 |
Mkurugenzi Manispaa ya Kinondoni, Aon Kigurumjuli |
NA MWANDISHI WETU
MKURUGENZI wa Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni, Aron
Kigurumjuli, sasa ameanza kufanya vituko kwa kuwazuia waandishi wa habari
kuingia na vitendea kazi vya aina yoyote ofisini kwake wanapokwenda kufanya
naye mahojiano.
Kigurumjuli ameweka mlinzi katika mlango wa ofisi yake
anayechagua watu wa kuingia na pia anachagua nani na yupi asiingie ambapo leo
asubuhi, mlinzi huyo ameizuia Tanzania PANORAMA Blog kuonana na bosi wake kwa
ajili ya kufanya mahojiano ikiwa na 'notebook' na kalamu mpaka itii sharti la
kuingia mikono mitupu.
Katika hatua ya kushangaza, Kigurumjuli pia, wiki iliyopita
alitoa maneno ya kashfa na kejeli kwa viongozi waandamizi wa serikali pamoja na
aidha; leo hakupokea simu wala kujibu meseji kwa watu aliopanga miadi ya
kukutana nao ofisini kwake.
Vituko hivi vya Kigurumjuli vimekuja siku chache baada ya
yeye mwenyewe kuieleza Tanzania PANORAKA Blog kuwa amepata presha hivyo hawezi
kwenda kazini baada ya kuripotiwa kwa taarifa za kukwama kwa ujenzi wa soko
jipya la Tandale huku taarifa nyingine zikieleza kuwa ana hasira kwa sababu
ya kuripotiwa kwa mkwamo wa ujenzi wa soko la Tandale na amejiapiza
kuwashughulikia wanaofuatilia habari hiyo.
Katika tukio la leo asubuhi, Kigurumjuli alikuwa ametoa
miadi ya kukutana ili azungumzie matatizo yaliyokwamisha ujenzi wa soko la
Tandale. Miadi hiyo haikufanikiwa baada ya mlinzi aliyemuweka mlangoni kutaka
aachiwe vitendea kazi vyote vya Tanzania PANORAMA Blog ikiwa ni pamoja na begi
alilotaka apewe alishike.
"Toa vitu vyako vyote kwenye kibegi chako weka hapo
kwenye kiti, hilo begi nipe hapa nilishike ukitoka utachukua vitu vyako nitakupa
na begi lako," alieleza mlinzi ambaye jina lake halikufahamika.
Alipoelezwa kuwa ndani ya begi kuna kalamu, 'notebook' na
nyaraka kadhaa na kufunguliwa akague na mwandishi alieleza yupo tayari
kupekuliwa, alisisitiza kuwa bosi wake
ameagiza waandishi wasiingie na kitu chochote isipokuwa wao tu.
"Hii ni amri, kalamu na karatasi zako toa weka kwenye
kiti, begi nipe hapa nitakushikia hatuna sababu ya kubishana," alisema kwa msisitizo.
Tanzania PANORAMA Blog haikumpatia begi mlinzi huyo kama
alivyokuwa akisisitiza kwa sababu lilikuwa na taarifa za kuwepo kwa mipango
miovu ya kupandikiziwa vitu visivyofaa kisha wangeitwa wana usalama kupekua
begi hilo na kukuta vitu hivyo kabla ya kuwatia matatani kwa lengo la
kuwazuia wasiripoti taarifa za soko la Tandale.
 |
Unezi wa soko jipya la Tandale ulipokuwa umefikia mwezi Agosti |
Kabla ya kuondoka eneo hilo, lilimpigia simu Mkurugenzi
huyo kumjulisha hali halisi ilivyo hapo nje ya mlango wa ofisi yake, simu yake
ilisikika ndani ikiita lakini hakuipokea na pia alitumiwa ujumbe mfupi wa maneno
mara tatu ambao aliusoma lakini hakujibu.
Katika mahojiano ya wiki iliyopita kuhusu kukwama kwa
ujenzi wa soko la Tandale na kuweka zuio kwa waandishi wa habari kiripoti
habari za soko hilo bila ruhusa yake, Kigurumjuli alisema yeye binafsi ndiye
aliyekwenda kutafuta fedha za ujenzi wa soko la Tandale, Wizara ya Fedha na Mipango
na alipewa za kutosha ila tatizo lililopo sasa ni kukosekana kwa saruji.
Alipoulizwa sababu iliyomfanya yeye binafsi kwenda wizarani
kushawishi kutolewa kwa fedha huku tayari aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI,
Selemani Jaffo akiwa amekwishatoa tamko kuhusu ujenzi wa masoko yaliyokuwa
kwenye mpango wa kujengwa..... haraka alilikatisha swali hilo na kuanza
kung'aka.
"Ni kinini hicho, Selemani Jafo ndiyo kitu gani hicho.
