 |
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Partick Mfugale |
MAISHA ya wananchi wa
Tanzania kwa kiasi kikubwa sasa yamebadilika. Miundombinu ya barabara na
madaraja ya kisasa ambayo hapo awali Watanzania waliyaona kwenye picha na
sinema zilizoandaliwa katika nchi za Ulaya na Amerika, sasa ipo nchini na kwa
kiwango kikubwa imekuwa msaada kwa safari zao wenyewe na pia kusafirisha mazao
na bidhaa za biashara.
Mabadiliko hayo ya maisha
ya wanachi wa Tanzania yameenda sambamba na mabadiliko ya mwenendo wa uchumi wa
Taifa. Uchumi wa Tanzania sasa unakuwa kwa kasi kubwa na tayari umekwishachumpa
kutoka kwenye uchumi wa nchi masikini hadi uchumi wa kati, miaka mitano kabla
ya matarajio.
Wataalamu wa uchumi
wanaeleza kuwa kuchumpa kwa uchumi wa Tanzania kutoka ule wa nchi masikini hadi
uchumi wa kati miaka mitano kabla ya matarajio kumewezeshwa pamoja na mambo
mengine, ujenzi wa miondombinu imara na yenye kuvutia jambo linaloifanya nchi,
kwanza kufikika sehemu zote lakini pia kuwa na mandhari ya kuvutia.
Haikuwa kazi rahisi
kuyafikia mafanikio haya katika sekta ya ujenzi wa miundombinu. Wapo Watanzania
waliotokwa jasho la damu na chumvi kuyawezesha na kinara wa utiririkaji jasho
la kuigeza Tanzania kuwa mithili ya paradiso ni Rais John Pombe Magufuli ambaye
kwa miaka mitano ya awamu ya kwanza ya utawala wake, ratiba yake ya kulala
imebadilika, analala kwa saa chache na muda mwingi yupo kibaruani akichuruzikwa
jasho.
 |
Rais John Pombe Magufuli |
Wa pili katika hili, ni
Wakala wa Barabara, (Tanroads) ambao mabadiliko ya kiutendaji katika taasisi za
serikali yaliyoasisiwa na Rais Dk. Magufuli mara tu alipoingia marakani mwaka
2015 yaliwafanya wawe kama wanajimu kwa kutafasili ndoto za mnyama mdogo
anayejulikana kwa jina la Kakakuona.
Kakakuona hutembea akiota
kuwa akikutana na binadamu na kufanikiwa kukimbia kwa kasi ili binadamu
asimkamate kisha akajificha asionekane basi atakuwa na uwezo wa kibinadamu wa
kufanya maendeleo makubwa katika maisha yake.
Binadamu nao, (baadhi ya
jamii) huota kwamba wakimuona mnyama mdogo Kakakuona, basi kuna baraka mbele
yao kwa sababu mnyama huyo haonekana hovyo hovyo. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa
kwa Tanroads ambayo ndoto za Kakakuona kutaka kukimbia kwa kasi kisha ajifiche
ili awe kama binadamu na maendeleo yake imezifanya ziwe za kweli na kwa
Watanzania waliokuwa wakiota siku wakikutana na Kakakuona basi kuna baraka
inayokuja mbele yao, Tanroads imezigeuza ndoto zao kuwa kweli.
Ukweli huu umo katika kazi
za kutukuka zilizofanywa na Tanroads kwenye ujenzi wa madaraja ambayo sasa
yamegeuka kuwa vivutio vya utalii kwa watanzania wenyewe na hata baadhi ya
wageni kutoka mataifa ya nje kutokana na muonekane wake wa kuvutia. Mbali na
hilo, ndoto za watanzania katika baadhi ya maeneo ambako kulikuwa na matatizo makubwa
ya kufika na hata uhai wa watu kupotea kwa sababu ya kukosa madaraja, hali hiyo
sasa haipo, madaraja yamejengwa na hapa chini ni orodha fupi ya madaraja hayo.
DARAJA LA MAGUFULI
Kwa mujibu
wa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi
Dorothy Ntenga, Daraja la Magufuli lililojengwa katika Mto Kilombero
liligharimu zaidi ya shilingi bilioni 50 ambazo zote zilitolewa na Serikali.
