banner

Thursday, December 3, 2020

DC MURO AIBUA FURAHA ILIYOPOTEA MIAKA 12 KWA WANANCHI WA KIJIJI CHA MANYIRE

 

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Murro


NA MWANDISHI MAALUMU- ARUMERU

FURAHA ilipotea ya wananchi wa Kijiji cha Manyire, Kata ya Mlangarini, Halmashauri ya Arusha waliokuwa wamenyang'anywa ardhi yao na mtu aliyefahamika kwa jina moja la William, mapema wiki hii ilirejea upya baada ya Serikali ya Wilaya ya Arumeru kuwarejea ardhi hiyo.

Shangwe zilizoambatana na vigelegele vya akina mama ziliibuka katika eneo ulipokuwa ukifanyika mkutano wa kutatua mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa kijiji hicho na William, baada ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru (DC), Jerry Muro kutangaza kuwa ardhi iliyokuwa imetwaliwa na Wiliam kutoka kwa wananchi hao imerejeshwa rasmi kwao na serikali.

Katika mkutano huo uliofanyika mapema wiki hii kijiji hapo, William alitakiwa na DC Muro kuwasilisha nyaraka zake zote zilizokuwa zikimpa uhalali wa umiliki wa ardhi lakini baada kukaguliwa na wataalamu wa ardhi wa serikali ilibainika kuwa hakukuwa na nyraka yoyote kati ya alizowasilisha iliyokuwa ikimpa uhalali huo.

"Nimekuja hapa ili tumalize hili tatizo lililodumu kwa miaka mingi! Hii ni serikali makini na Rais John Pombe Magufuli ametutuma tuje tusikilize kero zenu wananchi.

" Nimekuja, nimekagua, nimezunguka eneo ambalo kuna mgogoro wa ardhi uliosababisha nyumba kuchomwa moto. Tumeangalia vielelezo na nyaraka zote za maeneo ambayo Mzee William anasema ni mali yake.

"Hakuna nyaraka hata moja imethibitisha maeneo hayo ni mali ya Mzee William. Jinsi alivyopata hana vielelezo na hana nyaraka yoyote inayosema maeneo hayo ni mali yake.

" Hivyo serikali imejiridhisha na tunatamka maeneo yale ambayo wananchi walinyang'anywa na Mzee William tumewarudishia," alisema DC Muro.

Kutolewa kwa kauli hiyo na DC Muro kuliibua shangwe kutoka kwa wananchi na baadhi yao waliishukuru serikali ya wilaya kwa kuumaliza mgogoro huo wa ardhi uliokuwa ukihatarisha hali ya amani katika Kijiji cha Manyire.

DC Muro alifika kijijini hapo mapema wiki hii akiwa amefuatana na baadhi ya wataalamu wa ardhi kukagua uharibifu uliotokea kwenye nyumba iliyochomwa moto kwa sababu ya mgogoro wa ardhi.

Akiwa kijijini hapo DC Muro alifanya kikao na wananchi pamoja na boma la Mzee William ambapo watalaamu wa ardhi  walipitia upya vielelezo vya umiliki wa ardhi vya kila upande na kubaini upungufu mkubwa katika nyaraka za William.

 

SERIKALI KUANDAA TAMASHA, TUZO KUBWA ZA SANAA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Hassan Abbas


NA MWANDISHI WETU

SERIKALI iko mbioni kuandaa tamasha kubwa la muziki na sanaa litakalofahamika kwa jina la moja ya vivutio vikubwa vya utalii vilivyopo hapa nchini.

Akizungumza wiki hii jijini Dar es Salaam na wadau wa sanaa na muziki, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbas amesema kwa kutambua urithi mkubwa wa sanaa uliopo nchini ukiwemo muziki, filamu, ngoma na uga mwingine, serikali kwa kushirikiana na wadau, itaratibu tamasha kubwa la aina yake litakalofanyika baadaye mwaka huu.

