banner

Monday, December 21, 2020

WATANZANIA NA USINGIZI WA NJOZI TATU


NA MWANDISHI WETU

KWA mwaka wa pili sasa, Watanzania wanalala usingizi ulioambatana na jonzi tatu.

Njozi hizo ni, mosi; Wakala wa Barabara (TANROADS), pili; barabara ya juu iliyopo eneo la Tazara inayofahamika zaidi kwa jina la Mfugale Flyover, na tatu; Mhandisi Patrick Mfugale.

Walianza kuota njozi hizi usiku wa kuamkia Septemba 16, 2018 baada ya kuanza kutumika kwa barabara ya juu ya Mfugale iliyopo eneo la Tazara, Septemba 15, 2018.

Kabla ya hapo, Watanzania hasa waliokuwa wakitumia barabara ya Julius Nyerere na Nelson Mandela, walikuwa wanaota wamefukuzwa au kupewa barua ya karipio kali kwa kuchelewa kazini.



Wasafiri walikuwa wanaota wameachwa na ndege au treni na wafanyabiashara waliota hasara na kupoteza saa nyingi wakiwa katika foleni.

Ali Msafiri, mfanyabiashara na mkazi wa eneo la Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam ambaye alihudhuria uzinduzi wa Mfugale Flyover alinukuriwa na vyombo vya habari akieleza hivi:

"Kuzinduliwa kwa Mfugale Flyover kutaturahisishia usafiri wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na hata wasiokuwa wakazi wanaofika katika jiji hili kubwa la kibiashara nchini Tanzania.

"Wananchi tutakuwa tumepata fursa na foleni na msongamano utabaki ndoto sasa. Lile tatizo sugu na la miaka mingi la kwenda kazini sasa naona limeisha."

Watanzania wengi walikuwa wakilala hoi kutokana na shida ya usafiri iliyokuwa ikisababishwa na foleni. Wakazi wa Jiji la Dar  es Salaam wanaotumia barabara za Nyerere na Mandela kwenda kazini na kurudi nyumbani walilazimika kulala kuanzia saa tano usiku na kuamka saa 10 alfajili ili kuwahi kupambana na foleni.



Wasafiri wanaosafiri kwa ndege au treni ya Tazara nao walilazimika kutenga muda wa hadi saa tatu za kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam au pembezoni kwenda uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere au Stesheni ya Reli ya Tazara kwa sababu ya foleni na msongamano wa magari.

Wafanyabiashara na wasafirishaji wanaotumia barabara hizo walikuwa wakipoteza fedha na muda mwingi kukabiliana na foleni na shughuli za kiuchumi kwa taifa na raia mmoja mmoja zilikuwa zikikutana na changamoto kubwa kutokana na tatizo la foleni katika barabara hizo.

Daniel Masanja, Dreva la roli ambaye mara nyingi hutumia barabara ya Mandela kusafirisha mizigo inayotoka bandarini ambaye naye alihudhuria uzinduzi huo, yeye alikaririwa akisema hivi;



"Kulikuwa na shida kubwa sana. Tulikuwa tunapoteza fedha nyingi sana kwa kukaa saa nyingi barabarani, sasa tutasafirisha mizigo ya wateja na kuifikisha kwa wakati, hakika tutaongeza tija. Tutalala tukiota njonzi njema za barabara ya juu ya Mfugale."

Septemba 16, 2018, wanafunzi, wafanyakazi, wafanyabiashara, wasafirishaji na wasafiri walitumia barabara za Nyerere na Mandela kwa mara ya kwanza zikiwa hazina msongamano baada ya kuzinduliwa kwa Mfugale Flyover.



Mfugale Flyover ni barabara ya kwanza ya juu katika historia ya Tanzania inayounganisha sehemu kuu za Jiji la Dar es Salaam na maeneo makuu ya kiuchumi kama Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Bandari ya Dar es Salaam, machinjio ya Vingunguti na barabara zinazoelekea viwandani.

Ni barabara inayojumuisha njia kuu nne na daraja. Imetatua tatizo la msongamano na foleni na sasa imeongeza muda wa watu kufanya kazi badala ya kutumia muda mwingi wakiwa wamekwama barabarani kwenye foleni.

Kuanza kutumika kwa Mfugale Flyover kumewafanya Watanzania na wageni wanaotumia barabara za Nyerere na Mandela kulala usingizi mwororo huku wakiota ndoto ya kupita barabara ya juu ya Mfugale kuwahi katika shughuli zao za kiuchumi, masomo na usafiri.



Hii ndiyo ndoto ya kwanza ambayo Watanzania wanaota sasa kila walalapo usingizi.

Ndoto ya pili wanayoota sasa Watanzania ni TANROADS. Watanzaia wanaiota TANROADS kuwa taasisi yao iliyoshirikiana na kampuni kubwa ya ujenzi kutoka Japan ya Sumitomo Mitsui Construction Co. LTD kujenga barabara ya kwanza ya juu iliyopewa jina la Mhandisi Mfugale kwa mafanikio makubwa.



