banner

Tuesday, October 27, 2020

MAJALIWA: ZIMEBAKI SIKU SABA TU, TUWE MAKINI

 

 

NA MWANDISHI WETU

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa Mtwara wawe makini kuamua wanataka kiongozi wa aina gani kwasababu zimebakia siku saba tu kabla ya uchaguzi mkuu.

"Zimebaki siku saba tu ndugu zangu kabla ya siku ya uchaguzi. Lazima tuwe makini na tutafakari ni aina gani ya kiongozi tunamtaka," alisema.

Alitoa wito huo leo (Jumanne, Oktoba 20, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Kitangari, Wilayani ya Newala kwenye mkutano uliofanyika stendi kuu ya Newala.

Majaliwa ambaye yuko mkoani Mtwara kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Newala Vijijini,  Maimuna Mtanda na mgombea udiwani wa Lata ya Kitangari, Mfaume Ladda.

Amesema wananchi wanapaswa kuamua aina ya kiongozi wa kumchagua ili aweze kuleta maendeleo ya haraka. "Maendeleo hayana chama sababu tukijenga shule watasoma watoto wetu wote. Kwa hiyo, nawaomba sana tumchague Dk. Magufuli ili aje aendeleze mazuri aliyoyaanzisha."

Kuhusu uboreshwaji wa miundombinu, Majaliwa alisema upanuzi wa Bandari ya Mtwara unaendelea ambapo sh. bilioni 170 zilitolewa na Serikali ili ujenzi wa kitako kikubwa cha kuweza kuweka mizigo na magari zaidi ya 600 ufanyike.

"Vilevile sh. bilioni 50 zimetolewa kwa ajili ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara ili uweze kupokea moja kwa moja ndege kubwa kutoka Ulaya bila kulazimika kutua kwanza Dar es Salaam."

Kuhusu ujenzi wa barabara ya lami, Majaliwa alisema Serikali ilitoa sh. bilioni 89 kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa km. 210 ambayo itaunganisha wilaya nne na itaanzia Mtwara Vijijini - Nanyamba - Newala - Masasi.

Kuhusu zao la Korosho, Majaliwa alisema mfumo wa mnada ulisaidia bei ya korosho ipande na kufikia sh.4,000/- lakini msimu uliopita bei ilizorota kwa sababu ya ugonjwa wa Corona.

"Wanunuzi wa ndani walipanga kununua Korosho kwa sh. 1,800/- lakini Mheshimiwa Rais aliamua kutoa sh. bilioni 900 ili zitumike kulipia ununuzi wa korosho za wakulima.

Majaliwa ambaye awali alisimamishwa na wananchi wa Kata ya Mkwiti, alisema Serikali imetoa sh. milioni 600 kufanya upembuzi yakinifu wa barabara ya kutoka Mtama hadi Tandahimba kupitia Mkwiti ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

“Kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Mtama hadi Tandahimba kutasaidia kuboresha biashara na usafiri baina ya maeneo hayo na Jiji la Dar es Salaam.”

Pia alimuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, na kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Tandahimba kwa tiketi ya CCM, Katani Ahmad Katani na mgombea udiwani wa kata ya Mkwiti, Ismail Iddi Said.

 

 

 

 

 

 

 

Sunday, October 18, 2020

MAABARA NA KLINIKI ZA MIFUGO KUANZISHWA WILAYA ZA WAFUGAJI - MAJALIWA

 


NA MWANDISHI WETU

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema serikali ijayo ya CCM itaanzisha maabara na kliniki za kutibu mifugo katika wilaya zote za wafugaji nchini, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Orgosorok, Wilaya ya Ngorongoro, Mkoa wa Arusha, katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Waziri Mkuu, mji mdogo wa Loliondo.

"Tumeanza kuwatumikia na kuwahudumia wafugaji kwa kuhakikisha kuwa wana maeneo mazuri ya malisho, na sasa tumeamua kuwachimbia mabwawa ya kunywesha mifugo.

"Bado tutaendelea kubaini maeneo ya wafugaji na kuwachimbia mabwawa na majosho. Na sasa, tunaanzisha maabara kwa ajili ya kupima magonjwa ya mifugo. Tunajenga kliniki kwa ajili ya kutibu mifugo kwenye wilaya zote zinazofuga na pia tunatoa dawa ya ruzuku kwa ajili ya mifugo," amesema.

Amesema Serikali ya CCM itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuhudumia mifugo na hivyo, wafugaji waendelee kufuga kwa uhakika ili Watanzania wanufaike na sekta ya mifugo.

