banner

Saturday, December 5, 2020

MKUTANO MAALUMU WA KAMATI KUU YA ACT WAZALENDO

 MKUTANO MAALUMU WA KAMATI KUU YA ACT WAZALENDO


Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo ikiendelea na kikao chake kinachofanyika leo katika Hotel ya ONOMO (Ramada) kujadili hali ya kisiasa nchini na hatma ya chama hicho kujiunga katika Serikali ya Unoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK)





POLISI DAR WAUA WATUHUMIWA WAWILI WA UJAMBAZI

 



NA MWANDISHI WETU

JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni limewaua watu wawili wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio ya wizi toka maungoni, kuvunja nyumba na maduka usiku na kuiba, unyang’anyi wa kutumia silaha na wizi wa pikipiki.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC), Kamishna Msaidizi, Ramadhani Kingai, imeeleza kuwa watuhumiwa hao wa uhalifu waliuawa wiki iliyopita katika eneo la Mbezi Luis wakati wakipambana kwa risasi na polisi wa kikosi maalumu cha kupambna na majambazi cha Mkoa wa Kinondoni.

Katika taarifa yake hiyo, RPC Kingai alieleza kuwa X.F. 407. CLP Bundala Said Kimenya na X.F. 1205 CLP  Muhidin Sadick Mhina, ambao ni askari waliofukuzwa jeshini kutokana na matendo yao kihalifu waliuawa baada ya kukurupushwa na polisi wakijiandaa kufanya tukio la kihalifu.

“Mnamo tarehe 26/11/2020 majira  ya saa 12 jioni  huko maeneo ya Kimara Luguruni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni lilikuwa na taarifa fiche kuwa kuna majambazi wamepanga kufanya uhalifu kwa kutumia silaha katika eneo la Kiluvya.

“Kikosi maalumu cha kupambana na majambazi Mkoa wa Kinondoni kiliweka mtego eneo la Luguruni eneo la Sheli iitwayo hapa kazi tu karibu na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, ambapo majambazi hayo yalikuwa yakitokea Kimara kulekea Kiluvya kupitia Morogoro Road.

“Walipofika eneo hilo wakiwa gari T 889 DKG, Toyota Brevis, rangi ya  Silver walisimamishwa na askari polisi lakini hawakusimama, waligeuza gari yao kwa kasi kurudi walikotoka, ndipo askari walipoanza kuwakimbiza majambazi hao ambao wakaanza kufyatua risasi hovyo.

“Walipofika eneo la Mbezi Luis karibu na Shule ya St Anne Pr & Sec School, askari walifanikiwa kupiga tairi risasi ambapo gari lilipoteza mwelekeo na kuingia mtarano, jambazi mmoja aliuawa pale pale na watatu walikimbia huku mmoja akiwa amejeruhiwa mguu,’ inasomeka sehemu ya taarifa ya RPC Kingai.

Aidha, inaendelea kuwa baadaye polisi wakiwa katika ufuatiliaji walijulishwa kuwepo kwa jambazi eneo la standi ya Kibo aliyekuwa akitaka kupanda gari huku akiwa amejeruhiwa mguu ambapo askari walifika haraka kumtia mbaroni akiwa na silaha.

Tatarifa inaeleza zaidi kuwa Mhina na Kimenya ni askari waliofukuzwa kazi kabla ya kuuawa kutokana na matendo yao ya kihalifu na kwamba watuhumiwa wengine wawili wanaendelea kutafutwa.

Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Mloganzila.

 

 

WACHONGA VINYAGO KUPEWA ENEO UWANJA WA MKAPA

 



NA MWANDISHI WETU

SERIKALI itawapatia eneo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa wasanii wa sanaa za uchongaji vinyago, uchoraji na sanaa nyingine za ubunifu ili wapate nafasi kubwa ya kuonyesha kazi zinazoakisi utamaduni wa Mtanzania.

Hayo yameelezwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbas katika mkutano wake na wadau wa sanaa za ufundi jijini Dar es Salaam.

Dk. Abbas alisema serikali kupatikana kwa eneo hilo kuwatoa nafasi kwa Wasanii hao kuuza kazi zao kwa wingi kwa watanzania na raia wa kigeni kila kunapotea michezo inayozishirikisha timu ndani na nje.

Alisema serikali pia itasimamia kivitendo hoja ya wasanii hao ya kutaka watanzania wengi watumie kwa wingi sanaa za uchongaji, uchoraji na nyinginezo za wasanii wa Tanzania.  

Katika hatua nyingine, Dk.Abbas alitembelea kituo cha ubinifu sanaa za muziki, Tanzania House of Talents (THT) alisema serikali haitakiacha kamwe bali itashiriki kwa karibu kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwake yanaendelezwa.

Akizungumza na wasanii wa THT katika kituo hicho kilichoasisiwa na marehemu Ruge Mutahaba alisema wizara yake itakiunganisha kituo hicho na Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo

DC MURO ATAKA MAJI YA BILIONI 9 YAWE TAYARI NDANI YA SIKU 30

 



NA MWANDISHI MAALUM – ARUMERU

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru (DC) Jerry Muro amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji  katika Halmashauri ya Arusha kuukamilisha ndani ya siku 30 ili kutotoka nje ya mkataba.