Kwamba ujenzi wa daraja
hilo umezingatia viwango vilivyowekwa kwenye mkataba na mkandarasi ambaye ni
kampuni ya M/S China Railway 15 Group Corporation.
Daraja hilo
linarahisisha shughuli za usafirishaji wa mazao, ufugaji na madini katika
Wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero.
Ilikuwa ndoto ya muda
mrefu kwa wananchi hao kupata daraja na wakati likijengwa, mmoja wa wakazi wa
maeneo hayo, Zainabu Mtalanga alipata kumwambia aliyekuwa Waziri wa Ujenzi,
Profesa Makame Mbarawa kuwa; “Tunaishukuru serikali kwa ujenzi wa
daraja hili kwani limekuwa mkombozi kwetu wananchi wa Wilaya za Ulanga na Kilombero.
“Hapo nyuma vifo vingi
vimetokea pasipo kutegemewa wakati tukitumia kivuko kufuata huduma za kijamii
wilaya jirani ambapo kuna huduma zote za muhimu.”
DARAJA LA MAGARA
Taarifa ya Meneja wa
Tanroads Mkoa wa Manyara, Mhandisi Bashiri Rwesingisa, kuhusu ujenzi wa Daraja
la Magara inaeleza kuwa ujenzi wake uligharimu zaidi ya shilingi bilioni 12
Lilijengwa na Mkandarasi
M/s China Railway Seventh Group likiwa na urefu wa mita 84 na barabara za
maingilio KM 4 na linaunganisha Hifadhi ya Taifa ya Manyara na Tarangire
kupitia Mayoka, pamoja na kuunganisha mashamba makubwa ya mpunga na miwa
yaliyopo ng’ambo ya pili ya Mto na Masoko ya Babati na Arusha.
Daraja la Magara ni
kichocheo cha ukuaji wa utalii na uchumi katika Mkoa wa Manyara na Taifa
kwa ujumla likiwa umbali wa KM 21 kutoka Mbuyu wa Mjerumani katika barabara kuu
ya Babati – Arusha na sasa linawezesha kuvuka Mto Magara katika barabara ya
Mkoa ya Mbuyu wa Mjerumani – Mbulu yenye urefu wa KM 49.
DARAJA LA MOMBA
Meneja wa Tanroads wa Mkoa
wa Rukwa, Mhandisi Ndelalutse Karoza analieleza daraja hilo kuwa ni kiunganishi
cha mkoa huo na Mkoa wa Songwe kwa upande wa Bonde la Ziwa Rukwa na limejengwa
kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania kwa 100.
Kwa mujibu wa Karoza, gharama
za ujenzi wa Daraja la Momba ni shilingi bilioni 17.7 na limejengwa na
Kampuni ya ukandarasi ya Genjio Engineering Group Cooperation ya China
Karoza anasema ujenzi wa daraja hilo ni muhimu sana kwa
mikoa ya Rukwa na Songwe pamoja na Tanzania kwa ujumla na kubainisha kuwa
ukamilifu wa daraja hilo utawainua wananchi kiuchumi na kijamii ikiwemo
kupunguza gharama za usafirishaji wa mazao.
Daraja la Mto Sibiti lipo
Iramba mkoani Sindiga. Lina urefu wa mita 83 na gharama za ujenzi wake ni
shilingi bilioni 19.2
DARAJA LA NYERERE
(KIGAMBONI)
Lipo Kurasini jijini Dar
es Salaam na linamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na NSSF.
Ni daraja la aina ya
kuning’inia lililojengwa na Mkandarasi China Railway Jiangchang Engineering (T)
Ltd na China Major Bridge Engineering Company. Lina urefi wa mita 680 na upana
wa mita 27.5 na gharama yake ya ujenzi ni Dola za Marekani milioni 136
Daraja la Nyerere ndilo
linalovuka mkondo wa kurasini jijini Dar es Salaam likiwa na njia sita za
kupitisha magari. Daraja la Nyerere ndilo kubwa kuliko yote Afrika Mashariki na
linavutia sana kutokana na kujengwa kwa ustadi.