Dk. Abbas alisema sekta hiyo inapaswa kuhakikisha inaiburudisha jamii ya watanzania wachapakazi ipasavyo na kwamba sambamba na kuandaliwa kwa tamasha hilo, pia serikali kwa kushirikiana na wadau itarejesha tuzo za muziki na sekta nyingine zilizo chini ya wizara inayoiongoza..

"Moja ya kazi kubwa ya sekta ya sanaa nchini ni kuhakikisha jamii yetu inayochapa kazi sana kwa sasa inaburudika ipasavyo, sasa naona sanaa inakuja tu pale panapokuwepo mdhamini au mwandaaji fulani asipokuwepo hakuna matukio na nchi iko kimya.

"Serikali sasa inakwenda kuchechemsha sekta hii kwa kuratibu tamasha kubwa sana litakaloanzia Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kuendelea kuungana na Tamasha la Kimataifa la Sanaa Bagamoyo.


KAtibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Hassan Abbas akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa wizara yake


"Tusisubiri wadhamini, wakija sawa, kama wako likizo basi mimi nasema sisi wenyewe tunaweza kwa umoja wetu sasa tukutane Uwanja wa Uhuru Disemba 26 mwaka huu na kisha Desemba 27 twende Bagamoyo.

"Wasanii wakiungana watajaza uwanja. Twende tutateremsha wasanii wetu wote ambao ni urithi wa sasa na baadaye wa nchi hii halafu tuone kama watu hawatakuja," amesema Dk. Abbas.

Dk. Abbas yupo katika ziara ya kikazi ya kukutana na wadau mbalimbali wa sanaa na sekta nyingine zilizo chini ya wizara yake.

 

Tuesday, December 1, 2020

NGUVU YA BUNGE YAJARIBIWA NA CC YA CHADEMA

 


NA MWANDISHI WETU

 HATIMAYE imebainikiwa kuwa uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwavua uanachama makada wake 19 wanawake, kinaowatuhumu kwa utovu wa nidhamu na kula kiapo cha kuwa wabunge wa viti maalumu bila kupitishwa na chama ni mwendelezo wa matukio yake ya 'kisanii'

Hayo yameelezwa na wataalamu bingwa wa mambo ya kibunge, Wataalamu wa Katiba, Wanasheria nguli wa Sheria za Uchaguzi na maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika mahojiano maalumu na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu hatua ya Kamati Kuu ya Chadema kuwavua ubunge makada wake hao na uhalali wa uamuzi wa Spika kuwaapisha nje ya ukumbi wa Bunge.

Mmoja wa watalaamu waliobeba katika mambo ya mabunge ya Jumuiya ya Madola ambaye ni mshauri na mkufunzi wa kanuni, utamaduni, utaratibu na mienendo wa mabunge barani Afrika ameeleza kuwa uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema ni mchezo wa kisiasa wenye lengo la kukirudisha chama hicho midomoni na masikioni mwa watanzania wakati huu kinapoelekea kutoweka.

Alisema kisheria, kikanuni na utamaduni wa mabunge wa Jumuiya ya Madola, wabunge 19 wanawake wa viti maalumu wa Chadema hawana kosa lolote katika mchakato mzima uliowezesha kuapishwa kwao hivyo hawapaswi kuhukumiwa kwa namna yoyote ile.



Alisewa mbali na wabunge hao, Spika wa Bunge, Job Ndugai pia hana kosa kwa sababu hajakiuka sheria na kanuni za Bunge kuwaapisha wabunge hao na wala hajatenda kinyume na tamaduni na taratibu za kibunge ambapo Bunge la Tanzania linafuata mfumo wa kiuendeshaji wa mabunge ya Jumuiya ya Madola.

Alisema kabla ya kuapishwa kwa wabunge hao kulikuwa na mawasiliano ambayo kisheria ni ya siri baina ya chama cha siasa husika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi yaliyohusu uwasilishaji na upokeaji wa orodha ya watu wenye sifa za kuwa wabunge, orodha ambayo baada ya kupokelewa na NEC, ilifanyiwa kazi kisha ikawasilishwa kwa Spika.

