banner

Tuesday, December 8, 2020

MKURUGENZI KINONDONI AANZA KUFANYA VITUKO

 

Mkurugenzi Manispaa ya Kinondoni, Aon Kigurumjuli

NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI wa Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni, Aron Kigurumjuli, sasa ameanza kufanya vituko kwa kuwazuia waandishi wa habari kuingia na vitendea kazi vya aina yoyote ofisini kwake wanapokwenda kufanya naye mahojiano.

Kigurumjuli ameweka mlinzi katika mlango wa ofisi yake anayechagua watu wa kuingia na pia anachagua nani na yupi asiingie ambapo leo asubuhi, mlinzi huyo ameizuia Tanzania PANORAMA Blog kuonana na bosi wake kwa ajili ya kufanya mahojiano ikiwa na 'notebook' na kalamu mpaka itii sharti la kuingia mikono mitupu.

Katika hatua ya kushangaza, Kigurumjuli pia, wiki iliyopita alitoa maneno ya kashfa na kejeli kwa viongozi waandamizi wa serikali pamoja na aidha; leo hakupokea simu wala kujibu meseji kwa watu aliopanga miadi ya kukutana nao ofisini kwake.

Vituko hivi vya Kigurumjuli vimekuja siku chache baada ya yeye mwenyewe kuieleza Tanzania PANORAKA Blog kuwa amepata presha hivyo hawezi kwenda kazini baada ya kuripotiwa kwa taarifa za kukwama kwa ujenzi wa soko jipya la Tandale huku taarifa nyingine zikieleza kuwa ana hasira kwa sababu ya kuripotiwa kwa mkwamo wa ujenzi wa soko la Tandale na amejiapiza kuwashughulikia wanaofuatilia habari hiyo.

Katika tukio la leo asubuhi, Kigurumjuli alikuwa ametoa miadi ya kukutana ili azungumzie matatizo yaliyokwamisha ujenzi wa soko la Tandale. Miadi hiyo haikufanikiwa baada ya mlinzi aliyemuweka mlangoni kutaka aachiwe vitendea kazi vyote vya Tanzania PANORAMA Blog ikiwa ni pamoja na begi alilotaka apewe alishike.

"Toa vitu vyako vyote kwenye kibegi chako weka hapo kwenye kiti, hilo begi nipe hapa nilishike ukitoka utachukua vitu vyako nitakupa na begi lako," alieleza mlinzi ambaye jina lake halikufahamika.

Alipoelezwa kuwa ndani ya begi kuna kalamu, 'notebook' na nyaraka kadhaa na kufunguliwa akague na mwandishi alieleza yupo tayari kupekuliwa,  alisisitiza kuwa bosi wake ameagiza waandishi wasiingie na kitu chochote isipokuwa wao tu.

"Hii ni amri, kalamu na karatasi zako toa weka kwenye kiti, begi nipe hapa nitakushikia hatuna sababu ya kubishana," alisema kwa msisitizo.

Tanzania PANORAMA Blog haikumpatia begi mlinzi huyo kama alivyokuwa akisisitiza kwa sababu lilikuwa na taarifa za kuwepo kwa mipango miovu ya kupandikiziwa vitu visivyofaa kisha wangeitwa wana usalama kupekua begi hilo na kukuta vitu hivyo kabla ya kuwatia matatani kwa lengo la kuwazuia wasiripoti taarifa za soko la Tandale.

Unezi wa soko jipya la Tandale ulipokuwa umefikia mwezi Agosti


Kabla ya kuondoka eneo hilo, lilimpigia simu Mkurugenzi huyo kumjulisha hali halisi ilivyo hapo nje ya mlango wa ofisi yake, simu yake ilisikika ndani ikiita lakini hakuipokea na pia alitumiwa ujumbe mfupi wa maneno mara tatu ambao aliusoma lakini hakujibu.