Kuhusu barabara, Majaliwa amesema Serikali ijayo ya CCM itajenga kwa kiwango cha lami barabara yenye urefu wa km. 300 kutoka Mto wa Mbu hadi Ngorongoro.

Majaliwa amewaomba wananchi wa Ngorongoro wamchangue tena Dk. John Magufuli ili aendelee kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ameonyesha uwezo mkubwa katika kukusanya mapato ya Serikali na kusimamia matumizi yake.

Amesema: “Kazi ya Urais ni kazi nzito na haina nafasi ya kufanyiwa majaribio na mtu ambaye hana historia na uongozi wa nchi,” na kusisitiza kuwa: “Amani ya nchi inategemea kwa kiwango kikubwa na kiongozi aliyeko madarakani, kwani akiwa kiongozi mahiri ataisimamia amani iliyopo, na akiwa kiongozi legelege amani itayumba.”

Wakati huohuo, Mama Mary Majaliwa amewaomba wakazi wa Ngorongoro wampe kura zote za ndiyo Dk. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa Jimbo la Ngorongoro William Ole Nasha na wagombea udiwani wote kwa tiketi ya CCM.

Naye mgombea ubunge wa Jimbo la Ngorongoro kwa tiketi ya CCM, William Tate Ole Nasha amesema maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha awamu ya kwanza ya miaka mitano ya Dk. Magufuli ni makubwa na hakika historia ya maendeleo imeandikwa katika Wilaya ya Ngorongoro.

“Kwa mara ya kwanza, Chuo cha Ufundi VETA kinajengwa Ngorongoro na Serikali imetoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho katika eneo la Samunge, Loliondo," amesema.

Ole Nasha amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya na hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwani wananchi wa Ngorongoro hawatalazimika kwenda Arusha au nchi jirani ili kupata matibabu.

Majaliwa yuko mkoani Arusha kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa Jimbo la Ngorongoro, William Ole Nasha na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM.

 

Saturday, October 17, 2020

POLISI WALIA UKATA

 

NA MWANDISHI WETU

ASKARI Polisi wa Kituo Kidogo cha Polisi Mtongani kilichopo Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam wameeleza kuwa wanakabiliwa na ukata mkali unaokwamisha utekelezaji wa majukumu yao ya kulinda usalama wa raia na mali zao.

Wameeleza hayo baada ya Tanzania PANORAMA Blog kuhoji sababu za mafaili ya kesi zilizofunguliwa kituo kidogo cha Polisi Mtongani kushindwa kupelekwa Kituo cha Polisi Kawe kwa zaidi ya siku tano.

Akijibu swali la mmoja wa walalamikaji jana asubuhi lililohoji; kwanini mafaili ya kesi zilizofunguliwa hayajapelekwa Kawe kwa zaidi ya siku tano wakati siyo mbali, mmoja wa askari aliyekuwa kituo hapo alisema "muzee walishindwa tu kukwambia ukweli, hali ni mbaya, tuna hali mbaya hadi usafiri wa kupeleka mafaili hapo Kawe hatuna."

Alipoambiwa kuwa mlalamikaji yupo tayari kuwasaidia polisi usafiri wa kubeba faili hizo kuzipeleka Kituo cha Polisi Kawe kwa sababu amesumbuka muda mrefu na anatumia gharama kuzunguka vituo vya polisi Kawe na Mtongani, polisi huyo alisema hilo haliruhusiwi ila atajitahidi kutafuta njia ya kuyapeleka mafaili hayo.

Dalili za kuwepo kwa ukata kwa polisi hao zilianza kuonekana Jumamosi ya Oktoba 10, 2020 baada ya Mwandishi wa Tanzania PANORAMA Blog kufika kituo kidogo cha Polisi Mtongani akiwa amejeruhiwa vibaya na wezi waliokuwa wamewateka abiria kwenye daladala na kuwashambulia kwa bisibisi na mapanga kabla ya kuwanyang'anya pesa, simu na vitu vingine vya thamani walivyokuwa navyo kisha kuwatupa pembezoni mwa barabara.

Mwandishi wetu aliwaeleza polisi hao kuwa alipanda daladala la wahalifu akiwa na abiria wenzake wawili katika kituo cha daladala cha njia panda ya kwenda Hotel ya Bahari Beach ambapo mmoja wa wahalifu alikuwa ametangaza kuwa linakwenda stendi ya Makumbusho.