Hapa unaongea na Mkurugenzi, upo ofisini kwa mkurugenzi usinitajie majina ya
ajabu ajabu wewe. Huyo Jafo wakati nahangaika hazina alikuwepo?
 |
Kigurumjuli |
“Fedha nimetafuta mimi na nimepewa mimi na nimekujibu hivyo
au ulisikia kuna Jafo au huyo mkuu wenu wa mkoa? Wao kazi si kutembea tu na .....
(anasema maneno yasiyofaa) kwenye miradi tunayotafuta sisi. Hivi sasa tuna
tatizo la saruji usiniletee mambo ya wanasiasa hapa. Uliza swali jingine,"
alisema kwa sauti ya juu Kigurumjuli.
Aidha Kigurumjuli alikana kutoa maagizo kwa mkarandasi
yanayowataka waandishi wa habari kuwa na vibali vya maandishi kutoka kwake
wanapotaka kuripoti habari za ujenzi wa soko la Tandale.
Taarifa ya kuwepo kwa zuio hilo kwa waandishi wa habari lilitolewa
na meneja miradi wa Kampuni Namis, James Msumali ambaye baada ya kufikiwa na
Tanzania PANORAMA Blog na kuombwa kuzungumzia mkwamo huo alisema mkataba wa
ujenzi una kipengele kinachozuia kutolewa kwa taarifa yoyote ya ujenzi wa soko
mpaka kiwepo kibali cha maandishi kutoka Kigurumjuli.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa kampuni ya Namis Thomas Uiso ambaye
awali alikuwa ameitaka Tanzania PANORAMA Blog kumpelekea maswali kwa maandishi
ili naye apate wasaa mzuri wa kuyajibu, ombi ambalo lilitekelezwa, alipotafutwa
wiki iliyopita aliandika ujumbe wenye maneno machafu badala ya kujibu na muda
mfupi baadaye aliufuta kisha alipiga simu na kueleza kuwa soko la Tandale
linasimamiwa na Mkurugenzi ambaye ameagiza mwandishi yoyote anayetaka taarifa
aelekezwe kwake.
"Maswali gani, wewe......(anaandika maneno ambayo
hatuwezi kuyaandika). Nimepata taarifa zako mkurugenzi kanambia, hovyo sana
wewe kumbe unachimba maisha ya watu. Ukimtaja Jafo au Kunenge ndiyo watu
tutaogopa? Hao ni ........ (Anaandika maneno yasiyoandikika) huu ni utawala
mwingine utapotea wewe na hutamuona Jafo wala Kunenge.
"Kuwa gentleman
bhana, hapa ni mjini, haya ni maisha. Kwani unadhani hata nikiharibikiwa wewe
ndiyo utapewa hiyo tenda? Ondoa huo uchafu ulioandika kwenye blog yako halafu kamuone
mkurugenzi maisha yaendelee...., »alisema Uiso.
WIKI ILIYOPITA Tanzania
PANORAMA Blog iliripoti kuwa, WAKATI
Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa imeelekeza nguvu kubwa kwenye ujenzi wa
miundombinu, shule, hospitali na masoko, jitihada hizo zimeanza kuonyesha
dalili ya kuingia doa baada ya kusimama kwa ujenzi wa soko jipya la Tandale.
Katikati ya hilo, msimamo
wa serikali ya awamu ya tano wa kutoa taarifa zinazohusu shughuli za maendeleo
bila ukiritimba, zinazofanywa na serikali ili kutoa fursa kwa wananchi kujua
miradi inayotekelezwa kwa kodi zao, nao unaonekana kuingia doa baada ya
mkandarasi anajenga soko la Tandale kuweka zuio la upatikanaji wa taarifa hizo.
Haya yamebainika baada ya
Tanzania PANORAMA Blog kufika eneo la ujenzi wa soko jipya la Tandale mapema
wiki iliyopita kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo baada ya kudokezwa
na baadhi ya wafanyakazi kuwa umesimama kutokana na ukosefu wa fedha.
Tanzania PANORAMA baada ya
kufika katika eneo la mradi lilishuhudia mafundi wakiwa wamekaa kivulini huku
ujenzi ukiwa hauendelei na baada ya kuwahoji baadhi yao walisema wanasubiri
kulipwa fedha zao waondoke kwa sababu mahali hapo hakuna kazi tena.
"Bora umekuja na
sijui umeingiaje huku maana hamruhusiwi nyie kuingia humu na wakikuona
watakugawana. Hapa hakuna kazi kama unavyoona ujenzi umesimama hakuna fedha.
Tunasikia bosi hajalipwa huko serikalini ndiyo bado anafuatilia malipo lakini
sisi tumeambiwa tukiulizwa tuseme tuna tatizo la simenti ambalo ni tatizo la
kitaifa kwa sasa.