Katika mahojiano ya wiki iliyopita kuhusu kukwama kwa ujenzi wa soko la Tandale na kuweka zuio kwa waandishi wa habari kiripoti habari za soko hilo bila ruhusa yake, Kigurumjuli alisema yeye binafsi ndiye aliyekwenda kutafuta fedha za ujenzi wa soko la Tandale, Wizara ya Fedha na Mipango na alipewa za kutosha ila tatizo lililopo sasa ni kukosekana kwa saruji.

Alipoulizwa sababu iliyomfanya yeye binafsi kwenda wizarani kushawishi kutolewa kwa fedha huku tayari aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jaffo akiwa amekwishatoa tamko kuhusu ujenzi wa masoko yaliyokuwa kwenye mpango wa kujengwa..... haraka alilikatisha swali hilo na kuanza kung'aka.

"Ni kinini hicho, Selemani Jafo ndiyo kitu gani hicho. Hapa unaongea na Mkurugenzi, upo ofisini kwa mkurugenzi usinitajie majina ya ajabu ajabu wewe. Huyo Jafo wakati nahangaika hazina alikuwepo?

 

Kigurumjuli

“Fedha nimetafuta mimi na nimepewa mimi na nimekujibu hivyo au ulisikia kuna Jafo au huyo mkuu wenu wa mkoa? Wao kazi si kutembea tu na ..... (anasema maneno yasiyofaa) kwenye miradi tunayotafuta sisi. Hivi sasa tuna tatizo la saruji usiniletee mambo ya wanasiasa hapa. Uliza swali jingine," alisema kwa sauti ya juu Kigurumjuli.

Aidha Kigurumjuli alikana kutoa maagizo kwa mkarandasi yanayowataka waandishi wa habari kuwa na vibali vya maandishi kutoka kwake wanapotaka kuripoti habari za ujenzi wa soko la Tandale.

Taarifa ya kuwepo kwa zuio hilo kwa waandishi wa habari lilitolewa na meneja miradi wa Kampuni Namis, James Msumali ambaye baada ya kufikiwa na Tanzania PANORAMA Blog na kuombwa kuzungumzia mkwamo huo alisema mkataba wa ujenzi una kipengele kinachozuia kutolewa kwa taarifa yoyote ya ujenzi wa soko mpaka kiwepo kibali cha maandishi kutoka Kigurumjuli.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa kampuni ya Namis Thomas Uiso ambaye awali alikuwa ameitaka Tanzania PANORAMA Blog kumpelekea maswali kwa maandishi ili naye apate wasaa mzuri wa kuyajibu, ombi ambalo lilitekelezwa, alipotafutwa wiki iliyopita aliandika ujumbe wenye maneno machafu badala ya kujibu na muda mfupi baadaye aliufuta kisha alipiga simu na kueleza kuwa soko la Tandale linasimamiwa na Mkurugenzi ambaye ameagiza mwandishi yoyote anayetaka taarifa aelekezwe kwake.

"Maswali gani, wewe......(anaandika maneno ambayo hatuwezi kuyaandika). Nimepata taarifa zako mkurugenzi kanambia, hovyo sana wewe kumbe unachimba maisha ya watu. Ukimtaja Jafo au Kunenge ndiyo watu tutaogopa? Hao ni ........ (Anaandika maneno yasiyoandikika) huu ni utawala mwingine utapotea wewe na hutamuona Jafo wala Kunenge.

"Kuwa gentleman bhana, hapa ni mjini, haya ni maisha. Kwani unadhani hata nikiharibikiwa wewe ndiyo utapewa hiyo tenda? Ondoa huo uchafu ulioandika kwenye blog yako halafu kamuone mkurugenzi maisha yaendelee...., »alisema Uiso.

WIKI ILIYOPITA Tanzania PANORAMA Blog iliripoti kuwa, WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa imeelekeza nguvu kubwa kwenye ujenzi wa miundombinu, shule, hospitali na masoko, jitihada hizo zimeanza kuonyesha dalili ya kuingia doa baada ya kusimama kwa ujenzi wa soko jipya la Tandale.

Katikati ya hilo, msimamo wa serikali ya awamu ya tano wa kutoa taarifa zinazohusu shughuli za maendeleo bila ukiritimba, zinazofanywa na serikali ili kutoa fursa kwa wananchi kujua miradi inayotekelezwa kwa kodi zao, nao unaonekana kuingia doa baada ya mkandarasi anajenga soko la Tandale kuweka zuio la upatikanaji wa taarifa hizo.