"Hatukujua kama ndani ya daladala hilo kulikuwa na wahalifu, mmoja wao alitangaza kuwa linakwenda Makumbusho hivyo mimi na abiria wenzangu wawili tukapanda pale kituo cha kona ya kwenda Bahari Beach. Lakini lilipoondoka tu wale wezi ambao walikuwa zaidi ya 20 mle ndani wakaanza kupiga kelele kama washangiliaji wa mpira na dreva akawasha muziki kwa sauti ya juu ikawa kelele tu.

" Hapo wakaanza kutushambulia, walianza na mama tuliyepanda naye akawa anakataa kuachia pochi yake, wakamkata panga mkononi ukabaki unaning'inia, wakachukua kila kitu wakamsogeza mwisho kabisa wa gari na kijana mwingine niliyepanda naye yeye alikuwa amekatwa mapanga mawili kichwani na kuwapa kila kitu akabaki analia tu.

"Mimi nilijaribu kumwambia dreva apunguze sauti ya muziki ajabu alitoa upanga akanambia tulia kisha akaendelea kuendesha gari kwa kasi. Kwa sababu mlango wa gari ulikuwa umefungwa na taa zilikuwa zimezimwa niliiona hatari iliyokuwa mbele, sikuwa mbishi niliwapa pesa, simu nao walinisachi na kuchukua kila walichoona kinafaa.

" Walinishambulia kwa ngumi tu lakini walinijeruhi vibaya usoni na mdomoni nadhani kwa sababu sikuwa mbishi na walikwenda kunitupa Kona ya Mbuyuni wakawa wameondoka na mama ambaye wamemkata mkono, namba ya gari nimeikariri ina mstari wa njano ya wekundu wa damu ya mzee, tukiifukuza tunaikamata kwa sababu nimeona huko mbele kuna foleni," alijieleza mwandishi wetu mbele ya kaunta ya polisi.

Polisi aliyekuwa akisikiliza maelezo yake alisema hawana uwezo wa kuifukuza daladala hiyo kwa sababu eneo hilo la kipolisi hadi Kawe lina gari moja tu bali anamfungulia RB na atampa PF 3 akatibiwe kwa sababu alikuwa akivuja damu nyingi.

"Hatuna jinsi ya kulifukuza mzee tuna gari moja tu nalo muda huu linasambaza askari kwenye malindo, we acha kumzungumzia mama aliyekatwa mkono naye watamtupa huko mbele atakwenda kutoa taarifa kituo chochote cha polisi kama ulivyofanya wewe.

" Nakufungulia faili nakupa PF 3 nenda Hospitali ukatibiwe angalia tisheti yote ulivyoloa damu, jihurumie umeumua sana acha kuhurumia wengine.

"Kwa sababu umetutajia namba na rangi za mstari wa hilo daladala Jumatatu tu tutalikamata.  Hao wahalifu wamekuwa tishio huwa wanaenda beach huko kila weekend kufanya uhalifu msiwe mnapanda daladala zao maana ndiyo mbinu yao mpya.

"Katibiwe nenda nyumbani kasikilizie hali yako Jumatatu asubuhi saa mbili uwe polisi Kawe utamkuta mpelelezi wa kesi yako, kesho jumapili hakuna kazi hivyo jumatatu litakamatwa hilo daladala," alisema askari aliyekuwa kaunta.

Jumatatu, Oktoba 12, 2020, saa tano asubuhi mwandishi wetu alifika Kituo cha Polisi na kuonyesha RB namba KMT/RB/2428/2020 aliyopewa kituo kidogo cha Polisi Mtongani ili aonyeshwe mpelelezi wa kesi yake lakini polisi aliyekuwa kaunta alisema mafaili kutoka Mtongani hayajafika kituoni hapo wala hakuna kumbukumbu zake zilizorekodiwa kwenye rejista kituoni hapo na kuelekezwa arudi Mtongani kesi yake itashugulikiwa huko.

Alhamis, Oktoba 16, 2020 mwandishi wetu alirejea kituo cha Polisi Mtongani ambako baada ya polisi kukagua makaratasi mengi yaliyokuwa kaunta walisema faili lake bado lipo kituoni hapo likisuburi utaratibu wa kupelekwa Polisi Kawe.

"Siyo peke yako mzee, faili zote hizi hazijapelekwa hali mbaya, hakuna usafiri.  Wewe uwe unapitapita pale Polisi Kawe siku tukilipeleka utalikuta ataambiwa," alisema askari aliyekuwa kaunta.