Wanaota maneno ya Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli aliyeitaka TANROADS kuitunza barabara hiyo na sasa ikiwa imepita miaka miwili tangu kuzinduliwa kwake, ipo katika mwonekano mzuri kutokana na uangalizi makini wa TANROADS.

Watanzania ambao sasa si taifa masikini tena wanaota mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo uliosainiwa Oktoba 15, 2015 kati ya Tanzania National Roads Agency (TANROADS) na Sumitomo Mitsui Construction Co.,Ltd. (SMCC), lengo likiwa kuboresha makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela. Lengo ambalo limefikiwa.



Awali wengi walikuwa wakiota kuwa ujenzi  wa barabara za aina hiyo hautawezekana Tanzania kwa sababu unagharimu matrilioni ya Dolla za Marekani ambayo Tanzania haina hivyo ili kuwa na barabara ya aina hiyo ni sharti kuomba mkopo kwa wazungu.

Sasa ndoto hizo hazipo, Watanzania wanaota shilingi bilioni 100 za kodi zao zinazokusanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kuwa zinaweza kujenga barabara ya juu ya kisasa kama zile zilizoko Chicago na California nchini Marekani na wakiamka wanapita kwenye barabara ya aina hiyo.



Ni ndoto iliyosubiriwa tangu Aprili 16, 2016, siku ambayo Rais Magufuli alizindua ujenzi wa barabara hiyo ya juu.

Ndoto ya tatu inamuhusu Injinia Patrick Mfugale ambaye mchango wake katika ujenzi wa daraja hilo utabaki kuwa kielelezo cha Mtanzania mzalendo aliyetumia vema elimu yake kulinufaisha taifa lake.



Watu walio karibu pamoja na wasaidizi wake wanaeleza kuwa Injinia Mfugale ni mkali kwa watu wanaomsifia yeye binafsi hata kama anastahili kusifiwa. Anapenda sifa zinazomstahili zielekezwe kwa serikali anayoitumikia, taifa na Watanzania.

Kwa sababu ya ukali wake huo, Watanzania wamebaki kuuota uzalendo, utaalamu na uadilifu wake ndotoni. Haina shaka sifa zake nyingi zitatolewa hadharani na bila kuogopa katazo lake atakapokuwa hayupo.

Lakini kwa sababu katazo lake hilo siyo sheria hivyo haliifungi Tanzania PANORAMA Blog kumtendea haki, linafuata nyayo za Rais Magufuli ambaye kwa kuutambua mchango wake katika ujenzi wa barabara hiyo na utumishi wake uliotukuka kwa taifa alimpa heshima ya juu kwa kuiita kwa jina lake.



Dunia sasa inapaswa kumtambua Mhandisi Patrick Mfugale kuwa mtaalamu wa kwanza wa fani ya uhandisi duniani aliyetumia utaalamu wake kujenga sehemu kubwa ya miundombinu ya barabara na madaraja ya taifa lake.

Kumbukumbu za kazi za kihandisi zilizoonwa na Tanzania PANORAMA Blog mpaka sasa zinaonyesha kuwa rekodi ya Mhandisi Mfugale ya kusaidia kujenga madaraja 1400 katika nchi ya baba na mama zake haijafikiwa na mhandisi mwingine yeyote duniani.



Rekodi zinamtaja pia Mhandisi Mfugale kuwa mtaalamu wa kwanza wa fani ya uhandisi duniani ambaye baada kupata elimu ya juu ya uhandisi nje ya nchi hakulikimbia taifa lake kwenda kufanya kazi ughaibuni ambako wahandisi hulipwa mishahara minono, bali alirejea kulijenga na mpaka sasa amebuni na kusimamia barabara za Taifa la Tanzania zenye urefu wa zaidi ya kilomita 36,258.

Kwa mujibu wa rekodi za kihandisi zilizoonwa na Tanzania PANORAMA Blog, Mhandisi Mfugale ndiye pekee duniani mpaka sasa aliyetoa mchango mkubwa kwa nchi yake katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Watanzania wanaoota taswira ya Patrick Mfugale kila wanapopita juu ya Mfugale Flyover wanapaswa kukumbuka maneno yake mbele ya Rais Magufuli siku ya ufunguzi wa barabara hiyo ili yawajengee uzalendo, unyenyekevu katika utumishi na uwajibikaji, aliposema;



"Ukiwa waziri wa ujenzi ulinituma Japan kwenda kuweka sahihi mkataba wa kazi hiyo, lakini tulikuwa hatujapata mkandarasi na ulinielekeza kuwa nisirudi huku mpaka niwe nimesaini mkataba.

"Na nilipoiambia Japan nimeambiwa na nchi yangu nisirudi, wakasema viza yako imeisha, kwa hiyo ni lazima urudi, nikasema ninaweza nikakaa hata railway stesheni, ili mradi kama mkimbizi lakini tenda hii tutafute namna ya kufanya daraja hili lijengwe,"

Mtu huyu Mhandisi Patrick Mfugale alizaliwa mkoani Iringa na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi ya Consolata ya mjini Iringa na 1975 alihitimu elimu yake ya shule ya upili katika shule ya upili mkoani Moshi.