Haya yamebainika baada ya Tanzania PANORAMA Blog kufika eneo la ujenzi wa soko jipya la Tandale mapema wiki iliyopita kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo baada ya kudokezwa na baadhi ya wafanyakazi kuwa umesimama kutokana na ukosefu wa fedha.

Tanzania PANORAMA baada ya kufika katika eneo la mradi lilishuhudia mafundi wakiwa wamekaa kivulini huku ujenzi ukiwa hauendelei na baada ya kuwahoji baadhi yao walisema wanasubiri kulipwa fedha zao waondoke kwa sababu mahali hapo hakuna kazi tena.

"Bora umekuja na sijui umeingiaje huku maana hamruhusiwi nyie kuingia humu na wakikuona watakugawana. Hapa hakuna kazi kama unavyoona ujenzi umesimama hakuna fedha. Tunasikia bosi hajalipwa huko serikalini ndiyo bado anafuatilia malipo lakini sisi tumeambiwa tukiulizwa tuseme tuna tatizo la simenti ambalo ni tatizo la kitaifa kwa sasa.

" Kama unaweza twende tukupeleke kwa msimamizi wetu ukamuhoji ila uwe unajiamini. Ila sisi tunasubiri akipata pesa kutoka serikalini akitulipa ndiyo basi tunatafuta kazi sehemu nyingine maana hata wiki hii mnafanya kazi wiki ijayo hakuna kazi sasa tunajiuliza hiyo serikali inatoa hela kwa wiki?" alisema mmoja wa mafundi hao.

Msimamizi wa mradi ambaye alipofikiwa na Tanzania PANORAMA na kuulizwa kwanza alielekeza afuatwe ofisini ambako alichukua simu na kuwasiliana na makao makuu ya kampuni yake kisha alisema;

"Unasema kuna wenzako kwenye gari wanakusubiri .... umesema hujapiga picha.... hili ni eneo la site, mtu yoyote haruhusiwi kuingia humu bila kibali cha makao makuu, awe mkuu wa mkoa, awe waziri anapotaka kuja hapa ni lazima awe na kibali kwa sababu anaweza kuangukiwa na kitu kizito kama nondo au ubao ukaaumia.

"Sasa nimeongea na makao makuu, nadhani umeona naongea na simu, kama una maswali nenda huko watakujibu na kama unataka kutembelea hapa uje na kibali cha maandishi kutoka makao makuu.

"Tena tumekuheshimu sana kwa sababu umeingia eneo ambalo haliruhusiwi ila kwa vile una wenzako nje njoo nikipitishe njia salama usije ukajikwaa halafu mkaanza kutunga uongo, " alisema.

Tanzania PANORAMA lilifika Makao Makuu ya Kampuni ya Namis, iliyopo Mbezi Africana ambayo ndiyo iliyopewa kandarasi ya kujenga soko la Tandale kwa ajili ya kupata maelezo ya kasimama kwa ujenzi wa soko hilo na kuelezwa kuwa mkataba wa ujenzi una kipengele kinachozuia kutoa taarifa yoyote ya mwenendo wa ujenzi isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Akizungumza kuhusu katazo hilo lililo kwenye mkataba huo, Meneja Mradi aliyejitambulisha kwa jina la James Msumali alisema changamoto zinazowakabili katika ujenzi huo anaweza kuzizungumzia iwapo atapata idhini ya maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa.

"Mimi ndiyo meneja mradi na ndiye ninayeweza kuzungumza, boss unayetaka kuonana naye hayupo. Utaratibu upo hivi, mkataba wetu una kipengele kinachoelekeza kuwa taarifa yoyote ya mradi haiwezi kutolewa mpaka kwa Kibali cha Mkurugenzi.

"Tena Kibali cha maandishi au anipigie simu yeye mwenyewe aseme nitoe taarifa kwako. Kwa hiyo nenda Manispaa kamtafute Mkurugenzi muombe kibali au mwambie anipigie simu ndiyo uje nikueleze hicho unachotafuta," alisema Msumali.