Alipoelezwa kuwa kwa sababu ya kupunguza usumbufu na gharama za usafiri na pia kuokoa muda anaweza kutoa msaada wa usafiri ili mafaili hayo yapelekwe Kawe aliambiwa hilo haliruhusiwi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura alipotafutwa jana kwa simu yake ya kiganjani kuzungumzia ukata huo alipokea msaidizi wake na kueleza kuwa yupo kwenye kikao atafutwe muda mwingine.

Alipotafutwa leo alipokea simu na kueleza kuwa hasikii vizuri anachoulizwa pengine yupo eneo baya hivyo atumiwe ujumbe na alipotumiwa ujumbe kwenye simu yake akiulizwa kuhusu kuwepo ukata katika eneo lake la utawala na kukwama kwa mafaili ya kesi kituo cha Polisi Mtongani kwa siku tano, hakujibu.

UJENZI UBUNGO 'INTERCHANGE' KUKAMILIKA DISEMBA 30, 2020

 

NA MWANDISHI MAALUMU

UJENZI wa barabara za juu eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam, maarufu kama Ubungo Interchange unaozikutanisha barabara tatu za Mandela, Sam Nujoma na Morogoro unatarajiwa kukamilika Disemba 30, mwaka huu.

Ujenzi huo unaotekelezwa na serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), sasa umefikia asilimia 81.

Akizungumza katika mahojiano maalumu  meneja wa mradi huo, Mhandisi Barakaeli Mmari amesema ujenzi huo ulioanza Mei, 2017 unaendelea vizuri na hivi sasa barabara zote mbili za juu zimefunguliwa kwa majaribio.

“Kwa mara ya kwanza Mei 30, 2020 tuliifungua barabara ya ghorofa ya chini ya Morogoro kwa majaribio ambapo tuliruhusu magari kupita na Septemba 30, 2020 barabara ya ghorofa ya pili ya Nelson Mandela / Sam Nujoma ilifunguliwa kwa majaribio.

"Ni matarajio yetu kuwa ifikapo Disemba 30, 2020 ujenzi utakuwa umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wataendelea kufaidi barabara hiyo," amesema Mhandisi  Mmari.

Amesema lengo la ujenzi wa barabara za juu ni kuondoa msongamano katika makutano ya barabara hizo eneo la Ubungo uliokuwa ukisababisha watu kuchelewa kufika  kwenye kwenye shughuli zao kwa wakati na kupoteza muda mwingi ambao ungetumika kuwaongeza kipato.

Akizungumza kuhusu matumizi ya barabara hiyo kwa madereva amesema katika eneo hilo kuna barabara ngazi (ghorofa) tatu, ya chini, ya kati na ya juu, ambapo ngazi ya chini itatumiwa na magari yanayotoka Mjini kwenda Mwenge, Mwenge-Kimara, Kimara-Buguruni na Buguruni kwenda Mjini.

Amesema itatumiwa pia na magari yote yatakayokuwa yanapinda kushoto kwenye maungio hayo.

Mhandisi Mmari amesema ngazi ya kati  itatumiwa na magari yanayotoka Kimara kwenda mjini na yatokayo mjini kwenda Kimara na ngazi ya juu itatumiwa na magari yanayotoka  Mwenge kwenda Buguruni na  Buguruni kwenda Mwenge.

Aidha, Mhandisi Mmari amesema barabara za juu zimejumuisha njia maalumu kwa ajili ya mabasi ya mwendo kasi. 

Kuhusu ajira, Mhandisi Mmari amesema mradi huo umetoa ajira kwa watanzania wengi wakiwemo wananchi wa kawaida mpaka wahandisi ambao wanashughulika na kazi za kihandisi katika kutekeleza ujenzi kwa ufanisi.

“Tumeajiri wafanyakazi kati ya 800 hadi 900 kwa mwezi na kati ya hao Wafanyakazi wa nje ni asilimia 10 tu huku wafanyakazi wazawa wakiwa asilimia 90, kwa hiyo ujenzi huu umeleta faida kwa watanzania wengi hasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam," Amesema Mhandisi Mmari.

Kwa upande mwingine, Wananchi wa Ubungo waliozungumzia mradi huo hawakuficha furaha yao kwa kufunguliwa kwa majaribio barabara hizo.

“Tunaishukuru Serikali kwani foleni sasa hakuna, magari yanapita vizuri na sisi tunapita vizuri tu, naamini tunakoelekea tutafanya mambo mazuri zaidi ya haya,"  ameeleza Bakari Juma.

