.33, KNCU ilikuwa na mali 10 zenye thamani ya sh. bilioni 2.03 na TCCCo ilikuwa na mali sita zenye thamani ya sh. bilioni 2.2.

Bangu alikabidhi taarifa hiyo ikiwa na mapendekezo kadhaa kwa serikali.

Monday, November 30, 2020

UTATA UJENZI WA SOKO JIPYA TANDALE

 

 

Ujenzi wa Soko la Tandale ulipokuwa umefikia mwezi Agosti, mwaka huu

NA MWANDISHI WETU


WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa imeelekeza nguvu kubwa kwenye ujenzi wa miundombinu, shule, hospitali na masoko, jitihada hizo zimeanza kuingia doa baada ya kusimama kwa ujenzi wa soko jipya la Tandale.

Katikati ya hilo, msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kutoa taarifa zinazohusu shughuli za maendeleo bila ukiritimba, zinazofanywa na serikali ili kutoa fursa kwa wananchi kujua miradi inayotekelezwa kwa kodi zao, nao unaonekana kuingia doa baada ya mkandarasi anajenga soko la Tandale, Namis Corporate Ltd kuweka zuio la upatikanaji wa taarifa hizo.

Haya yamebainika baada ya Tanzania PANORAMA Blog kufika eneo la ujenzi wa soko jipya la Tandale mapema wiki iliyopita kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo baada ya kudokezwa na baadhi ya wafanyakazi kuwa umesimama kutokana na ukosefu wa fedha.

Tanzania PANORAMA Blog baada ya kufika katika eneo la mradi, lilishuhudia mafundi wakiwa wamekaa kivulini huku ujenzi ukiwa umesimama na baada ya kuwahoji baadhi yao walisema wanasubiri kulipwa fedha zao waondoke kwa sababu mahali hapo hakuna kazi tena.

"Bora umekuja na sijui umeingiaje huku maana hamruhusiwi nyie kuingia humu na wakikuona watakugawana. Hapa hakuna kazi kama unavyoona ujenzi umesimama hakuna fedha. Tunasikia bosi hajalipwa huko serikalini ndiyo bado anafuatilia malipo lakini sisi tumeambiwa tukiulizwa tuseme tuna tatizo la simenti ambalo ni tatizo la kitaifa kwa sasa.

" Kama unaweza twende tukupeleke kwa msimamizi wetu ukamuhoji ila uwe unajiamini labda watatulipa. Sisi tunasubiri akipata pesa kutoka serikalini akitulipa ndiyo basi tunatafuta kazi sehemu nyingine maana hapa, wiki hii mnafanya kazi wiki ijayo hakuna kazi sasa tunajiuliza hiyo serikali inatoa hela kwa wiki?" alisema mmoja wa mafundi hao.

Msimamizi wa mradi alipofikiwa na Tanzania PANORAMA Blog na kuulizwa, kwanza alielekeza afuatwe ofisini ambako alichukua simu na kuwasiliana na Makao Makuu ya kampuni yake kisha alisema;

"Unasema kuna wenzako kwenye gari wanakusubiri .... Umesema hujapiga picha.... Hili ni eneo la ‘site,’ mtu yoyote haruhusiwi kuingia humu bila kibali cha makao Makuu, awe Mkuu wa Mkoa, awe Waziri anapotaka kuja hapa ni lazima awe na kibali kwa sababu anaweza kuangukiwa na kitu kizito kama nondo au ubao ukaumia.

" Sasa nimeongea na Makao Makuu nadhani umeona naongea na simu, kama una maswali nenda huko watakujibu na kama unataka kutembelea hapa uje na kibali cha maandishi kutoka makao makuu.

"Tena tumekuheshimu sana kwa sababu umeingia eneo ambalo haliruhusiwi ila kwa vile una wenzako nje njoo nikupitishe njia salama usije ukajikwaa halafu mkaanza kutunga uongo, " alisema.

Tanzania PANORAMA Blog lilifika Makao Makuu ya Kampuni ya Namis Corporate Ltd yaliyopo Mbezi Africana kwa ajili ya kupata maelezo ya kasimama kwa ujenzi wa soko la Tandale na kuelezwa kuwa mkataba wa ujenzi una kipengele kinachozuia kutoa taarifa yoyote ya mwenendo wa ujenzi isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Akizungumza kuhusu katazo hilo alilodai lipo kwenye mkataba huo, Meneja Mradi aliyejitambulisha kwa jina la James Msumali alisema changamoto zinazowakabili katika ujenzi huo anaweza kuzizungumzia iwapo atapata kibali cha maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa.

"Mimi ndiyo meneja mradi na ndiye ninayeweza kuzungumza, bosi unayetaka kuonana naye hayupo. Utaratibu upo hivi, mkataba wetu una kipengele kinachoelekeza kuwa taarifa yoyote ya mradi haiwezi kutolewa mpaka kwa kibali cha Mkurugenzi.

"Tena kibali cha maandishi au anipigie simu yeye mwenyewe aseme nitoe taarifa kwako. Kwa hiyo nenda Manispaa kamtafute Mkurugenzi muombe kibali au mwambie anipigie simu ndiyo uje nikueleze hicho unachotafuta," alisema Msumali.