Mwaka 1977, Mfugale aliajiriwa Wizara ya Ujenzi kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Rocky nchini India ambako alihitimu mwaka 1983  na kutunukiwa shahada yake ya kwanza ya uhandisi kisha akarejea nchini kuja kulijenga taifa lake

Mwaka 1991 Mhandisi Mfugale alisajiliwa kama mhandisi mtaalamu na mwaka 1992 aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa barabara za mikoa.

Mwaka 1994 hadi 1995 alikwenda ughaibuni kusoma katika Chuo Kikuu cha  Loughborough, Braunshweig nchini Uingereza ambako alihitimu ya kutunukiwa shahada yake ya pili ya uhandisi na kisha akarejea tena nchini kuendelea kulijenga taifa lake.

Mwaka 1995  aliteuliwa kuwa mhandisi mkuu wa madaraja nchini Tanzania na wakati huo huo akiwa masomoni nchini Uingereza alitafiti na kutengeneza mfumo wa madaraja nchini Tanzania.



Mhandisi Mfugale alibuni Daraja la Magarasi lenye mita 178 lililogharimu shilingi za Tanzania milioni 300 na pia, kwa uchache amejenga
Daraja la Mkapa Rufiji, Daraja la Umoja linalounganisha Tanzania na Msumbuji, Daraja la Rusumo, Daraja la Kikwete na  Daraja la Nyerere huko Kigamboni


Wednesday, December 16, 2020

UBUNGO INTERCHANGE PICHA HALISI YA WATANZANIA


 

 NA MWANDISHI WETU

BARABARA za juu zilizopo eneo la Ubungo zinazofahamika zaidi kwa jina la Ubungo Interchange ni picha halisi ya uchapakazi, uwezo wa kiuchumi na utaalamu wa Watanzania.

Kila mtumiaji wa barabara hizo, awe mtanzania au raia wa kigeni licha ya kuvutiwa na uzuri wake anapopita juu yake, picha ya raia wazalendo wa Watanzania wanaoipenda nchi yao, pia humjia akilini.

Ubungo Interchange imejengwa na vijana wa kitanzania waliokuwa asilimia 90 ya wajenzi wote, imesimamiwa na wataalamu wa ndani ya Tanzania ambao ni Wakala wa Barabara (TANROADS) wakiongozwa na Mtendaji Mkuu, Patrick Mfugale huku meneja mradi akiwa Mhandisi Barakaeli Mmari.

Mfugale


Saruji, mchanga, nondo na vifaa vingine vyote vilivyotumika katika ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango kikubwa ama zimetengenezwa na kuzalishwa na viwanda vya ndani vya Tanzania au ni vifaa vilivyo ndani ya Tanzania. Ubungo Interchange ni barabara za Watanzania zilizojengwa na Watanzania kwa kutumia akili, fedha, vifaa na nguvu kazi ya Watanzania wenyewe.

Barabara hizo za kuvutia katika ukanda wote wa Afrika Mashariki zinakutanisha barabara tatu za Mandela, Sam Nujoma na Morogoro na ujenzi wake ulikamilika Disemba, 2020.

Rais Magufuli


Rais John Pombe Magufuli alipotangaza mpango wa ujenzi wa barabara hizo kulikuwa na mapokeo ya aina mbili, kwanza ni Watanzania waliopokea taarifa za mpango huo kwa furaha kwa imani kwamba zitapunguza au kuondoa kabisa tatizo la msongamano wa magari katika eneo la Ubungo ambalo lilikuwa likidumaza sana uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Furaha hiyo pia ilijengeka katika nyuso za wananchi wengi kwa matumaini ya kupata ajira na zaidi ni tamaa ya maendeleo. Kila Mtanzania alitamani kuiona Tanzania ikiwa na interchange yenye mwonekano wa zile zilizo kwenye mataifa ya dunia ya kwanza

Mapokeo ya pili yalikuwa ya husda kutoka kwa maadui wa taifa ambayo nayo yaligawanyika katika makundi mawili makuu; la kwanza ni lile lililotamani mpango huo usifanikiwe na sababu yao kubwa ni kutotaka kuiona Tanzania ikipiga hatua za kimaendeleo huku kundi jingine ni lile lililotaka lihusike kwenye ujenzi ili kwanza livune pesa na kutoa ajira kwa watu wao ambao haina shaka wangeletwa kwa wingi kufanya kazi kwenye mradi huo na pia kutamani Tanzania iendelee kuwa tegemezi kwa kukosa pesa za ujenzi au kuomba msaada na wataalamu kutoka nje.