Naye Johnson Mwakalukwa amesema barabara hiyo imesaidia wasafiri kutoka mikoani kwani sasa wakifika Mbezi wanakutana na barabara ya njia nane na wanakuja kumalizia na Ubungo 'Interchange,' hivyo kuokoa muda mwingi waliokuwa wakiutumia kwenye foleni.

Thursday, October 15, 2020

TANROAD DAR ES SALAAM WALALAMIKA SHERIA ZA BARABARA KUPUUZWA

 

NA MWANDISHI WETU

UONGOZI wa Wakala wa Barabara (Tanroad) Mkoa wa Dar es Salaam, umesema maagizo ya kisiasa yanayotolewa na wanasiasa kuhusu matumizi na utunzaji wa miundombinu ya barabara yamekuwa yakikinzana na sheria na miongozo ya utunzaji barabara.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Mipango Tanroad Mkoa wa Dar es Salaam, Elisony Mweladzi alipofanya mahojiano na TANZANIA PANORAMA wiki iliyopita kuhusu malalamiko ya wafanyabiashara wa eneo la Kimara Mwisho kupangishwa vibanda vya biashara vilivyo katika eneo la Tanroad kwa bei kubwa.

Katika majibu yake, Mweladzi alisema sheria na miongozo iliyopo hairuhusu mtu yeyote kufanya biashara pembeni ya barabara hivyo Tanroad haijakodisha eneo lolote lililo pembezoni mwa barabara isipokuwa wafanyabiashara wamekuwa wakivamia maeneo yaliyo wazi na kuyatumia  kibiashara kwa kufuata maagizo ya kisiasa yanayotolewa na wanasiasa.

"Kwanza nataka ieleweke hakuna mwekezaji eneo la Kimara mwisho bali kuna wafanyabiashara pale. Kweli lile ni eneo la Tanroad na imelitoa kwa wafanyabiashara wapatao sita, Wanne upande wa kulia na wawili wapo upande wa kushoto wa barabara.

"Hawa tumewakodisha maeneo hayo na wanalipa kwa dola (fedha za marekani) lakini kwa ajili ya maegesho ya magari na siyo kuweka vibanda vidogo vidogo vya wafanyabiashara wa bidhaa za vyakula na nyinginezo.

" Sasa sisi tunatoa vibali vya kuegesha magari tu lakini hatuhusiki hata kidogo na vibali vya wafanyabiashara wadogo ndani ya hifadhi ya barabara. Na tulishachukua hatua hapo awali na kama wapo wengine basi tutawashughulikia.

"Tatizo linalotukwamisha kusimamia ipasavyo jambo hili ni matamko ya kisiasa yanayotolewa na viongozi wa kisiasa kwa sababu hawazingatia sheria, wanawaruhusu kufanya biashara pembezoni mwa barabara jambo ambalo ni kinyume kabisa cha sheria. Nadhani hata wewe mwandishi unaujua ugumu wa kusimamia sheria panapokuwa na upinzani kutoka kwa wanasiasa," alisema  Mweladzi.

Awali wafanyabiashara wadogo wa eneo Kimara Mwisho waliiambia TANZANIA PANORAMA kuwa mwekezaji aliyepewa eneo la pembezoni mwa barabara na Tanroad anawatoza fedha nyingi za kukodi vibanda vya biashara na hata wasiokuwa na vibanda nao wanatozwa bila kujali wana vitambulisho vya wamachinga.

Walisema vibanda vya mbogamboga na mama lishe vinatozwa kuanzia sh 50,000 hadi 300,000 na wapiga kiwi viatu ambao kikawaida hawana vibanda wao wanalipia eneo wanaloweka meza sh 45,000 hadi 50,000.

Akijibu hilo, Mweladzi alisema malalamiko hayo yanashagaza kwa sababu wafanyabiashara hao walipata kufika ofisini kwake wakimsifia na kumshukuru mfanyabiashara aliyewapa eneo hilo na kuwaruhusu kufanya biashara bila kuwatoza chochote na waliomba Tanroads inamruhusu awajengee choo.

TANZANIA PANORAMA lilifika ofisini kwa mfanyabiashara huyo eneo la Kimara Mwisho na kukutana na wasaidizi wake walioeleza kuwa bosi wao hayupo hivyo wapewe muda wawasiliane naye kabla ya kujibu maswali waliyoulizwa.

Wakijibu kwa niaba ya bosi wao walisema, Biashara yote inayoendelea katika eneo hilo la pembezoni mwa barabara inatambuliwa na kusimamiwa na Meneja wa Tanroads wa Mkoa wa Dar es Salaam hivyo kuna jambo lolote linalohitaji ufafanuzi basi aulizwe yeye.