Alipofikiwa na kuelezwa hali hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kigurumjuli alihoji ni kwanini Tanzania PANORAMA linafuatilia mradi wa ujenzi wa soko la Tandale wenye kelele nyingi badala ya  kuandika maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ghorofa la ofisi ya Mkurugenzi au ujenzi wa bwawa na kufua umeme la Mwalimu Nyerere.

"Kwanini Ujenzi wa Soko la Tandale ambalo lina kelele nyingi saaana. Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa ghorofa hiyo hapo sasa umefikia ghorofa ya nne, kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere? Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa, kwanini huandiki kuhusu stendi Mpya ya mabasi ya Dad es Salaam?

" Lakini nimeitwa mahali sasa siwezi kuwasiliza kwa sababu nimeitwa na wakubwa. Njooni kesho," alisema Kagurumjuli.

Alipotafutwa siku iliyofuata alisema kusimama kwa mradi huo kunachangiwa na sababu nyingi ikiwemo ya kukosekana kwa saruji. Alipoulizwa kuhusu zuio la kuandika habari za soko hilo alisema halitambui isipokuwa mwananchi anapaswa kufuata utaratibu kuingia katika miradi ya aina hiyo.

"Hilo zuio silijui na nitoe barua kwa mwandishi kwenda kuandika habari kutok lini hiyo. Hao watakuwa na yao lakini wananchi wanaruhusiwa kuingia kwenye miradi ya aina hiyo kwa kufuata utaratibu maalumu ulioandaliwa na (project manager) Meneja mradi," alisema Kagurumjuli.

Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa Namis Corporate Ltd, Uiso alikataa kuzungumza lolote na kueleza aulizwe meneja mradi, Msumali.

Tanzania PANORAMA inaendelea kufuatilia sakata hilo.

TANZANIA INA WATU THABITI AFRIKA- DK ABBAS

 


NA MWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbas emesema watanzania ni watu thabiti  ba webte historia ya kutukuka katika mapambano ya ukombozi wa Bara la Afrika.

Dk Abbas ameyasema hayo jana alipotembelea makao makuu ya ofisi za Ukombozi wa Bara la Afrika kujionea changamoto zinazoukabili.

Akizungumza katika ofisi hizo, alisema Tanzania ni nchi yenye watu wenye historia thabiti barani Afrika kutokana na kushiriki kikamilifu kuzikomboa nchi nyingi barani Afrika.

"Tanzania si tu imetoa mchango mkubwa katika historia ya Ukombozi wa Afrika bali imegharamika mno kuanzia watu wetu, fedha zetu na hata kuiweka nchi yetu katika hatari ya kushambuliwa.

“Viongozi wetu walifanya uthubutu mkubwa na sisi leo sio watu poa, tuko imara kuilinda nchi yetu na sisi tuliopewa dhamana ya mradi huu lazima tutimize wajibu wetu ili kuitunza historia hii na kuwajengea vijana wa sasa uzalendo na utamaduni wa kuwa watu wa kuthubutu kwa ajili ya nchi yao na Afrika," alisema Dk. Abbas.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbas

Alisema kutokana na umuhuimu wa ofisi hizo ambazo Umoja wa Afrika (AU) uliamua makao makuu yake yawe Dar es Salaam na serikali imeuweka chini ya usimamizi wa Idara ya Utamaduni katika wizara ya Habari sasa unahamishwa kutoka Idara ya Utamaduni na kuwa moja kwa moja chini ya Ofisi yake.

"Tunataka kwenda kasi na kwa viwango, wazee wetu walithubutu kufanya mambo makubwa kutufikisha hapa tulipo, sasa naona mnafanya kazi kubwa lakini mradi huu bado unachangamoto nyingi ambazo Idara ya Utamaduni pekee haiwezi kuzipeleka kwa kasi, watabaki washauri wa kitaalamu tu kwangu na kwa mradi huu, lakini kuanzia leo 7, Disemba, 2020, mratibu wa mradi huu atawajibika na kuripoti moja kwa moja kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari," aliagiza Dk. Abbas.