Matamanio haya yamekuwa hewa kwa sasa ambapo Watanzania wengi wanayaishi maono na falsafa za Rais Magufuli zinazowafanya watembee kifua mbele kwa sababu wanaamini wanaweza kuijenga nchi yao wenyewe na TANROADS imekuwa mfano bora kabisa katika hili.



Mei 2020, Mhandisi Barakaeli Mmari alipoutangzia umma kuwa kwa mara ya kwanza barabara ya ghorofa ya chini ya Morogoro itafunguliwa kwa majaribio ifikapo Mei 30, 2020 kwa kuruhusu magari kupita na Septemba 30, 2020 barabara ya ghorofa ya pili ya Nelson Mandela / Sam Nujoma itafunguliwa kwa majaribio pia, Watanzania na raia wa nchi jirani wanaotumia barabara ya Morogoro kama lango kuu la kuingilia jijini Dar es Salaam walianza kushuhudia picha halisi ya Tanzania mpya.



Mhandisi Mmari ambaye alitoa darasa la matumizi ya barabara hizo alisema kuna barabara ngazi tatu, ya chini, ya kati na ya juu. Ngazi ya chini itatumiwa na magari yanayotoka mjini kwenda Mwenge, Mwenge-Kimara, Kimara-Buguruni na Buguruni kwenda mjini. Vile vile, itatumiwa na magari yote yatakayokuwa yanapinda kushoto kwenye maungio hayo.

Alisema ngazi ya kati itatumiwa na magari yanayotoka Kimara kwenda mjini na yatokayo mjini kwenda Kimara.



Ngazi ya juu itatumiwa na magari yatokayo Mwenge kwenda Buguruni na yatokayo Buguruni kwenda Mwenge.

Mhandisi Mmari alisema barabara za juu zimejumuisha njia maalumu kwa ajili ya mabasi ya mwendo kasi.



Hivi sasa, Watanzania wakiwa wamezama katika ujenzi wa miradi mikubwa ya kitaifa, picha halisi ya ubora wa miradi hiyo inaonekana kwa kutazama na kupita juu ya barabara za ghorofa za Ubungo Interchange.

GULAM ATAFAKARI KUPAMBANA NA UBALOZI WA INDIA

 

Mwenyekiti wa Kampuni za MeTL, Gulam Dewji

NA MWANDISHI WETU

MFANYABIASHARI mwenye ukwasi wa kutosha ambaye kampuni, viwanda, mashamba na biashara zake zimetoa ajira kwa Watanzania na raia wa kigeni anatafakari kujibu mapigo dhidi ya Ubalozi wa India uliyoyataja makampuni yake kuwa siyo sehemu salama kufanya kazi.

Wiki iliyopita, siku moja baada ta Gulam kumpa maagizo mmoja wa wasaidizi wake kutuma ujumbe kwa Tanzania PANORAMA Blog wa kusaka suluhu baina ya menejimenti za Kampuni za Mohamedi Enterprises Tanzania Limited (MeTL) na wafanyakazi wa kigeni wanaodai kunyanyaswa alisema anajipanga kujibu mapigo.

Gulam alisema amesikitisha na tamko la ubalozi wa India lililosambazwa mitandaoni kwa sababu linalenga kuwatetea watu wanaomuibia na kumsumbua.

“Ndiyo nimeliona tamko kwani nani kasema hajui kuwa ni tamko la Ubalozi wa India, lakini mimi nasema nakusanya ushahidi halafu nitatoa tangazo kwa vyombo vya habari kwa sababu ubalozi unatetea wezi, unatetea watu wanaoniibia na kunitesa sana na hata polisi wanazo taarifa hizi. Sasa ninazungumza na ubalozi halafu nitatoa statement yangu ambayo mimi nitaitoa kama tangazo,” alisema Gulam.   

AWALI Tanzania PANORAMA Blog, iliripoti kuwa uongozi wa kampuni zilizo chini ya mwamvuli wa Mohamedi Enterprises Tanzania Limited (MeTL) umesema utatafuta njia ya kumaliza mgogoro baina yake na wafanyakazi ambao ni raia wa India katika meza ya mazungumzo.

Hayo yameelezwa na mmoja wa maafisa wa kampuni hiyo aliyetumwa na Mkurugenzi wa MeTL, Gulam Dewji kutoa ufafanuzi kwa Tanzania PANORAMA Blog kuhusu andishi lililowekwa kwenye mitandao ya kijamii likiwatahadhalisha raia wa India wote kuepuka kufanya kazi katika Kampuni za MeTL.

Andiko hilo mtandaoni linaeleza kuwa Ubalozi wa India umekuwa ukipokea kwa mfululizo malalamiko ya wafanyaakazi wa Kampuni za MeTL kunyanyaswa na uongozi pamoja na mwajiri wao kuwafungulia kesi za kughushi mahakamani kiasi cha kusababisha wanafamilia wa wafanyakazi hao kulazimika kurejea India.

Kwamba Mwenyekiti wa Makampuni ya MeTl, Gulam Dewji na maafisa waandamizi wamekuwa wakiwafanyia vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wafanyakazi hao wanapofikisha malalamiko kwao.

