banner

Wednesday, December 16, 2020

GULAM ATAFAKARI KUPAMBANA NA UBALOZI WA INDIA

 

Mwenyekiti wa Kampuni za MeTL, Gulam Dewji

NA MWANDISHI WETU

MFANYABIASHARI mwenye ukwasi wa kutosha ambaye kampuni, viwanda, mashamba na biashara zake zimetoa ajira kwa Watanzania na raia wa kigeni anatafakari kujibu mapigo dhidi ya Ubalozi wa India uliyoyataja makampuni yake kuwa siyo sehemu salama kufanya kazi.

Wiki iliyopita, siku moja baada ta Gulam kumpa maagizo mmoja wa wasaidizi wake kutuma ujumbe kwa Tanzania PANORAMA Blog wa kusaka suluhu baina ya menejimenti za Kampuni za Mohamedi Enterprises Tanzania Limited (MeTL) na wafanyakazi wa kigeni wanaodai kunyanyaswa alisema anajipanga kujibu mapigo.

Gulam alisema amesikitisha na tamko la ubalozi wa India lililosambazwa mitandaoni kwa sababu linalenga kuwatetea watu wanaomuibia na kumsumbua.

“Ndiyo nimeliona tamko kwani nani kasema hajui kuwa ni tamko la Ubalozi wa India, lakini mimi nasema nakusanya ushahidi halafu nitatoa tangazo kwa vyombo vya habari kwa sababu ubalozi unatetea wezi, unatetea watu wanaoniibia na kunitesa sana na hata polisi wanazo taarifa hizi. Sasa ninazungumza na ubalozi halafu nitatoa statement yangu ambayo mimi nitaitoa kama tangazo,” alisema Gulam.   

AWALI Tanzania PANORAMA Blog, iliripoti kuwa uongozi wa kampuni zilizo chini ya mwamvuli wa Mohamedi Enterprises Tanzania Limited (MeTL) umesema utatafuta njia ya kumaliza mgogoro baina yake na wafanyakazi ambao ni raia wa India katika meza ya mazungumzo.

Hayo yameelezwa na mmoja wa maafisa wa kampuni hiyo aliyetumwa na Mkurugenzi wa MeTL, Gulam Dewji kutoa ufafanuzi kwa Tanzania PANORAMA Blog kuhusu andishi lililowekwa kwenye mitandao ya kijamii likiwatahadhalisha raia wa India wote kuepuka kufanya kazi katika Kampuni za MeTL.

Andiko hilo mtandaoni linaeleza kuwa Ubalozi wa India umekuwa ukipokea kwa mfululizo malalamiko ya wafanyaakazi wa Kampuni za MeTL kunyanyaswa na uongozi pamoja na mwajiri wao kuwafungulia kesi za kughushi mahakamani kiasi cha kusababisha wanafamilia wa wafanyakazi hao kulazimika kurejea India.

Kwamba Mwenyekiti wa Makampuni ya MeTl, Gulam Dewji na maafisa waandamizi wamekuwa wakiwafanyia vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wafanyakazi hao wanapofikisha malalamiko kwao.

Linahitimishwa kwamba raia wote wa India wasikubali kuajiriwa na Kampuni za MeTL kutokana na mwenendo usiofaa wa viongozi wake wa juu.

Alipoulizwa Mwenyekiti Gulam, kuhusu suala hilo kupitia simu yake ya kiganjani alisema aandikiwe maswali kwa maandishi ili ayajibu na alipoandikiwa, muda mfupi baadaye mtu mmoja mwenye asili ya kiasia alituma ujumbe kwa njia ya whatsapp akieleza kuwa ametumwa na Gulam kufikisha ujumbe kwa Tanzania PANORAMA Blog.

Ujumbe aliuotuma ulisomeka; ‘Bwana Dewji amezungumza na sisi na ametuhakikishia uwajibikaji wa menejimenti katika kulinda maslahi ya wafanyakazi. Tumekubaliana kuwa na mazungumzo ya kina, tungependa kutatua jambo hili kwa njia ya mazungumzo.’