MAFUNZO YA MFUMO WA KUHIFADHI DATA ZA WAJUMBE WA BODI ZA TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA KATIKA PICHA

 MATUKIO KATIKA PICHA MAFUNZO YA KUHIFAHI DATA YALIYOANDALIWA NA HAZINA



Mkurugenzi wa Huduma za Kimenejimenti katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Neema Musomba akitoa muhtasari wa mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyozinduliwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbaro, jana  katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)


Mwezeshaji katika mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma, Felix Ngoi akitoa mada wakati wa uzinduzi wa hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuzinduliwa jana katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina).



Mwezeshaji katika mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma, Ntimi Malambugi akitoa mada wakati wa uzinduzi wa hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuzinduliwa jana katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina).


Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Profesa Raphael Chibunda (kulia), akiwaongoza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbaro (kushoto) na Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka kuelekea kwenye wa uzinduzi wa mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyoanza jana katika Kampasi Kuu ya SUA, Morogoro. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina).


Washiriki wa mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma wakifuatilia mafunzo hayo yaliyozinduliwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbaro jana katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina).


Monday, December 7, 2020

KATIBU MKUU HAZINA ASEMA MFUMO WA KUHIFADHI DATA ZA BODI UTAONDOA CHANGAMOTO YA UTEUZI

 


Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Pili Mazowea akimkaribisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbaro wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyoanza jana katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Katikati yao ni Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. (Pichana Ofisi ya Msajili wa Hazina)

NA MWANDISHI WETU - MOROGORO

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais,  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro amesema kuanzishwa kwa mfumo wa kuhifadhi taarifa za wajumbe wa bodi za taasisi na mashirika ya umma, kutasaidia kuondoa changamoto ya ucheleweshaji wa uteuzi wa bodi mpya.

Kwa mujibu wake, serikali ilitoa maelekezo kwa makatibu wakuu na watendaji wakuu wa taasisi za umma kuwasilisha katika mamlaka za uteuzi taarifa za bodi ya taasisi kukaribia kumaliza muda wake miezi sita kabla.

“Maelekezo hayo yalikuwa na lengo la kuhakikisha ndani ya kipindi cha miezi sita, mchakato wa uteuzi wa Bodi uwe umekamilika. Utekelezaji wa maelekezo hayo umekuwa ukisuasua na matokeo yake bado kuna taasisi hazipati Bodi zaWakurugenzi kwa wakati.

Naamini kwa mfumo huu unaozinduliwa leo(jana) utaisadia Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na mamlaka za uteuzi kufanyia kazi changamoto hiyo na kuhakikisha Bodi zinateuliwa kwa wakati,” alisema Dk. Ndumbaro.

Katibu Mkuu Utumishi aliyasema hayo wakati akizindua mafunzo ya matumizi ya mfumo mpya wa usimamizi wa taarifa za wajumbe wa bodi katika wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma yanayofanyika mjini hapa, na kuandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Hivyo basi, mfumo huu utakuwa kitendeakazi muhimu cha ofisi yako na naamini hata makatibu wakuu wa wizara wataweza kutumia mfumo huu kupata taarifa za hali ya Bodi zilizo chini ya wizara zao, na kushauri mamlaka za uteuzi mapema iwezekanavyo na hivyo kuondoa changamoto zinazotokana na uchelewaji wa teuzi za Bodi,” aliongeza.

Alieleza kuwa anafahamu kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa na changamoto ya muda mrefu ya kuzikumbushia mamlaka za uteuzi kuhusu kumalizika kwa muda wa Bodi za Wakurugenzi katika taasisi za umma na mara nyingi amekuwa akipata na kalaza barua hizo.

“Aidha,  taasisi nyingi za umma zimekuwa zikikaa muda mrefu bila ya kuwa na Bodi zaWakurugenzi. Kutokuwepo kwa Bodi ya Wakurugenzi katika Taasisi husababisha maamuzi mengi katika taasisi hiyo kukwama na kupelekea uchelewashaji wa mambo mengi ya msingi kutofanyika kwa wakati.

