banner

Saturday, December 5, 2020

WACHONGA VINYAGO KUPEWA ENEO UWANJA WA MKAPA

 



NA MWANDISHI WETU

SERIKALI itawapatia eneo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa wasanii wa sanaa za uchongaji vinyago, uchoraji na sanaa nyingine za ubunifu ili wapate nafasi kubwa ya kuonyesha kazi zinazoakisi utamaduni wa Mtanzania.

Hayo yameelezwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbas katika mkutano wake na wadau wa sanaa za ufundi jijini Dar es Salaam.

Dk. Abbas alisema serikali kupatikana kwa eneo hilo kuwatoa nafasi kwa Wasanii hao kuuza kazi zao kwa wingi kwa watanzania na raia wa kigeni kila kunapotea michezo inayozishirikisha timu ndani na nje.

Alisema serikali pia itasimamia kivitendo hoja ya wasanii hao ya kutaka watanzania wengi watumie kwa wingi sanaa za uchongaji, uchoraji na nyinginezo za wasanii wa Tanzania.  

Katika hatua nyingine, Dk.Abbas alitembelea kituo cha ubinifu sanaa za muziki, Tanzania House of Talents (THT) alisema serikali haitakiacha kamwe bali itashiriki kwa karibu kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwake yanaendelezwa.

Akizungumza na wasanii wa THT katika kituo hicho kilichoasisiwa na marehemu Ruge Mutahaba alisema wizara yake itakiunganisha kituo hicho na Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo

DC MURO ATAKA MAJI YA BILIONI 9 YAWE TAYARI NDANI YA SIKU 30

 



NA MWANDISHI MAALUM – ARUMERU

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru (DC) Jerry Muro amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji  katika Halmashauri ya Arusha kuukamilisha ndani ya siku 30 ili kutotoka nje ya mkataba.

Akizungumza katika eneo linapojengwa tanki kubwa la kuhifadhi maji alikofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wake, DC Murro alisema ameridhishwa na maendeleo yake lakini mkandarasi anapaswa kuhakikisha anaumaliza ndani ya siku 30 zilizosalia kama inavyoelekezwa kwenye mkataba.

Amesema amefanya ziara hiyo baada ya kutokea changamoto ya kupasuka kwa mabomba kila maji yanapofunguliwa kutoka kwenye tanki kubwa lililopo juu, changamoto ambayo imepatiwa ufumbuzi katika ziara hiyo.



“Mradi huu una thamani ya zaidi ya shulingi bilioni tisa na tangu umeanza kutekelezwa sasa tumebakiza siku 30 kwa ajili ya mradi huu kukamilika lakini nimeona unaenda vizuri ndiyo maana nikasema tutembee ili tuone wapi kuna changamoto ili tuweze kuzitatua kabla ya siku 30 hizi hazijafika tukabidhi mradi.

“Mpaka sasa nataka niwahakikishie zaidi ya asilimia 50 ya maji yameishaingia kwenye mzunguko lakini changamoto kubwa hapa ilikuwa kupasuka kwa mabomba. Ukifungua maji kutoka juu yakishuka mabomba yanapasuka, sasa nikaona hapana lazima nije mwenyewe nijue kwanini yanapasuka. Leo, tumalize ule mzizi wa fitina tujue kwa nini mabomba yanapasuka.

“Sasa tuna habari njema, moja kati ya sababu zilizokuwa zinasababisha mabomba kupasuka ni presha ya maji kutoka juu pale mlimani kwenye tanki kubwa kwa sababu maji yanashuika kwa kasi kwa sababu yakishuka kwa kasi yakikuta wewe hujafungua maji yanajaa yanapasua mabomba, lakini changamoto hii leo tumeimaliza na hamtaiona tena katika maisha yenu. Sasa tunaendelea kuongeza mlazo wa mabomba,”alisoma DC Murro.

Mradi huu mkubwa utahudumia vijiji vitano vilivyo katika Kata ya Ngaramtoni, Lemanyata  na Oludonywasi vyenye wakazi zaidi ya 50,000 watanufaika na unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Water Aid.

Katika ziara hiyo, DC Murro aliambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha, Mbunge wa Arumeru  magharibi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha, wawakilishi la Shirika la Water Aid na watendaji  wengine  wa serikali na  mamlaka za maji.