Ujumbe mwingine chini ya huo aliuotuma ulisomeka; ‘leo hii mmelalamika mazingira ya watu wenu ila tusema ukweli pia mnawanyanyasa sana Watanzania sema tu wanashindwa nani wa kuwasemea pia kutokana na hali za maisha yao ila mazingira ya ufanyaji kazi siyo.

Jitahidi za Tanzania PANORAMA Blog kuzungumza na Ubalozi wa India kuhusu suala hili zinaendelea.    

MWANAFUNZI ALIYEPOTEA ST. MARY’S APATIKANA

 

Labna Said

NA MWANDISHI WETU

LABNA Salim Said,  mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s iliyopo Mbezi Makonde ambaye alipotea tangu Oktoba 4, 2020, amepatikana.

Mwanafunzi huyo alipatikana Disembe 12, 2020, eno la Banana Relini akiwa amewekwa kinyumba na mwanaume ambaye jina lake halikufahamika mara moja baada ya kufanikiwa kuwakimbia polisi waliokwenda kuwakamata.

Taarifa za kupatikana kwa Labna zilithibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC) Ramadhani Kingai katika mahojiano mafupi kwa njia ya simu ambaye alisema, taarifa za kupatikana kwa mwanafunzi huyo anazo lakini hawezi kuongea zaidi kwa sababu yupo kwenye kikao.

Mama mzazi wa Labna anayefahamika kwa jina la Rabia Swedan alisema walipata taarifa za kuwepo kwa mtoto wao eneo Banana Relini usiku na walifika eneo hilo wakiwa wameambatana na polisi wawili na kumkuta akiwa amelala chini pamoja na aliyemtorosha.

“Inasikitisha, tulipata taarifa za huyu mtoto kuwepo Banana Relini usiku, tukaenda Kituo cha Polisi Stakishari kuomba polisi, tukapewa wawili tukaambatana nao mpaka kwenye hiyo nyumba tukawakuta wamelala chini. Yule bwana aliyekuwa naye alipotuona na polisi akakurupuka akakimbia, sasa kwa sababu polisi walikuwa wawili hawakuweza kumfukuza.

“Mtoto alikuwa hoi, tulimpeleka Stakishari polisi huo usiku wa saa saba akakaa hapo wakimuhoji mpaka saa 12.00 asubuhi, kwa jinsi alivyokuwa wakatuambia tumpeleke hospitali.

“Tukampeleka Hospitali ya Amana na baada ya matibabu tukamchukua hadi Kituo cha Polisi Goba kwa sababu ndiko kesi yake inakopelelezwa, nao  wakamuhoji wakaturudishia tuendelee kumtibu ila akiwa na nafuu tutampeleka tena polisi,” alisema Swedan.   

Mwanafunzi msichana Labna wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 na kutokomea kusikojulikana hadi alipopatikana Disemba 12.

Labna alitoweka akiwa chini ya uangalizi wa shule lakini taarifa za kutoweka kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake, Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa Labna akiulizia kama ameishafika nyumbani.

Katika hatua ya kushangaza, uongozi wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s haukutoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mwanafunzi huyo na badala yake wazazi ndiyo walioripoti tukio la mtoto wao kupotea akiwa shuleni.

 

 

Thursday, December 10, 2020

MeTL YAZUNGUMZIA TUHUMA ZINAZOIANDAMA

 

Mwenyekiti wa Makampuni ya MeTL, Gulam dewji

NA MWANDISHI WETU

UONGOZI wa Kampuni zilizo chini ya mwamvuli wa Mohamedi Enterprises Tanzania Limited (MeTL) umesema utatafuta njia ya kumaliza mgogoro baina yake na wafanyakazi ambao ni raia wa India katika meza ya mazungumzo.