“Athari za kutokuwepo na Bodi ya wakurugenzi ni pamoja na kutopitishwa kwa hesabu zilizokaguliwa, watendaji kuendelea kukaimu nafasi zao kwa muda mrefu pamoja na kuchelewesha stahili mbalimbali za watumishi,” alisema.

Aliongeza, “Hatua za kuimarisha usimamizi wa Bodi za Wakurugenzi ni za kupongezwa na zinahitajika kuwa endelevu ili kufikia malengo ya kuwepo kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina. Nafahamu, ofisi yako haikuwa na mfumo ambao ungeiwezesha kufuatilia uteuzi wa Bodi kwa mamlaka za uteuzi pamoja na taarifa nyingine za utendaji wao.”

Alimpongeza Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka kwan iutekelezaji wa mfumo huu ni matokeo ya juhudi zinazofanywa na ofisi yake katika kuimarisha usimamizi wa utendaji wa Bodi na Menejimenti za wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha taasisi za Umma zinakuwa na Bodi za Wakurugenzi zilizo haina kupunguza watendaji wakuu wanaokaimu kwa muda mrefu.



Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbaro akijibu maswali ya washiriki wa mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuzinduliwa jana na Dkt Ndumbaro katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Kulia ni Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka na kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Kimenejimenti katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Neema Musomba. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)

Aidha, aliwashukuru wadau wa maendeleo wanaofadhili Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP) kwa kuwezesha kifedha ujengaji wa mfumo huo na kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na serikali katika kuimarisha maendeleo ya nchi.

“Aidha, nawapongeza kwa dhati vijana wetu, Watanzania wenzetu, ndani ya serikali kwa weledi wao na jitihada zao zilizosababisha kufanikisha kujengwa kwa mfumo huu,” alisema Dk Ndumbaro na kuongeza kuwa amefurahi kwasababu mfumo huo utasaidia kuhakikisha bodi pamoja na watendaji wakuu wanateuliwa kwa wakati.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alisema ofisi yake kwa kutumia wataalamu wa ndani ikishirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango katika mwaka wa fedha 2019/20 pamoja na washirika wa maendeleo ilianzisha Mradi wa Kusimika Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za wajumbe wa Bodi za Taasisi za Umma.

Alisema mfumo huu utatumika katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, mamlaka za uteuzi wa Bodi za Wakurugenzi pamoja na wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma katika usimamiaji wa masuala yote yanayohusu bodi hizo.

Mbuttuka alieleza kuwa Mfumo wa Usimamizi wa Bodi za Wakurugenzi (BMIS) umejengwa na wataalamu wa ndani ili kuhifadhi taarifa za uteuzi wa wajumbe wa bodi, wasifu wao, idadi ya taasisi wanazohudumu, aina za ujumbe wao pamoja kurahisisha utolewaji wa taarifa za bodi kwa wakati.

Alifafanua kuwa mfumo utaisaidia Ofisi ya Msajili wa Hazina na mamlaka za uteuzi kupata taarifa mapema kuhusu bodi kumaliza muda wake, wajumbe wa bodi wanaohudumu katika bodi zaidi ya tatu. 

“Uwepo wa mfumo huu utasaidia kuimarisha usimamizi wa Bodi za Wakurugenzi katika taasisi za umma kwa kuhakikisha taasisi hizo zinakuwa na Bodi kwa wakati. Mfumo pia utasaidia upatikanaji wa taarifa za uhakika za wajumbe wa Bodi na kwa wakati, ushiriki wao katika vikao na pia itapunguza urasimu wa ufuatiliaji wa uteuzi wa Bodi pale Bodi inapomaliza muda wake. 

Inategemewa kuwa uwepo wa mfumo huu utasaidia sana kuondoa changamoto ya taasisi kutokuwa na Bodi kwa muda mrefu, baadhi ya wajumbe Bodi kuteuliwa katika Bodi zaidi ya tatu, watendaji wakuu kukaimu muda mrefu, usahihi wa taarifa za taasisi kuhusu hali ya Bodi na watendaji wakuu, kuongeza ufanisi wa utendaji wa Bodi na kuzifanya mamlaka za uteuzi kupata taarifa kwa wakati kuhusu hali za Bodi katika taasisi za umma,” alielezaMbuttuka.

