NA MWANDISHI WETU
HATIMAYE imebainikiwa kuwa uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwavua uanachama makada wake 19
wanawake, kinaowatuhumu kwa utovu wa nidhamu na kula kiapo cha kuwa wabunge wa
viti maalumu bila kupitishwa na chama ni mwendelezo wa matukio yake ya
'kisanii'
Hayo yameelezwa na wataalamu bingwa wa mambo ya kibunge,
Wataalamu wa Katiba, Wanasheria nguli wa Sheria za Uchaguzi na maafisa wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika mahojiano maalumu na Tanzania PANORAMA Blog
kuhusu hatua ya Kamati Kuu ya Chadema kuwavua ubunge makada wake hao na uhalali
wa uamuzi wa Spika kuwaapisha nje ya ukumbi wa Bunge.
Mmoja wa watalaamu waliobeba katika mambo ya mabunge ya
Jumuiya ya Madola ambaye ni mshauri na mkufunzi wa kanuni, utamaduni, utaratibu
na mienendo wa mabunge barani Afrika ameeleza kuwa uamuzi wa Kamati Kuu ya
Chadema ni mchezo wa kisiasa wenye lengo la kukirudisha chama hicho midomoni na
masikioni mwa watanzania wakati huu kinapoelekea kutoweka.
Alisema kisheria, kikanuni na utamaduni wa mabunge wa
Jumuiya ya Madola, wabunge 19 wanawake wa viti maalumu wa Chadema hawana kosa
lolote katika mchakato mzima uliowezesha kuapishwa kwao hivyo hawapaswi
kuhukumiwa kwa namna yoyote ile.
Alisewa mbali na wabunge hao, Spika wa Bunge, Job Ndugai
pia hana kosa kwa sababu hajakiuka sheria na kanuni za Bunge kuwaapisha wabunge
hao na wala hajatenda kinyume na tamaduni na taratibu za kibunge ambapo Bunge
la Tanzania linafuata mfumo wa kiuendeshaji wa mabunge ya Jumuiya ya Madola.
Alisema kabla ya kuapishwa kwa wabunge hao kulikuwa na
mawasiliano ambayo kisheria ni ya siri baina ya chama cha siasa husika na Tume
ya Taifa ya Uchaguzi yaliyohusu uwasilishaji na upokeaji wa orodha ya watu
wenye sifa za kuwa wabunge, orodha ambayo baada ya kupokelewa na NEC, ilifanyiwa
kazi kisha ikawasilishwa kwa Spika.
"Kwa mujibu wa sheria, katibu mkuu wa chama ndiyo
mwenye jukumu la kuwasilisha majina NEC na kwa maelezo ya NEC hilo lilifanyika.
Na mawasiliano kati ya chama cha siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu
chama kuwasilisha orodha ya majina ya watu wenye sifa kuwa wabunge wa viti
maalumu na tume kuyapokea na kuyafanyia kazi huwa siri.
"Yakishafanyiwa kazi na NEC ndiyo humjulisha Spika na
yeye huendelea na taratibu za kibunge.
"Wakati hayo yakitendeka baina ya Katibu Mkuu wa
Chadema na NEC, wabunge hawakupewa fursa ya kujua mawasiliano yaliyofanyika na
hawakupaswa kujua. Baada ya hilo walijulishwa na chama chao kuwa wameteuliwa
kuwa wabunge na walipaswa kuripoti bungeni.
"Spika yeye alipokea barua tu toka NEC kumjulisha juu
ya uteuzi huo na ndiyo utaratibu ulivyo, Spika hutaarifiwa na NEC. Sasa mpaka
hapo wabunge hao 19 na Spika hawawa kosa lolote.
"Labda kama NEC ingesema aliyeandika barua siyo katibu
mkuu na kwa hiyo orodha ya Chadema isingepokelewa lakini NEC imesema wazi
katika tamko lake kuwa orodha hiyo ilitoka Chadema.
"Kwa hiyo Chadema iweke wazi na ijibu kauli ya NEC
kuwa wao ndiyo waliandika barua na kuwasilisha orodha ya wabunge wa viti
maalumu bila kuwa na sharti la namna walivyopatikana kwa sababu siyo hitaji la
NEC kujua, badala ya kumshambulia Spika na kudhalilisha wabunge
waliokwishaapishwa" alisema mtaalamu huyo wa mambo ya kibunge ya Jumuiya
ya Madola.
Mbali na huyo, mwanasheria nguli wa sheria za uchaguzi na
masuala ya Katiba ambaye naye hakupenda kutajwa jina lake, yeye alisema wabunge
19 wa viti maalumu wa Chadema hawawezi kutengua kiapo chao na uamuzi wa Kamati
Kuu ya Chadema hauwazuii kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kibunge.
"Mambo ya hicho chama sipendi kuyaongelea kisheria kwa
sababu kila siku wanaibuka na jambo. Lakini nitakueleza kisheria ilivyo ila
sitaki kuandikwa jina mimi kwa sababu sihitaji kuingia kwenye malumbano ya
kisanii na hao watu. Naeleza kuwajuza watanzania.
"Kwa namna yoyote ile wabunge 19 wa viti maalumu wa
Chadema wataendelea na wajibu wao, sioni sababu ya kutengua kiapo chao.
"Kuapa nje ya Bunge ni sharti jipya la kikanuni kwa
wabunge waliochelewa kuapa kabla ya ufunguzi wa Bunge na Spika mwenyewe
amekwishalitolea ufafanuzi na lipo ndani ya kanuni za Bunge labda kama hao Chadema
hawasomi kanuni.
"Kwa msingi huo sharti hilo linapata nguvu ya ibara ya
89 ya Katiba kwa kutunga Kanuni za Bunge na ndiyo uwepo wa kanuni hiyo mpya.
"Lakini Pia anayetuhumu ndiyo mwenye jukumu la
kuthibitisha pasipo shaka kuwa barua ile siyo yao na siyo ya NEC. Chadema watoke
wakanushe kama barua iliyopo NEC siyo ya kwao.
"Upo ushahidi wa kutosha kuwa Katibu Mkuu wa Chadema,
John Mnyika aliwasilisha barua ya orodha ya wabunge wa viti maalumu kwa rejista
na mawasiliano ya simu na ofisi ya NEC baada ya kuomba ajulishwe rasmi kwa
barua sharti la kuwasilisha orodha ya majina ya wabunge wa viti maalumu,"
alisema ngwiji huyo wa Sheria za Uchaguzi na Mambo ya Katiba.
Alitoa mfano kuwa kinachofanya na Chadema ni sawa sawa na
mbunge aliyetambulishwa na chama chake kuwa mgombea, baada zoezi la uchaguzi
anapopewa hati ya kutangazwa kuwa mbunge na baadaye kwenda kula kiapo
anafukuzwa na chama chake.