Linahitimishwa kwamba raia wote wa India wasikubali kuajiriwa na Kampuni za MeTL kutokana na mwenendo usiofaa wa viongozi wake wa juu.

Alipoulizwa Mwenyekiti Gulam, kuhusu suala hilo kupitia simu yake ya kiganjani alisema aandikiwe maswali kwa maandishi ili ayajibu na alipoandikiwa, muda mfupi baadaye mtu mmoja mwenye asili ya kiasia alituma ujumbe kwa njia ya whatsapp akieleza kuwa ametumwa na Gulam kufikisha ujumbe kwa Tanzania PANORAMA Blog.

Ujumbe aliuotuma ulisomeka; ‘Bwana Dewji amezungumza na sisi na ametuhakikishia uwajibikaji wa menejimenti katika kulinda maslahi ya wafanyakazi. Tumekubaliana kuwa na mazungumzo ya kina, tungependa kutatua jambo hili kwa njia ya mazungumzo.’

Ujumbe mwingine chini ya huo aliuotuma ulisomeka; ‘leo hii mmelalamika mazingira ya watu wenu ila tusema ukweli pia mnawanyanyasa sana Watanzania sema tu wanashindwa nani wa kuwasemea pia kutokana na hali za maisha yao ila mazingira ya ufanyaji kazi siyo.

Jitahidi za Tanzania PANORAMA Blog kuzungumza na Ubalozi wa India kuhusu suala hili zinaendelea.    

MWANAFUNZI ALIYEPOTEA ST. MARY’S APATIKANA

 

Labna Said

NA MWANDISHI WETU

LABNA Salim Said,  mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s iliyopo Mbezi Makonde ambaye alipotea tangu Oktoba 4, 2020, amepatikana.

Mwanafunzi huyo alipatikana Disembe 12, 2020, eno la Banana Relini akiwa amewekwa kinyumba na mwanaume ambaye jina lake halikufahamika mara moja baada ya kufanikiwa kuwakimbia polisi waliokwenda kuwakamata.

Taarifa za kupatikana kwa Labna zilithibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC) Ramadhani Kingai katika mahojiano mafupi kwa njia ya simu ambaye alisema, taarifa za kupatikana kwa mwanafunzi huyo anazo lakini hawezi kuongea zaidi kwa sababu yupo kwenye kikao.

Mama mzazi wa Labna anayefahamika kwa jina la Rabia Swedan alisema walipata taarifa za kuwepo kwa mtoto wao eneo Banana Relini usiku na walifika eneo hilo wakiwa wameambatana na polisi wawili na kumkuta akiwa amelala chini pamoja na aliyemtorosha.

“Inasikitisha, tulipata taarifa za huyu mtoto kuwepo Banana Relini usiku, tukaenda Kituo cha Polisi Stakishari kuomba polisi, tukapewa wawili tukaambatana nao mpaka kwenye hiyo nyumba tukawakuta wamelala chini. Yule bwana aliyekuwa naye alipotuona na polisi akakurupuka akakimbia, sasa kwa sababu polisi walikuwa wawili hawakuweza kumfukuza.

“Mtoto alikuwa hoi, tulimpeleka Stakishari polisi huo usiku wa saa saba akakaa hapo wakimuhoji mpaka saa 12.00 asubuhi, kwa jinsi alivyokuwa wakatuambia tumpeleke hospitali.

“Tukampeleka Hospitali ya Amana na baada ya matibabu tukamchukua hadi Kituo cha Polisi Goba kwa sababu ndiko kesi yake inakopelelezwa, nao  wakamuhoji wakaturudishia tuendelee kumtibu ila akiwa na nafuu tutampeleka tena polisi,” alisema Swedan.   

Mwanafunzi msichana Labna wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 na kutokomea kusikojulikana hadi alipopatikana Disemba 12.

Labna alitoweka akiwa chini ya uangalizi wa shule lakini taarifa za kutoweka kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake, Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa Labna akiulizia kama ameishafika nyumbani.

Katika hatua ya kushangaza, uongozi wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s haukutoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mwanafunzi huyo na badala yake wazazi ndiyo walioripoti tukio la mtoto wao kupotea akiwa shuleni.

 

 

Thursday, December 10, 2020

MeTL YAZUNGUMZIA TUHUMA ZINAZOIANDAMA

 

Mwenyekiti wa Makampuni ya MeTL, Gulam dewji

NA MWANDISHI WETU

UONGOZI wa Kampuni zilizo chini ya mwamvuli wa Mohamedi Enterprises Tanzania Limited (MeTL) umesema utatafuta njia ya kumaliza mgogoro baina yake na wafanyakazi ambao ni raia wa India katika meza ya mazungumzo.

Hayo yameelezwa na mmoja wa maafisa wa kampuni hiyo aliyetumwa na Mkurugenzi wa MeTL, Gulam Dewji kutoa ufafanuzi kwa Tanzania PANORAMA Blog kuhusu andishi lililowekwa kwenye mitandao ya kijamii likiwatahadhalisha raia wa India wote kuepuka kufanya kazi katika kampuni za MeTL.

