Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea cheti cha ushindi wa Ubunge wa Jimbo la Ruangwa kutoka kwa Msimamizi Mkuu wa uchaguzi wa Jimbo hilo, Frank Chonya (kushoto) kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Oktoba 29, 2020. Kulia ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
MWANDISHI WETU
MBUNGE Mteule wa Jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa amepokea cheti cha kumtambulisha rasmi kuwa mbunge mteule wa jimbo
hilo.
Alipokea cheti hicho Alhamisi, Oktoba 29, 2020 kutoka kwa
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ruangwa, Frank Chonya katika ofisi za
Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.
Akizungumza mara baada ya kupokea cheti hicho, Majaliwa
amesema anamshukuru Mungu kwa kuwezesha yote na kuwafikisha hapo na kuwavusha
salama kipindi cha kampeni kwa karibu miezi miwili
Majaliwa ambaye alikuwa ameambatana na mkewe Mama Mary
Majaliwa, alisema kipekee anashukuru vyama vya siasa wilayani humo kwa
kumuamini na kuthamini maendeleo.
"Sisiti kusema vyama vya siasa vimeendelea kuthamini
maendeleo ya wilaya yetu. Lakini katika hili, niseme kwamba tumeliweka mbele
sana suala la maendeleo ya wilaya yetu. Ninawashukuru sana."
Alisema kupatiwa cheti cha kumtambua rasmi kuwa mbunge
mteule hadi atakapoapishwa, kumetokana na imani yao kubwa waliyoionesha kwake
na kuamua apite bila kupingwa.
"Leo niko hapa mbele yenu, nimemaliza muda wangu wa
2015-2020, mmenivumilia, mmenipa ushirikiano na mmenisaidia kuifanya kazi yangu
vizuri. Ninawashukuru viongozi wote na wananchi wa Ruangwa kwa mchango wenu
uliowezesha Ruangwa ipige hatua ya maendeleo. Mimi, mke wangu na watoto
tunawashukuru sana."
Alisema katika miaka mitano iliyopita, yako mambo mengi
waliyofanya na katika kipindi hiki yako mambo yaliyobakia kama kupeleka umeme
na maji vijijini. "Ninawaahidi kushirikiana nanyi ili kufikia malengo
yaliyowekwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM."
Aliwapongeza madiwani wote walioshinda katika kata zote 22
na kuwaahidi kuwa yuko pamoja nao kuijenga Ruangwa.
Mapema, akizungumza kabla ya kumkabidhi cheti chake,
Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Ruangwa, Frank Chonya alisema jimbo hilo
lenye kata 22, lilikuwa na watu waliojiandikisha kupiga kura 106,043 na
lilikuwa na vituo 311 vya kupigia kura.
Alisema vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo ni CCM, ACT
Wazalendo, CUF na CHADEMA.
"Kabla ya uchaguzi, kata saba, wagombea wake kutoka
Chama cha Mapinduzi walipita bila kupingwa. Jana baada ya uchaguzi, CCM
imeshinda kata 12, ACT kata mbili na CUF kata moja." Alisema.