Friday, December 4, 2020

TANAPA YANYAKUA TUZO YA DHAHABU KIMATAIFA

 

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi- Mawasiliano, Pascal Shelutete

NA MWANDISHI MAALUM – ARUSHA

MAMLAKA ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), imeshinda tuzo ya dhahabu ya kimataifa ya utoaji huduma bora kwa mwaka 2020 inayotolewa na Taasisi ya European Society for Quality Research (ESQR).

Taarifa ya ushindi huo imetolewa leo na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi – Mawasiliano, Pascal Shelutete ambaye ameeleza kuwa tuzo hiyo itakabidhiwa kwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jesta Nyamanga, wiki ijayo, jijini Brussels.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kamishna Shelutete ameeleza kuwa TANAPA imeibuka mshindi miongoni mwa washindani 51 kutoka nchi 39 duniani.

“Tuzo za ESQR za huduma bora hutolewa kila mwaka na Shirika la ESQR kwa kutambua taasisi za serikali na zisizokuwa za kiserikali pamoja na watu binafsi wanaotoa huduma za viwango ya juu. Washindi wa tuzo hii huchaguliwa kwa kuzingatia matokeo ya kura zilizopigwa na taasisi zilizoshinda tuzo hizo awali, maoni ya wateja na utafiti wa masoko.

“Mchakato wa upatikanaji wa washindi wa tuzo hii unajumuisha utafiti wa taarifa mbalimbali kwa umma, machapisho, maoni chanya ya wateja, miradi ya kijamii na vyuo vikuu pamoja na maonyesho,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Kamishna Shelutete.

Anaandika zaidi kuwa tuzo hiyo ni matokeo ya mikakati madhubuti ya TANAPA katika kuhifadhi rasilimali za hifadhi pamoja na mrejesho chanya kutoka kwa wateja wa kitaifa na kimataifa.

“Utambuzi huu utakuwa chachu ya kuendelea kuongeza jitihada za uhifadhi endelevu wa hifadhi zetu na kutangaza vivutio katika masoko mbalimbali na kuendelea kuboresha huduma za utalii,” inasomeka.

Taarifa hiyo inahitimishwa na wito kwa umma, taasisi za kitaifa na kimataifa na wadau wa maendeleo kuendelea kutoa ushirikiano kaktika kuhifadhi rasilimali za hifadhi ya taifa na kuunga mkono juhudi za kukuza utalii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.   

WATUHUMIWA WA DAWA ZA KULEVYA WAFANYA MITIHANI YA KIDATO CHA NNE

 



NA MWANDISHI WETU

JESHI la Polisi limewaruhusu wanafunzi saba wanaosoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya St Mary’s, waliokamatwa wakivuta dawa za kulevya aina Bangi kufanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne.

Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni (RPC), Kamishna Msaidizi Ramadhani Kingai amesema, polisi imewaruhusu wanafunzi hao kufanya mitihani ya kumaliza elimu ya sekondari kwa sababu za kiutu na watakapomaliza hatua za kisheria dhidi ya tuhuma zao zitachukuliwa.

RPC Kingai amesema atatoa taarifa ya hatua zitakazochukuliwa na polisi Jumatatu, Oktoba 7, 2020a ambapo watakuwa wamekamilisha uchunguzi ukiwemo wa kutoweka kwa mwanafunzi aliyekuwa akisoma kidato cha tatu katika shule, Labna Salim Said.  

Vijana hao saba ambao majina yao hayajatajwa walikamatwa wakivuta na wakiwa na misokoto mingi ya bangi ndani ya nyumbani ya Kamishna Msataafu wa Jeshi la Magereza wakati wa msako wa Labna na baada ya kupekuliwa kwa nyumba hiyo ilingulika kuwa na shamba la bangi ndani ya ua unaoizunguka.

RPC Kingai alikataa kulitaja jina la Kamishna huyo na mahali ilipo nyumba yake ambamo walikutwa vijana hao wakiwa na misokoto ya bangi pamoja na shamba la bangi.

Katika hatua nyingine, RPC Kingai alisema hadi sasa polisi haijafanikiwa kumpata mwanafunzi Labna lakini juhudi za kumtafuta zinaendelea.