Andiko hilo mtandaoni linaeleza kuwa Ubalozi wa India umekuwa ukipokea kwa mfululizo malalamiko ya wafanyaakazi wa Kampuni za MeTL kunyanyaswa na uongozi pamoja na mwajiri wao kuwafungulia kesi za kughushi mahakamani kiasi cha kusababisha wanafamilia wa wafanyakazi hao kulazimika kurejea India.

Kwamba Mwenyekiti wa Makampuni ya MeTl, Gulam Dewji na maafisa waandamizi wamekuwa wakiwafanya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wafanyakazi hao wanapofikisha malalamiko kwao.

Linahitishwa kwamba raia wote wa India wasikubali kuajiriwa na Kampuni za MeTL kutokana na mwenendo usiofaa wa viongozi wake wa juu.

Gulam

Alipoulizwa Mwenyekiti Gulam, kuhusu suala hilo kupitia simu yake ya kiganjani alisema aandikiwe maswali kwa maandishi ili ayajibu na alipoandikiwa, muda mfupi baadaye mtu mmoja mwenye asili ya kiasia alituma ujumbe kwa njia ya whatsapp akieleza kuwa ametumwa na Gulam kufikisha ujumbe kwa Tanzania PANORAMA Blog.

Ujumbe aliuotuma ulisomeka; ‘Bwana Dewji amezungumza na sisi na ametuhakikishia uwajibikaji wa menejimenti katika kulinda maslahi ya wafanyakazi. Tumekubaliana kuwa na mazungumzo ya kina, tungependa kutatua jambo hili kwa njia ya mazungumzo.’

Ujumbe mwingine chini ya huo aliuotuma ulisomeka; ‘leo hii mmelalamika mazingira ya watu wenu ila tusema ukweli pia mnawanyanyasa sana watanzania sema tu wanashindwa nani wa kuwasemea pia kutokana na hali za maisha yao ila mazingira ya ufanyaji kazi siyo.

Jitahidi za Tanzania PANORAMA Blog kuzungumza na Ubalozi wa India kuhusu suala hili zinaendelea.    

BOSI AIRTEL ALIVYOKWAPUA MAMILIONI BILA KUBAINIKA

 



NA MWANDISHI WETU

IMEBAINIKA kuwa, mmoja wa waliokuwa maofisa wa juu wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, alichota mamilioni ya shilingi za kampuni hiyo kwa kufanya nayo biashara hewa.

Ili kufanikisha uchotaji wa mamilioni hayo, kigogo huyo ambaye jina lake tunalifadhi kwa sasa, alifungua kampuni iliyokuwa ikitoa huduma kwenye minara ya simu ya Aitel na kuweka mtu wa kuisimamia ili kuficha uhusika wake.

Uchunguzi wa awali kuhusu ufisadi wa mali za umma uliofanywa na Tanzania PANORAMA Blog kwa Kampuni ya Aitel umeonyesha kuwa, Airtel baada ya kubadilishwa jina kutoka Zain, kigogo huyo aliyekuwa amekwishachota pesa nyingi kwa kufanya biashara za udanganyifu, alifungua kampuni ambayo haraka haraka ilianza kupewa zabuni za Airtel.

Kwa mujibu wa uchunguzi, kampuni iliyofunguliwa ( jina tunalo) iliwekwa chini ya usimamizi wa mtu mwingine ambaye alikuwa akiripoti moja kwa moja kwa kigogo huyo na yeye alikuwa akifika kukagua mwenendo wake siku za mwisho wa wiki ambazo wafanyakazi hawakuwa kazini.

Uchunguzi umeonyesha kuwa kigogo huyo alitumia nafasi yake katika Airtel kutazama mianya ya kuiwezesha kampuni yake kupata zabuni hewa zenye thamani ya mamilioni ya fedha, jambo ambalo lingefanikiwa kampuni hiyo ingefungwa au kubadilishwa jina na iwapo ingetiliwa shaka na kuanza kufuatiliwa na mamlaka serikali, kigogo huyo angeacha kazi na kukimbilia nje ya nchi; na hiyo ingetegemea na hali halisi ya wakati ambao ingegundulika.

Tanzania PANORAMA Blog katika uchunguzi wake imebaini kuwa kigogo huyo baada ya kufanikiwa kuchomeka jina la kampuni yake kwenye menejimenti ya Airtel kama moja ya kampuni zenye sifa ya kufanya biashari kubwa, kwa kutumia wadhfa wake alianza kushawishi zabuni zenye thamani kubwa ipewe kampuni yake.

Uchunguzi umebaini kuwa haraka haraka bosi huyo aliwasilisha kwa menejimenti pendekezo la kununuliwa kwa jenereta mbili kubwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuendesha minara ya Airtel.