" Kama unaweza twende
tukupeleke kwa msimamizi wetu ukamuhoji ila uwe unajiamini. Ila sisi tunasubiri
akipata pesa kutoka serikalini akitulipa ndiyo basi tunatafuta kazi sehemu
nyingine maana hata wiki hii mnafanya kazi wiki ijayo hakuna kazi sasa
tunajiuliza hiyo serikali inatoa hela kwa wiki?" alisema mmoja wa mafundi
hao.
Msimamizi wa mradi ambaye
alipofikiwa na Tanzania PANORAMA na kuulizwa kwanza alielekeza afuatwe ofisini
ambako alichukua simu na kuwasiliana na makao makuu ya kampuni yake kisha
alisema;
"Unasema kuna wenzako
kwenye gari wanakusubiri .... umesema hujapiga picha.... hili ni eneo la site,
mtu yoyote haruhusiwi kuingia humu bila kibali cha makao makuu, awe mkuu wa
mkoa, awe waziri anapotaka kuja hapa ni lazima awe na kibali kwa sababu anaweza
kuangukiwa na kitu kizito kama nondo au ubao ukaaumia.
"Sasa nimeongea na
makao makuu, nadhani umeona naongea na simu, kama una maswali nenda huko
watakujibu na kama unataka kutembelea hapa uje na kibali cha maandishi kutoka
makao makuu.
"Tena tumekuheshimu
sana kwa sababu umeingia eneo ambalo haliruhusiwi ila kwa vile una wenzako nje
njoo nikipitishe njia salama usije ukajikwaa halafu mkaanza kutunga uongo,
" alisema.
Tanzania PANORAMA lilifika
Makao Makuu ya Kampuni ya Namis, iliyopo Mbezi Africana ambayo ndiyo iliyopewa
kandarasi ya kujenga soko la Tandale kwa ajili ya kupata maelezo ya kasimama
kwa ujenzi wa soko hilo na kuelezwa kuwa mkataba wa ujenzi una kipengele
kinachozuia kutoa taarifa yoyote ya mwenendo wa ujenzi isipokuwa kwa kibali cha
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Akizungumza kuhusu katazo
hilo lililo kwenye mkataba huo, Meneja Mradi aliyejitambulisha kwa jina la
James Msumali alisema changamoto zinazowakabili katika ujenzi huo anaweza
kuzizungumzia iwapo atapata idhini ya maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa.
"Mimi ndiyo meneja
mradi na ndiye ninayeweza kuzungumza, boss unayetaka kuonana naye hayupo.
Utaratibu upo hivi, mkataba wetu una kipengele kinachoelekeza kuwa taarifa
yoyote ya mradi haiwezi kutolewa mpaka kwa Kibali cha Mkurugenzi.
"Tena Kibali cha maandishi
au anipigie simu yeye mwenyewe aseme nitoe taarifa kwako. Kwa hiyo nenda
Manispaa kamtafute Mkurugenzi muombe kibali au mwambie anipigie simu ndiyo uje
nikueleze hicho unachotafuta," alisema Msumali.
Alipofikiwa na kuelezwa
hali hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kigurumjuli alihoji ni
kwanini Tanzania PANORAMA linafuatilia mradi wa ujenzi wa soko la Tandale wenye
kelele nyingi badala ya kuandika maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ghorofa
la ofisi ya Mkurugenzi au ujenzi wa bwawa na kufua umeme la Mwalimu Nyerere.
"Kwanini Ujenzi wa
Soko la Tandale ambalo lina kelele nyingi saaana. Kwanini huandiki kuhusu
ujenzi wa ghorofa hiyo hapo sasa umefikia ghorofa ya nne, kwanini huandiki
kuhusu ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere? Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa
Reli ya Kisasa, kwanini huandiki kuhusu stendi Mpya ya mabasi ya Dad es Salaam?
" Lakini nimeitwa
mahali sasa siwezi kuwasiliza kwa sababu nimeitwa na wakubwa. Njooni
kesho," alisema Kagurumjuli.
Alipotafutwa siku
iliyofuata alisema kusimama kwa mradi huo kunachangiwa na sababu nyingi ikiwemo
ya kukosekana kwa saruji. Alipoulizwa kuhusu zuio la kuandika habari za soko
hilo alisema halitambui isipokuwa mwananchi anapaswa kufuata utaratibu kuingia
katika miradi ya aina hiyo.
"Hilo zuio silijui na
nitoe barua kwa mwandishi kwenda kuandika habari kutok lini hiyo. Hao watakuwa
na yao lakini wananchi wanaruhusiwa kuingia kwenye miradi ya aina hiyo kwa
kufuata utaratibu maalumu ulioandaliwa na (project manager) Meneja mradi,"
alisema Kagurumjuli.
Alipotafutwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Namis Corporate Ltd, Uiso alikataa kuzungumza lolote na kueleza
aulizwe meneja mradi, Msumali.
Tanzania PANORAMA
inaendelea kufuatilia sakata hilo.