Mafunzo hayo yana washiriki 708 kutoka katika taasisi na mashirika ya umma 236, na watajengewa uwezo wa kutumia mfumo huu.

Katibu Mkuu aliwaomba kila mshiriki kuzingatia mafunzo haya kwa umakini na kuhakikisha anauelewa vizuri.

 

Saturday, December 5, 2020

KUFA KWA MAGAZETI YA KAMPUNI YA NHL KWAIBUA UPYA MACHUNGU YA WANAOIDAI

 


NA MWANDISHI WETU

MATUMAINI ya waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na awali, Habari Corporation Ltd ya kulipwa pensheni zao baada ya kuondolewa kazini kinyuime cha utaratibu yamezidi kutoweka baada ya kutolewa tangazo na kusitishwa kwa uchapishaji wa magazeti yanayozalishwa na kampuni hiyo kwa sababu ya ukata.

Tangazo la kusitishwa kwa uchapishaji wa magazeti yaliyokuwa yakizalishwa na New Habari (2005) Ltd ya Mtanzania, Rai, Dimba na Bingwa lilitolewa jana katika mitandao ya kijamii ikimkariri Mhariri Mtendaji, Dennis Msacky kuwatangazi wafanyakazi wanaodaiwa kuidai kampuni mshahara wa zaidi ya miezi mitatu, uamuzi huo sambamba za kupunguza wafanyakazi.

Taarifa ya kusitishwa kwa uzalishaji wa magazeti hoyo ilisomeaka; “Kampuni ya New habari 2006 LTD inayozalisha magazeti ya Mtanzania, Rai, Bingwa, Dimba imetangaza kusitisha uzalishaji za magazeti yote kutokana na mwenendo mbaya wa kibiashara.

“Akizungumza na wafanyakazi wa kampuni hiyo, Mhariri Mtendaji, Dennis Msacky amesema uzalishaji wa magazeti hayo utasitishwa kuanzia jumatatu ijayo.”  

Muda mfupi baada ya kusambaa kwa taarifa hiyo, zaidi ya watu 150 waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni New Habari waliopunguzwa bila kulipwa pensheni zao ingawa walikuwa wakikatwa kila  mwezi, walianza kuelezea hisia za kuibuliwa upya kwa machungu ya kupoteza haki zao kwa kueleza kuwa hawana tena uhakika wa kuzipa.

Afisa Mtendaji Mkuu wa New Habari, Erasto Matasia alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani kuzungumzia suala hilo alisema yuko msibani na kwamba aliyeteuliwa na kampuni kuzungumzia usitishwaji huo na kupunguzwa wafanyakazi kwa niaba ya Hussein Bashe ni Msacky.

“Mimi sipo huko, niko msibani, nakushauri mtafute Dennis Msacky aliyeteuliwa na kampuni kulizungumzia jambo hilo kwa niaba ya Bashe,” alisema Matasia.

Jitihada za kumpata Msacky hazikuweza kuzaa matunda baada ya simu yake ya kiganjani kuwa anaizima kila alipopigiwa na kuita.

Kampuni ya New Habari na kabla ya hapo ikifahamika kwa jina la Habari Corporation inaandamwa na madeni makubwa ya miaka mingi ya waliokuwa wafanyakazi wake ambao walikuwa wakikatwa fedha kwa ajili ya pensheni zao lakini baadhi ya viongozi wa juu wa kampuni hiyo walikuwa wakizitia kibindoni.

Bashe, ambaye kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge alikuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa New Habari 2006 LTD, amepata kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akikiri kuchota fedha za kampuni hiyo na kuzitumia katika biashara zake binafsi na kwamba alikuwa na matarajio ya kuzirejesha baada ya kupata faida.

Tanzania PANORAMA Blog inaendelea na ufuatiliaji wa sakata hili