Pendekezo hilo liliainisha bei ya jenereta hizo kuwa; moja gharama yake ni Dola za Marekani 240,000 na ya pili Dola za Marekani 480,000 ambazo zingekaa makao makuu tayari kufanya kazi wakati wa dharura.

Mchakato wa ununuzi wa jenereta hizo ulifanyika haraka na malipo yalifanyika kwa mikupuo mitatu. Mkupuo wa kwanza ulihusisha malipo ya Dola za Marekani 480,000 ambazo zililipwa kwa invoice mbili na Dola za Marekani 240,000 invoice moja.

Hata hivyo Tanzania PANORAMA Blog inaripoti kwa uhakika kuwa manunuzi ya jenereta hizo hayakufanyika bali pesa hizo ziliwekwa kibindoni na bosi huyo.

Taarifa zinaeleza kuwa wakati akiandaa mpango mwingine wa kuchota zaidi ya Dola za Marekani 500,000 Serikali ya Awamu Tano ilianza kufuatilia mwenendo wa kampuni hiyo ili kuinusuru isife kutokana na hali mbaya iliyokuwa nayo.

"Baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kufuatilia mwenendo wa kampuni kwa karibu, bosi alijua sasa atakuwa hatarini akaamua kuacha kazi mara moja kabla hajafanikisha mipango yake mingine.

"Wakaguzi wa serikali walipokuja waligundua kuwa manunuzi ya hizo jenereta yalikuwa hewa kwani hakukuwa na hizo jenereta bali hela za Airtel zilikwapuliwa zikawekwa mfukoni lakini hawakuweza kumnasa bosi kwa sababu alikuwa ameishaacha kazi.

"Na ilikuwa ngumu kumnasa kwa sababu yeye alikuwa nyuma ya ile kampuni ambayo aliweka mtu wake, huyo ndiyo akawa bosi. Huyo ndiyo alipata msukosuko kidogo lakini sasa yupo huru.

"Kwa sababu serikali ilishindwa kumbaini hakukimbilia nje ya nchi bali alikwenda nje kidogo ya jiji akajenga shule yake kubwa huko akaanzisha na biashara zake nyingine. Mke wake ambaye alikuwa mtumishi wa NSSF aliyeaacha kazi ili kusaidiana na yule bwana aliyemuweka kuendesha hiyo kampuni ya wizi sasa ndiyo anatokeza zaidi kwenye biashara zake, " kilieleza chanzo cha ndani cha taarifa.

Tanzania PANORAMA Blog itaripoti ufisadi huu kwa kina mara baada ya kukamilisha uchunguzi wake.

 

Wednesday, December 9, 2020

POLISI WAACHIWA MZIGO WA KUMTAFUTA MWANAFUNZI ALIYEPOTEA ST MARY'S SEK

 

Katibu Mkuu Akwilapo

NA MWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu wa Wazara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Leonard Akwilapo amesema wajibu wa kumtafuta  mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St Mary's, Labna Said Salim aliyepotea akiwa chini ya uangalizi wa shule ni wa Jeshi la Polisi

Ameyasema hayo jana katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog ambayo ilimuuliza mchango wa wizara kumtafuta mwanafunzi huyo aliyepotea Oktoba 4, 2020.

"Hilo jambo wenye wajibu ni polisi na ndiyo maana sisi halijafika kwetu na hata kama lingekuwa limefika tungelipeleka polisi kwa sababu wao ndiyo wenye wajibu wa mambo kama hayo," alisema Akwilapo.

Labna


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ramandani Kingai alipoulizwa jana kuhusu hatua waliyofikia katika msako huo alisema mpasa sasa hawafikiwa kumpata mwanafunzi huyo

Alipoulizwa kuhusu vijana saba waliokamatwa wakivuta bangi nyumbani kwa Kamishna Mstaafu wa Jeshi Magereza ambaye jina lake limehifadhiwa, Kamanda Kingai alisema vijana hao ambao ni wanafunzi bado wanafanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne hivyo wanasubiriwa mpaka watakapomaliza ndipo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Taarifa ya uchunguzi wa awali wa kupotea kwa mwanafunzi huyo iliyotolewa na Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kinondoni, Joseph Kapere ambaye ni mjumbe wa timu iliyoundwa na Serikali ya Wilaya ya Kinondoni kuchunguza kupotea kwa mtoto huyo, mahali alipo sasa na mazingira ya kutoweka kwake ilieleza kuwa timu hiyo ilithibitisha pasipo shaka kuwa Shule ya Sekondari ya St Mary’s Mbezi Makonde imepungukiwa sifa zinazostahili kutoa elimu kwa mwanafunzi.

Wajumbe wengine katika timu hiyo ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ufisa Usalama na Mdhibiti wa Ubora wa Elimu Kanda.

Kapere alisema tayari Mkuu wa Shule ya St. Mary's, Recca Ntipoo amehojiwa na kuungama kutenda makosa katika baadhi ya mambo kwenye sakata hilo na kwamba aliipeleka timu hiyo mahali alikodai Labna alikwenda kuishi na mpenzi wake baada ya kutoroka shule.