"Kwa mujibu wa sheria, katibu mkuu wa chama ndiyo mwenye jukumu la kuwasilisha majina NEC na kwa maelezo ya NEC hilo lilifanyika. Na mawasiliano kati ya chama cha siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu chama kuwasilisha orodha ya majina ya watu wenye sifa kuwa wabunge wa viti maalumu na tume kuyapokea na kuyafanyia kazi huwa siri.

 


"Yakishafanyiwa kazi na NEC ndiyo humjulisha Spika na yeye huendelea na taratibu za kibunge.

"Wakati hayo yakitendeka baina ya Katibu Mkuu wa Chadema na NEC, wabunge hawakupewa fursa ya kujua mawasiliano yaliyofanyika na hawakupaswa kujua. Baada ya hilo walijulishwa na chama chao kuwa wameteuliwa kuwa wabunge na walipaswa kuripoti bungeni.

"Spika yeye alipokea barua tu toka NEC kumjulisha juu ya uteuzi huo na ndiyo utaratibu ulivyo, Spika hutaarifiwa na NEC. Sasa mpaka hapo wabunge hao 19 na Spika hawawa kosa lolote.

"Labda kama NEC ingesema aliyeandika barua siyo katibu mkuu na kwa hiyo orodha ya Chadema isingepokelewa lakini NEC imesema wazi katika tamko lake kuwa orodha hiyo ilitoka Chadema.

"Kwa hiyo Chadema iweke wazi na ijibu kauli ya NEC kuwa wao ndiyo waliandika barua na kuwasilisha orodha ya wabunge wa viti maalumu bila kuwa na sharti la namna walivyopatikana kwa sababu siyo hitaji la NEC kujua, badala ya kumshambulia Spika na kudhalilisha wabunge waliokwishaapishwa" alisema mtaalamu huyo wa mambo ya kibunge ya Jumuiya ya Madola.



Mbali na huyo, mwanasheria nguli wa sheria za uchaguzi na masuala ya Katiba ambaye naye hakupenda kutajwa jina lake, yeye alisema wabunge 19 wa viti maalumu wa Chadema hawawezi kutengua kiapo chao na uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema hauwazuii kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kibunge.

"Mambo ya hicho chama sipendi kuyaongelea kisheria kwa sababu kila siku wanaibuka na jambo. Lakini nitakueleza kisheria ilivyo ila sitaki kuandikwa jina mimi kwa sababu sihitaji kuingia kwenye malumbano ya kisanii na hao watu. Naeleza kuwajuza watanzania.

"Kwa namna yoyote ile wabunge 19 wa viti maalumu wa Chadema wataendelea na wajibu wao, sioni sababu ya kutengua kiapo chao.

"Kuapa nje ya Bunge ni sharti jipya la kikanuni kwa wabunge waliochelewa kuapa kabla ya ufunguzi wa Bunge na Spika mwenyewe amekwishalitolea ufafanuzi na lipo ndani ya kanuni za Bunge labda kama hao Chadema hawasomi kanuni.

"Kwa msingi huo sharti hilo linapata nguvu ya ibara ya 89 ya Katiba kwa kutunga Kanuni za Bunge na ndiyo uwepo wa kanuni hiyo mpya.

"Lakini Pia anayetuhumu ndiyo mwenye jukumu la kuthibitisha pasipo shaka kuwa barua ile siyo yao na siyo ya NEC. Chadema watoke wakanushe kama barua iliyopo NEC siyo ya kwao.

"Upo ushahidi wa kutosha kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliwasilisha barua ya orodha ya wabunge wa viti maalumu kwa rejista na mawasiliano ya simu na ofisi ya NEC baada ya kuomba ajulishwe rasmi kwa barua sharti la kuwasilisha orodha ya majina ya wabunge wa viti maalumu," alisema ngwiji huyo wa Sheria za Uchaguzi na Mambo ya Katiba.