Alipofikiwa na kuelezwa hali hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagulimjuli alihoji ni kwanini Tanzania PANORAMA Blog linafuatilia mradi wa ujenzi wa soko la Tandale wenye kelele nyingi badala ya  kuandika maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ghorofa la Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni au ujenzi wa bwawa na kufua umeme la Mwalimu Nyerere.

"Kwanini Ujenzi wa Soko la Tandale ambalo lina kelele nyingi saaana. Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa ghorofa hiyo hapo sasa umefikia ghorofa ya nne, kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere? Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa, kwanini huandiki kuhusu stendi Mpya ya mabasi ya Dar es Salaam?

" Lakini nimeitwa mahali sasa siwezi kuwasikiliza kwa sababu nimeitwa na wakubwa. Njooni kesho," alisema Kagurumjuli.

Alipotafutwa siku iliyofuata alisema kusimama kwa mradi huo kunachangiwa na sababu nyingi ikiwemo ya kukosekana kwa saruji. Alipoulizwa kuhusu zuio la kuandika habari za soko hilo alisema halitambui isipokuwa mwananchi anapaswa kufuata utaratibu kuingia katika miradi ya aina hiyo.

"Hilo zuio silijui na nitoe barua kwa mwandishi kwenda kuandika habari kutoka lini hiyo. Hao watakuwa na yao lakini wananchi wanaruhusiwa kuingia kwenye miradi ya aina hiyo kwa kufuata utaratibu maalumu ulioandaliwa na (project manager) Meneja mradi," alisema Kagurumjuli.

Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa Namis Corporate Ltd, Thomas Uiso alikataa kuzungumza lolote na kueleza aulizwe meneja mradi, Msumali.

Tanzania PANORAMA inaendelea kufuatilia sakata hilo.

 

JWTZ, TISS KUOMBWA KUMSAKA MWANAFUNZI ALIYEPOTEA ST MARY’S

 


NA MWANDISHI WETU

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) wataombwa kumsaka mwanafunzi aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde, Labna Said Salim ambaye ametoweka tangu Oktoba 4, 2020.

Taarifa iliyotolewa na Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kinondoni, Joseph Kapere kwa Tanzania PANORAMA Blog leo, imeeleza kuwa taasisi hizo zitaombwa kusaidia kumsaka mwanafunzi huyo popote alipo baada ya jitihada za Jeshi la Polisi kumsaka kushindwa kuzaa matunda.

Kapere ambaye alikuwa akizungumzia mwenendo wa uchunguzi wa timu ya maafisa wanne wa serikali iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo kuchunguza mazingira ya kutoweka kwa mwanafunzi huyo na kumsaka mahali alipo, ameeleza kuwa tume hiyo imekwishamkamata kijana anayedaiwa kuishi na mwanafunzi huyo baada ya kutoroka shuleni na sasa inasubiri wanafunzi wa kidato cha nne wamalize mitihani ya taifa ili iweze kuchukua hatua zaidi.

Timu hiyo inayomsaka mwanafunzi huyo inaundwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kinondoni, Afisa Usdalama wa Wilaya ya Kinondoni, Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kinondoni na Mdhibiti Ubora wa Elimu Kanda.

“Uchunguzi wetu unaendelea lakini hatufanikiwa kumpata huyo mtoto. Tiumekwishamkamata na kumuhoji kijana ambaye inadaiwa kuwa yule mtoto alitorokea kwake, anakiri kwamba ni kweli alikwenda chumbani kwake lakini huwa anakwenda mara kwa mara na marafiki zake na kwamba aliondoka akamuacha hapo chumbani akiwa na marafiki zake.

“Lakini wale marafiki zake saba tuliowakuta nyumbani kwa baba yake mahali ambako anaishi huyo kijana wakiwa wanavuta bangi wameeleza kuwa ni kweli huyo mtoto alipotoroka shule ule usiku alikwenda kwa huyo kijana wakawa wote kabla ya kutoweka kusikojulikana,

“Na wale waliomsindikiza kwenda kwenye hiyo nyumba ambao ni wanafunzi wenzake nao tuimewahoji na wanakiri kuwa mtoto Labna alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na huyo kijana na kwamba siku hiyo walimsindikiza akaenda kwake.

“Sasa unajua wanafunzi wengi wa kidato cha nne wako kwenye mitahani, tunasubiri jumatano wamalize ili tuiwakutanishe pamoja wote tuliowahoji watueleze kwa pamoja ndipo tuchukua hatua zaidi,” alisema Kapere.

Alipoulizwa hatua zitakazochikuliwa na timu hiyo baada ya kukamilisha uchunguzi wake alisema itaandika taarifa itakayoipeleka kwa Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi lakini itaomba Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) vialikwe kusaidia kumsaka mwanafunzi huyo kutokana na jeshi la polisi kutopata mafanikio.