 Mwanafunzi msichana Labna wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 na kutokomea kusikojulikana na hadi sasa hajapatikana lakini katika hatua ya kushangaza Labna ambaye alitoweka akiwa chini ya uangalizi wa shule, taarifa za kutoweka kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa Labna akiulizia kama ameishafika nyumbani.

Uongozi wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s haukutoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mwanafunzi huyo na badala yake wazazi ndiyo walioripoti tukio la mtoto wao kupotea akiwa shuleni.

Thursday, December 3, 2020

MBOWE AWEZA KUFUNGWA HADI MIAKA MIWILI

 




NA MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe anaweza kufungwa gerezani kifungo cha mpaka miaka miwili iwapo Mkurugenzi wa Mashtaka, Biswalo Mganga ataondoa huruma yake dhidi ya kosa alilolifanya yeye na wenzake la kudharua kwa makusudi nembo ya Taifa.

Hilo limebainika katika uchunguzi wa Tanzania PANORAMA Blog kuhusu makosa yanayoangukia kwenye kifungu namba saba (7) cha sheria ya Nembo ya Taifa ambayo Mbowe na wenzake waliyafanya wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Chadema wa kumchagua mgombea urais na makamu wake Mwaka 2020, katika ukumbi wa Mlimani City, siku chache kabla ya kuanza kwa kampeni zilizodumu kwa siku 60.

Kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kuwa katika mkutano huo uliohudhuliwa pia na Tundu Lissu ambaye kitaaluma ni Mwanasheria anayezijua vema sheria za nchi, Lazaro Nyalandu, waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii ambaye pia anazifahamu vema sheria na Mbowe ambaye alikuwa Mbunge katika Bunge la 11 akishiriki kutunga sheria za nchi, aliliiongoza baraza hilo kuimba wimbo wa Taifa huku yeye na wenzake hao wakiongezea maneno ambayo hayapo kisheria kwenye wimbo wa taifa.

Kwa mujibu wa sheria, kitendo hicho cha Mbowe na wenzake ni uvunjifu wa sheria namba saba kwa kuufanyia dhihaka wimbo wa taifa hivyo alipaswa kukamatwa yeye na wenzake wote waliofanya dhihaka hiyo na kushtakiwa mahakamani.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga, mapema wiki hii ameeleza kuwa hakuamuru kukamatwa kwa Mbowe na wenzake kwa kutanguliwa na busara ya kutoleta sintofahamu katika taifa kipindi cha uchaguzi mkuu.

DPP, Biswalo Mganga


Kauli hiyo ya DPP Mganga imepata nguvu kubwa kutokana ukweli uliopo kuwa wakati wote wa kampeni na kipindi cha uchaguzi mkuu, maadui wa taifa na hasa mataifa ya mabeberu walilenga kuibua hekaheka ambazo zingezaa machafuko na kuifanya nchi isitawalike, yakiwatumia wanasiasa watanzania vibaraka wanaoishi katika mataifa hayo.

Katika hatua ya kushangaza, Mbowe ambaye haina shaka anajua kuwa alitenda kosa na anapaswa kushtakiwa lakini bado yupo huru, ameanzisha chokochoko zinazoashiria kumshinikiza DPP Mganga kutokuwa na huruma na wale wote waliotenda kosa la kudharau kwa makusudi nembo ya Taifa.

Chokochoko hiyo ya Mbowe imedhihirika mwishoni mwa mwezi uliopita baada kuongoza kikao cha Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi kiimla kusikiliza na kuhukumu wabunge 19 wa viti maalumu wa chama hicho, kwa kutamka maneno yenye mwelekeo wa kutaka mmoja wa wabunge hao aliyekuwa akishtakiwa kwa kosa kama hilo hilo alilolifanya Mbowe la kudharau nembo ya taifa, arejeshwe gerezani baada ya DPP kumuachia kwa mamlaka aliyonayo kisheria.

Julai 4, 2020, Mbunge huyo akiwa katika Kijiji cha Puma, Wilaya ya Ikungi, Mkoa wa Singida alitenda kosa la kuimba wimbo wa taifa huku akiongeza maneno ambayo hayamo kisheria kwenye wimbo huo huku akipandisha bendera ya Chadema.