Akizungumza katika eneo linapojengwa tanki kubwa la kuhifadhi maji alikofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wake, DC Murro alisema ameridhishwa na maendeleo yake lakini mkandarasi anapaswa kuhakikisha anaumaliza ndani ya siku 30 zilizosalia kama inavyoelekezwa kwenye mkataba.

Amesema amefanya ziara hiyo baada ya kutokea changamoto ya kupasuka kwa mabomba kila maji yanapofunguliwa kutoka kwenye tanki kubwa lililopo juu, changamoto ambayo imepatiwa ufumbuzi katika ziara hiyo.



“Mradi huu una thamani ya zaidi ya shulingi bilioni tisa na tangu umeanza kutekelezwa sasa tumebakiza siku 30 kwa ajili ya mradi huu kukamilika lakini nimeona unaenda vizuri ndiyo maana nikasema tutembee ili tuone wapi kuna changamoto ili tuweze kuzitatua kabla ya siku 30 hizi hazijafika tukabidhi mradi.

“Mpaka sasa nataka niwahakikishie zaidi ya asilimia 50 ya maji yameishaingia kwenye mzunguko lakini changamoto kubwa hapa ilikuwa kupasuka kwa mabomba. Ukifungua maji kutoka juu yakishuka mabomba yanapasuka, sasa nikaona hapana lazima nije mwenyewe nijue kwanini yanapasuka. Leo, tumalize ule mzizi wa fitina tujue kwa nini mabomba yanapasuka.

“Sasa tuna habari njema, moja kati ya sababu zilizokuwa zinasababisha mabomba kupasuka ni presha ya maji kutoka juu pale mlimani kwenye tanki kubwa kwa sababu maji yanashuika kwa kasi kwa sababu yakishuka kwa kasi yakikuta wewe hujafungua maji yanajaa yanapasua mabomba, lakini changamoto hii leo tumeimaliza na hamtaiona tena katika maisha yenu. Sasa tunaendelea kuongeza mlazo wa mabomba,”alisoma DC Murro.

Mradi huu mkubwa utahudumia vijiji vitano vilivyo katika Kata ya Ngaramtoni, Lemanyata  na Oludonywasi vyenye wakazi zaidi ya 50,000 watanufaika na unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Water Aid.

Katika ziara hiyo, DC Murro aliambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha, Mbunge wa Arumeru  magharibi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha, wawakilishi la Shirika la Water Aid na watendaji  wengine  wa serikali na  mamlaka za maji.

Friday, December 4, 2020

TANAPA YANYAKUA TUZO YA DHAHABU KIMATAIFA

 

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi- Mawasiliano, Pascal Shelutete

NA MWANDISHI MAALUM – ARUSHA

MAMLAKA ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), imeshinda tuzo ya dhahabu ya kimataifa ya utoaji huduma bora kwa mwaka 2020 inayotolewa na Taasisi ya European Society for Quality Research (ESQR).

Taarifa ya ushindi huo imetolewa leo na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi – Mawasiliano, Pascal Shelutete ambaye ameeleza kuwa tuzo hiyo itakabidhiwa kwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jesta Nyamanga, wiki ijayo, jijini Brussels.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kamishna Shelutete ameeleza kuwa TANAPA imeibuka mshindi miongoni mwa washindani 51 kutoka nchi 39 duniani.

“Tuzo za ESQR za huduma bora hutolewa kila mwaka na Shirika la ESQR kwa kutambua taasisi za serikali na zisizokuwa za kiserikali pamoja na watu binafsi wanaotoa huduma za viwango ya juu. Washindi wa tuzo hii huchaguliwa kwa kuzingatia matokeo ya kura zilizopigwa na taasisi zilizoshinda tuzo hizo awali, maoni ya wateja na utafiti wa masoko.

“Mchakato wa upatikanaji wa washindi wa tuzo hii unajumuisha utafiti wa taarifa mbalimbali kwa umma, machapisho, maoni chanya ya wateja, miradi ya kijamii na vyuo vikuu pamoja na maonyesho,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Kamishna Shelutete.

Anaandika zaidi kuwa tuzo hiyo ni matokeo ya mikakati madhubuti ya TANAPA katika kuhifadhi rasilimali za hifadhi pamoja na mrejesho chanya kutoka kwa wateja wa kitaifa na kimataifa.

“Utambuzi huu utakuwa chachu ya kuendelea kuongeza jitihada za uhifadhi endelevu wa hifadhi zetu na kutangaza vivutio katika masoko mbalimbali na kuendelea kuboresha huduma za utalii,” inasomeka.

Taarifa hiyo inahitimishwa na wito kwa umma, taasisi za kitaifa na kimataifa na wadau wa maendeleo kuendelea kutoa ushirikiano kaktika kuhifadhi rasilimali za hifadhi ya taifa na kuunga mkono juhudi za kukuza utalii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.