Alitoa mfano kuwa kinachofanya na Chadema ni sawa sawa na mbunge aliyetambulishwa na chama chake kuwa mgombea, baada zoezi la uchaguzi anapopewa hati ya kutangazwa kuwa mbunge na baadaye kwenda kula kiapo anafukuzwa na chama chake.

TEMESA KUANZA KULIPA MADENI YA WAZABUNI

 


NA MWANDISHI WETU

WAKALA wa Ufundi na Umeme (TEMESA), itaanza kulipa sehemu ya madeni ya shilingi bilioni nne wanayodai wazabuni kutokana na fedha zilizolipwa na wizara na idara za serikali zilizotokana na agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wazabuni mbalimbali wanaidai TEMESA fedha za kusambaza vipuli na vilainishi pamoja na kutengeneza magari ya wizara na idara za serikali, madeni yanayofikia shilingi bilioni nne ya tangu 2012.

Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Dk. Stephen Massele alisema baada ya malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wazabuni,  sasa wataanza kulipa baada ya kukamilisha upitiaji wa madeni kwa kila mzabuni.

Dk. Massele alisema baadhi ya wazabuni ikiwemo kampuni ya Planet mawakili wao,  wamekwishapewa taarifa kwamba TEMESA inafanya mapitio ya madeni na itaanza kulipa  baada ya wiki moja.

Alisema fedha zitakazolipwa zimetokana na madeni wanayodai wizara na idara za serikali zilizopata huduma ya wazabuni hao na zitalipwa kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu mapema mwanzoni mwa mwaka huu.

Dk. Masele alisema madeni mengine ya wazabuni hao, yataendelea kulipwa kulingana na upatikanaji wa fedha kutoka kwa wadeni wao. TEMESA inazidai wizara na idara za serikali kiasi cha shilingi bilioni tano.

"Baadhi ya wazabuni tumewapa maelekezo kupitia mawakili wao,  wapo waliotuelewa kuwa tunakamilisha 'Reconciliation' ya fedha zilizolipwa kwa agizo la Waziri Mkuu nani ana fedha ya madeni yake na ndani ya wiki moja tutakamilisha malipo yake, " alisema Dk. Massele na kuongeza.

"Ambayo hayajalipwa hiyo watapewa taarifa na mameneja husika mengine yatasubiri kadiri tunavyolipwa. "

Kauli hiyo ya Dk. Masele imetolewa baada ya kuwepo malalamiko ya muda mrefu ya wazabuni kupitia viongozi wao wa Umoja wa Gereji Tanzania (UGETA).

Akizungumza na Tanzania PANORAMA, Mwenyekiti wa Umoja wa Gereji Tanzania (UGETA), Lumona Mkala, alisema wanachama wake wanaidai TEMESA MT Depot zaidi ya shilingi Bilioni nne za kusambaza vipuli na vilainishi vya mafuta ya magari.

Alitaja wazabuni wanaodai ni Beka investment shilingi  250,563,150, Moroturbo shilingi 80,256,197, Planet Busines link shilingi 175,312,570 na Ndeken shilingi 194,801,393

Wengine ni Kigustar Enterprisess,  Leonardo Automotive Garage, Nedea Enterprisess, RaaR Investment, Kigoma Garage, Adam Motor na Point A.

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWATUMIA SALAMU ZA ONYO WAHUJUMU USHIRIKA

 


NA MWANDISHI MAALUMU - OFISI YA WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa vyama vya ushirika wabadilike na wawe weledi ili warejesha heshima ya ushirika nchini.

Akizungumza jana katika ukumbi wa mikutano wa Hazina jijini Dodoma na wakuu wa mikoa sita, makatibu wakuu, Mrajisi wa Ushirika Taifa, warajisi wasaidizi wa mikoa,  Menejimenti ya Tume ya Ushirika,  wajumbe wa Bodi za NCU (1984) Ltd, KNCU (1984) Ltd, SHIRECU na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mkonge, Waziri Mkuu Majaliwa alisema viongozi wa vyama vya ushirika wanapaswa kubadilika kwa sababu wamepewa dhamana ya kuwasaidia Watanzania wanyonge.