Hayo yameelezwa na mmoja wa maafisa wa kampuni hiyo aliyetumwa na Mkurugenzi wa MeTL, Gulam Dewji kutoa ufafanuzi kwa Tanzania PANORAMA Blog kuhusu andishi lililowekwa kwenye mitandao ya kijamii likiwatahadhalisha raia wa India wote kuepuka kufanya kazi katika kampuni za MeTL.

Andiko hilo mtandaoni linaeleza kuwa Ubalozi wa India umekuwa ukipokea kwa mfululizo malalamiko ya wafanyaakazi wa Kampuni za MeTL kunyanyaswa na uongozi pamoja na mwajiri wao kuwafungulia kesi za kughushi mahakamani kiasi cha kusababisha wanafamilia wa wafanyakazi hao kulazimika kurejea India.

Kwamba Mwenyekiti wa Makampuni ya MeTl, Gulam Dewji na maafisa waandamizi wamekuwa wakiwafanya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wafanyakazi hao wanapofikisha malalamiko kwao.

Linahitishwa kwamba raia wote wa India wasikubali kuajiriwa na Kampuni za MeTL kutokana na mwenendo usiofaa wa viongozi wake wa juu.

Gulam

Alipoulizwa Mwenyekiti Gulam, kuhusu suala hilo kupitia simu yake ya kiganjani alisema aandikiwe maswali kwa maandishi ili ayajibu na alipoandikiwa, muda mfupi baadaye mtu mmoja mwenye asili ya kiasia alituma ujumbe kwa njia ya whatsapp akieleza kuwa ametumwa na Gulam kufikisha ujumbe kwa Tanzania PANORAMA Blog.

Ujumbe aliuotuma ulisomeka; ‘Bwana Dewji amezungumza na sisi na ametuhakikishia uwajibikaji wa menejimenti katika kulinda maslahi ya wafanyakazi. Tumekubaliana kuwa na mazungumzo ya kina, tungependa kutatua jambo hili kwa njia ya mazungumzo.’

Ujumbe mwingine chini ya huo aliuotuma ulisomeka; ‘leo hii mmelalamika mazingira ya watu wenu ila tusema ukweli pia mnawanyanyasa sana watanzania sema tu wanashindwa nani wa kuwasemea pia kutokana na hali za maisha yao ila mazingira ya ufanyaji kazi siyo.

Jitahidi za Tanzania PANORAMA Blog kuzungumza na Ubalozi wa India kuhusu suala hili zinaendelea.    

BOSI AIRTEL ALIVYOKWAPUA MAMILIONI BILA KUBAINIKA

 



NA MWANDISHI WETU

IMEBAINIKA kuwa, mmoja wa waliokuwa maofisa wa juu wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, alichota mamilioni ya shilingi za kampuni hiyo kwa kufanya nayo biashara hewa.

Ili kufanikisha uchotaji wa mamilioni hayo, kigogo huyo ambaye jina lake tunalifadhi kwa sasa, alifungua kampuni iliyokuwa ikitoa huduma kwenye minara ya simu ya Aitel na kuweka mtu wa kuisimamia ili kuficha uhusika wake.

Uchunguzi wa awali kuhusu ufisadi wa mali za umma uliofanywa na Tanzania PANORAMA Blog kwa Kampuni ya Aitel umeonyesha kuwa, Airtel baada ya kubadilishwa jina kutoka Zain, kigogo huyo aliyekuwa amekwishachota pesa nyingi kwa kufanya biashara za udanganyifu, alifungua kampuni ambayo haraka haraka ilianza kupewa zabuni za Airtel.

Kwa mujibu wa uchunguzi, kampuni iliyofunguliwa ( jina tunalo) iliwekwa chini ya usimamizi wa mtu mwingine ambaye alikuwa akiripoti moja kwa moja kwa kigogo huyo na yeye alikuwa akifika kukagua mwenendo wake siku za mwisho wa wiki ambazo wafanyakazi hawakuwa kazini.