“Sisi tutaandika taarifa yetu na tumeishaanza kuandika, tutaeleza upungufu wote tulioubaini kwenye hiyo shule na tutatoa mapendekezo tutapeleka kwa mkuu wa wilaya ambaye ndiye aliyeunda timu hii. Lakini niseme tu moja kwa moja katika mapendekezo yetu tutashauri TISS na JWTZ waalikwe kumsaka huyu mtoto kwasababu nadhani polisi wanahitaji msaada maana mpaka sasa hawajafanikiwa,” alisema Kapere.



Mwanafunzi Labna alitoweka shuleni Oktoba 4, 2020 na taarifa za awali zilieleza kuwa alitoroka akiwa na wafunzi wanzake kwenda kwenye maeneo ya starehe na kutokomea moja kwa moja.

Zephania Maduhu ambaye ni mjomba wa mwanafunzi huyo aliyekuwa akimlipia ada ya shule aliieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa ana wasiwasi mtoto wake ameuawa kwani tangu Oktoba 4, 2020 alipopotea akiwa chini ya uangalizi wa shule, taarifa za kupotea kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake, Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa mwanafunzi huyo akiulizia kama ameishafika nyumbani jambo ambalo limekuwa liibua hisia zinazotia shaka kuhusu usalama wa mtoto huyo.

“Huyo mtoto ninamlea mimi, ninamlipia ada ya shule mimi, ni mtoto wa dada yangu, anasoma St. Mary’s, Mbezi Makonde. Oktoba 8, mwaka huu, matron wake anaitwa Sarah Murra, alimpigia simu mama yake, yaani dada yangu akimuuliza kama Labna kafika nyumbani.

 “Dada yangu ambaye wakati huo alikuwa mkoani Shinyanga akashangaa akamuuliza amefikaje nyumbani wakati yupo shule au shule zimefungwa ghafla tena? Yule matron akamjibu ametoroka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 hivyo alikuwa anataka kujua kama yupo nyumbani, dada akamwambia yeye yupo mkoani Shinyanga na anajua mtoto wake yupo shule.

 “Aliporudi kutoka safari Shinyanga akakuta mtoto hajapatikana na shule haijatoa taarifa polisi yaani hata wasiwasi hawana. Ikabidi yeye aende kutoa ripoti Kituo cha Polisi cha Stakishari, waliponipa taarifa mimi nikafunga safari mpaka shuleni.

 “Pale shuleni nikamkuta mkuu wa shule anaitwa Reca Ntipoo, akanijibu mtoto alitoroka shule usiku hajarudi na hawajui alipokwenda. Nikauliza kama wamefanya jitihada zozote za kumtafuta na kama wameisha ripoti polisi akasema hilo ni jukumu letu wazazi.

 “Sasa hapo nikakasirika nikamuuliza mtoto tumemkabidhi shule na ada tumelipa kumbe katoroka zaidi ya mwezi hata taarifa polisi hawajatoa, hapo akajibu labda tukamtafute kwenye vijiwe vyao vya usiku wakitoroka huwa wanakwenda huko ambako wanafunzi wenzake wanavijua, akamuita mwanafunzi mmoja kweli akatuelekeza huko wanakokwenda usiku.

 “Nilikuwa na rafiki yangu alinisindikiza tukaenda kumtafuta huko hatukumpata, hatukuwa na jinsi ikatubidi sisi tukatoe taarifa nyingine kituo cha Polisi Goba na polisi tulipowaelezea nao walishangaa  kweli kweli.

 “Sasa RB tunayo ni STK/RB/10714/2020 na mpelelezi wa shauri hilo ni Afande Gwake Mwakapande. Sidhani kama yupo hai sisi tunaamini ameishakufa lakini uongozi wa shule hii ndiyo umetuulia mtoto wetu. Polisi wanajua sasa sijui kama wameishawauliza au bado,” alisema Maduhu.

 Kapere amekwishaieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa Mkuu wa Shule ya St. Mary’s, Ntipoo alikiri kufanya uzembe kutotoa taarifa polisi na kwa wazazi kuhusu kupotea kwa mwanafunzi Labna na kwamba kutoroka kwa wanafunzi usiku na kwenda kwenye maeneo ya starehe ni jambo alilolikuta shuleni hapo hivyo hata baada ya kutoonekana kwa Labna aliamini kuwa alitoroka usiku kwenda kwenye mambo yake lakini angerudi.

 Aidha Kapere amwishaeleza kuwa timu imebaini kuwa Shule ya Sekondari ya St Mary’s ni chafu, haina ulinzi wa kutosha na ukuta wake haufai.

 

 

 

KAMANDA BUKOMBE AONDOLEWA KINONDONI, APELEKWA MAKAO MAKUU


NA MWANDISHI WETU

ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni (RPC), Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Edward Bukombe, amehamishwa kituo chake cha kazi na kupelekwa makao makuu.   

Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog kutoka vyanzo vyake vya habari zimeeleza kuwa Kamanda Bukombe sasa anakwenda kuongoza kitengo cha picha na matukio na kwamba uhamisho huo ni wa kawaida.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, nafasi ya Kamanda Bukombe imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ramadhani Kingai ambaye katika mahojiano yake leo na Tanzania PANORAMA Blog amethibitisha kurithi wadhfa huo akitokea mkoani Arusha.