"Viongozi wa ushirika ni lazima tubadilike. Nyie mliopewa dhamana kwenye vyama vikuu hivi vitatu vya KNCU, NYANZA na SHIRECU lazima mbadilike. Nyie mmepewa dhamana ya kuwasaidia Watanzania wenzetu wanyonge wanaolima ekari moja, mbili au tatu,” alisema.

Katika mkutano huo maalumu ambao Waziri Mkuu Majaliwa alipokea taarifa ya ufuatiliaji wa mwenendo wa vyama vya ushirika vya NCU (1984) Ltd, KNCU (1984) Ltd na SHIRECU (1984) Ltd kutoka kwa timu maalumu ya uchunguzi , alisema viongozi wa ushirika bado hawajabadilika kwa sababu hata kazi ya usambazaji mbolea kwa wakulima bado ni changamoto.

Uwasilishwaji wa taarifa hiyo ulishuhudiwa na Wakuu wa Mikoa ya Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Tanga, Geita na Simiyu. Pia Makatibu Wakuu wa Wizara za Fedha, Ardhi, Kilimo, Viwanda na Biashara.

Wengine walioshuhudia ni Mrajisi wa Ushirika Taifa, Warajisi Wasaidizi wa Mikoa, Menejimenti ya Tume ya Ushirika, Wajumbe wa Bodi za KNCU, NYANZA na SHIRECU na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania.

"Ninasema viongozi bado hatujabadilika kwa sababu hata suala la usambazaji wa mbegu kwa wakulima ni changamoto. Wengine wamekuja kujifunza ushirika hapa nchini na wamesonga mbele lakini sisi hatuendi mbali kwa sababu ya kukosa weledi, uaminifu na uwajibikaji katika majukumu tuliyowakabidhi.

"Nendeni mkasimamie ushirika ili heshima ya ushirika wa zamani irejee, hali ya ushirika ule ambao uliacha mali za ushirika. Bado kazi hizo mali haijakamilika. Tunataka tuzisimamie na tuwakabidhi kitu ambacho kimekamilika," alisema.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alisema anasikitika kuona makosa ya ushirika yanafanyika wakati warajisi wasaidizi wapo na hata kwenye halmashauri kuna maafisa ushirika.

“Haya madudu yanafanyika lakini warajisi wa mikoa mpo na nyie ndiyo wasimamizi wa ushirika. Je mnafanya nini?”

“Lazima uhakikishe vyama vya msingi vinasimamiwa na vinakwenda kama ambavyo sheria yetu ya ushirika inasema. Warajisi wasaidizi wapo kila mkoa na kila wilaya kuna afisa ushirika. Ni kwa nini mambo hayaendi?

"Hatutasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu anayehujumu mali za ushirika. Tulianza na tutaendelea kusimamia mali za ushirika," alisema.

Mapema, akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa, kiongozi wa timu hiyo maalumu, Asangye Bangu alisema imefanikiwa kurejesha mali 60 za ushirika zenye thamani ya sh. bilioni 68.98.

“Mali hizo zinajumuisha majengo, viwanja, magari na mitambo ya mashine, hazikuwa mikononi mwa vyama hivi vitatu lakini sasa zimerudishwa kwenye vyama," alisema Bangu.

Alisema kati ya hizo, NYANZA ilikuwa na mali 37 zenye thamani ya sh. bilioni 61.36, SHIRECU ilikuwa na mali saba zenye thamani ya sh. bilioni 3.33, KNCU ilikuwa na mali 10 zenye thamani ya sh. bilioni 2.03 na TCCCo ilikuwa na mali sita zenye thamani ya sh. bilioni 2.2.

Bangu alikabidhi taarifa hiyo ikiwa na mapendekezo kadhaa kwa serikali.