Uchunguzi umeonyesha kuwa kigogo huyo alitumia nafasi yake katika Airtel kutazama mianya ya kuiwezesha kampuni yake kupata zabuni hewa zenye thamani ya mamilioni ya fedha, jambo ambalo lingefanikiwa kampuni hiyo ingefungwa au kubadilishwa jina na iwapo ingetiliwa shaka na kuanza kufuatiliwa na mamlaka serikali, kigogo huyo angeacha kazi na kukimbilia nje ya nchi; na hiyo ingetegemea na hali halisi ya wakati ambao ingegundulika.

Tanzania PANORAMA Blog katika uchunguzi wake imebaini kuwa kigogo huyo baada ya kufanikiwa kuchomeka jina la kampuni yake kwenye menejimenti ya Airtel kama moja ya kampuni zenye sifa ya kufanya biashari kubwa, kwa kutumia wadhfa wake alianza kushawishi zabuni zenye thamani kubwa ipewe kampuni yake.

Uchunguzi umebaini kuwa haraka haraka bosi huyo aliwasilisha kwa menejimenti pendekezo la kununuliwa kwa jenereta mbili kubwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuendesha minara ya Airtel.

Pendekezo hilo liliainisha bei ya jenereta hizo kuwa; moja gharama yake ni Dola za Marekani 240,000 na ya pili Dola za Marekani 480,000 ambazo zingekaa makao makuu tayari kufanya kazi wakati wa dharura.

Mchakato wa ununuzi wa jenereta hizo ulifanyika haraka na malipo yalifanyika kwa mikupuo mitatu. Mkupuo wa kwanza ulihusisha malipo ya Dola za Marekani 480,000 ambazo zililipwa kwa invoice mbili na Dola za Marekani 240,000 invoice moja.

Hata hivyo Tanzania PANORAMA Blog inaripoti kwa uhakika kuwa manunuzi ya jenereta hizo hayakufanyika bali pesa hizo ziliwekwa kibindoni na bosi huyo.

Taarifa zinaeleza kuwa wakati akiandaa mpango mwingine wa kuchota zaidi ya Dola za Marekani 500,000 Serikali ya Awamu Tano ilianza kufuatilia mwenendo wa kampuni hiyo ili kuinusuru isife kutokana na hali mbaya iliyokuwa nayo.

"Baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kufuatilia mwenendo wa kampuni kwa karibu, bosi alijua sasa atakuwa hatarini akaamua kuacha kazi mara moja kabla hajafanikisha mipango yake mingine.

"Wakaguzi wa serikali walipokuja waligundua kuwa manunuzi ya hizo jenereta yalikuwa hewa kwani hakukuwa na hizo jenereta bali hela za Airtel zilikwapuliwa zikawekwa mfukoni lakini hawakuweza kumnasa bosi kwa sababu alikuwa ameishaacha kazi.

"Na ilikuwa ngumu kumnasa kwa sababu yeye alikuwa nyuma ya ile kampuni ambayo aliweka mtu wake, huyo ndiyo akawa bosi. Huyo ndiyo alipata msukosuko kidogo lakini sasa yupo huru.

"Kwa sababu serikali ilishindwa kumbaini hakukimbilia nje ya nchi bali alikwenda nje kidogo ya jiji akajenga shule yake kubwa huko akaanzisha na biashara zake nyingine. Mke wake ambaye alikuwa mtumishi wa NSSF aliyeaacha kazi ili kusaidiana na yule bwana aliyemuweka kuendesha hiyo kampuni ya wizi sasa ndiyo anatokeza zaidi kwenye biashara zake, " kilieleza chanzo cha ndani cha taarifa.

Tanzania PANORAMA Blog itaripoti ufisadi huu kwa kina mara baada ya kukamilisha uchunguzi wake.

 

Wednesday, December 9, 2020

POLISI WAACHIWA MZIGO WA KUMTAFUTA MWANAFUNZI ALIYEPOTEA ST MARY'S SEK

 

Katibu Mkuu Akwilapo

NA MWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu wa Wazara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Leonard Akwilapo amesema wajibu wa kumtafuta  mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St Mary's, Labna Said Salim aliyepotea akiwa chini ya uangalizi wa shule ni wa Jeshi la Polisi

Ameyasema hayo jana katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog ambayo ilimuuliza mchango wa wizara kumtafuta mwanafunzi huyo aliyepotea Oktoba 4, 2020.

"Hilo jambo wenye wajibu ni polisi na ndiyo maana sisi halijafika kwetu na hata kama lingekuwa limefika tungelipeleka polisi kwa sababu wao ndiyo wenye wajibu wa mambo kama hayo," alisema Akwilapo.

Labna


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ramandani Kingai alipoulizwa jana kuhusu hatua waliyofikia katika msako huo alisema mpasa sasa hawafikiwa kumpata mwanafunzi huyo

Alipoulizwa kuhusu vijana saba waliokamatwa wakivuta bangi nyumbani kwa Kamishna Mstaafu wa Jeshi Magereza ambaye jina lake limehifadhiwa, Kamanda Kingai alisema vijana hao ambao ni wanafunzi bado wanafanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne hivyo wanasubiriwa mpaka watakapomaliza ndipo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Taarifa ya uchunguzi wa awali wa kupotea kwa mwanafunzi huyo iliyotolewa na Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kinondoni, Joseph Kapere ambaye ni mjumbe wa timu iliyoundwa na Serikali ya Wilaya ya Kinondoni kuchunguza kupotea kwa mtoto huyo, mahali alipo sasa na mazingira ya kutoweka kwake ilieleza kuwa timu hiyo ilithibitisha pasipo shaka kuwa Shule ya Sekondari ya St Mary’s Mbezi Makonde imepungukiwa sifa zinazostahili kutoa elimu kwa mwanafunzi.

Wajumbe wengine katika timu hiyo ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ufisa Usalama na Mdhibiti wa Ubora wa Elimu Kanda.

Kapere alisema tayari Mkuu wa Shule ya St. Mary's, Recca Ntipoo amehojiwa na kuungama kutenda makosa katika baadhi ya mambo kwenye sakata hilo na kwamba aliipeleka timu hiyo mahali alikodai Labna alikwenda kuishi na mpenzi wake baada ya kutoroka shule.

Alisema timu ilibaini shule hiyo ilifanya makosa kutotoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mtoto na pia kukaa kimya  siku nne bila kutoa taarifa kwa wazazi kuhusu kutoweka kwake wala kuwajulisha kuwa amewaeleza walimu hataki shule.

Katika maelezo yake Kapere alisema, Ntipoo aliungama kufahamu vitendo vya mwanafunzi kutoka shule kwa kuruka ukuta usiku na kwenda maeneo hatarishi kwao jambo ambalo Mwalimu huyo aliliona kuwa  la kawaida kwa sababu alikuta likifanyika shuleni hapo.

Aidha, Kapere alisema timu ilibaini shule hiyo kuwa na mazingira machafu, kukosa ulinzi wa kutosha na kutokuwa na ukuta imara.

Alisema mambo mengine yaliyogundulika katika uchunguzi wa timu hiyo ni kubainika kwa nyumba ya Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Magereza ambayo ina shamba la bangi  ambamo walikutwa wavulana saba, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya St Mary's waliokuwa wakivuta pamoja.

 Mwanafunzi msichana Labna wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 na kutokomea kusikojulikana na hadi sasa hajapatikana.

Labna alitoweka akiwa chini ya uangalizi wa shule lakini taarifa za kutoweka kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa Labna akiulizia kama ameishafika nyumbani.

Katika hatua ya kushangaza, uongozi wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s haukutoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mwanafunzi huyo na badala yake wazazi ndiyo walioripoti tukio la mtoto wao kupotea akiwa shuleni.