Alisema timu ilibaini shule hiyo ilifanya makosa kutotoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mtoto na pia kukaa kimya  siku nne bila kutoa taarifa kwa wazazi kuhusu kutoweka kwake wala kuwajulisha kuwa amewaeleza walimu hataki shule.

Katika maelezo yake Kapere alisema, Ntipoo aliungama kufahamu vitendo vya mwanafunzi kutoka shule kwa kuruka ukuta usiku na kwenda maeneo hatarishi kwao jambo ambalo Mwalimu huyo aliliona kuwa  la kawaida kwa sababu alikuta likifanyika shuleni hapo.

Aidha, Kapere alisema timu ilibaini shule hiyo kuwa na mazingira machafu, kukosa ulinzi wa kutosha na kutokuwa na ukuta imara.

Alisema mambo mengine yaliyogundulika katika uchunguzi wa timu hiyo ni kubainika kwa nyumba ya Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Magereza ambayo ina shamba la bangi  ambamo walikutwa wavulana saba, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya St Mary's waliokuwa wakivuta pamoja.

 Mwanafunzi msichana Labna wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 na kutokomea kusikojulikana na hadi sasa hajapatikana.

Labna alitoweka akiwa chini ya uangalizi wa shule lakini taarifa za kutoweka kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa Labna akiulizia kama ameishafika nyumbani.

Katika hatua ya kushangaza, uongozi wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s haukutoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mwanafunzi huyo na badala yake wazazi ndiyo walioripoti tukio la mtoto wao kupotea akiwa shuleni.

MKANDARASI SOKO LA TANDALE MWIZI MDOGO MDOGO - MKURUGENZI KINONDONI

 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Aron Kigurumjuli


NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Aron Kigurumjuli amesema mkandarasi aliyepewa kandarasi ya kujenga soko jipya la Tandale, Namis Corporation LTD ni mwizi mdogo mdogo ambaye akikamatwa hurejesha alichoiba.

Kigurumjuli aliyasema hayo wiki iliyopita katika mahojiano maalumu na Tanzania PANORAMA Blog yaliyofanyikia Kinondoni Dar es Salaam.

Alikuwa akijibu kuhusu madai kuwa, mkandarasi huyo alighushi leseni yake ya biashara na alibainika kutenda kosa hilo wakati akisaka zabuni ya ujenzi wa soko la Tandale.

Katika majibu yake, Kigurumjuli alisema Namis Corporation LTD haikughushi leseni ya biashara isipokuwa ilifanya udanganyifu ulioiwezesha kuwa inalipa pesa kidogo kinyume na hitaji la leseni yake na hivyo ikawa inaiibia serikali pesa kidogo za tozo ya leseni.

Kigurumjuli alisema, wataalamu wake walibaini kuwepo kwa dosari hiyo kwenye leseni ya Namis Corporation LTD wakati wa ukaguzi wa nyaraka uliofanyika kabla ya kuzawadiwa zabuni ya ujenzi wa soko la Tandale.

"Unasema inadaiwa si ndiyo? sasa mimi nakwambia madai hayo ni uongo. Namis hajaghushi leseni ya biashara, sema, acha nikusaidie yule alikuwa akiiba kidogo hela za serikali. Ni mwizi mdogo mdogo tu lakini tulimbaini tukambana, akakiri tukampiga faini, akalipa.

"Alikuwa anaibaje, sikiliza. Leseni za biashara zipo za aina nyingi sana, zipo za mpaka Dola za Marekani 200,000. Huyu leseni yake alipaswa alipie kiwango cha juu lakini yeye akakataka ya kiwango cha chini, akawa analipa below ya kiwango anachopaswa kulipa. Kama sikosei kwa shughuli zake za ukandarasi alipaswa kulipa 60,000 lakini yeye akawa analipa 30,000.

" Sasa wakati wa ukaguzi wa nyaraka zake alipokuwa ameomba tenda ya soko la Tandale wataalamu wangu wakagundua huyu anatuibia, anaiibia serikali. Wakambana, alibishabisha kidogo lakini alibanwa haswa akakubali kulipa.

"Tulimpiga faini kubwa. Shilingi milioni nane ya miaka mitano aliyokuwa amefanya ujanja wake. Sasa huyu huwezi kumpa kosa kubwa hilo la kughushi, huyu ni mwizi mdogo mdogo tu na alibanwa akalipa. Hayo mengine sasa kamuilize mwenyewe," alisema Kigurumjuli.

Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta Mkurugenzi wa Namis Corporation LTD, Thomas Uiso kuzungumzia suala hilo bila mafanikio kwani tongu aliposema mambo yote yanayohusiana na kukwama kwa ujenzi wa soko jipya la Tandale ambalo yeye ndiye mkandarasi aulizwe Mkurugenzi Kigurumjuli amekuwa hapokei simu wala kujibu ujumbe wa maandishi.

Tanzania PANORAMA jana lilimpigia simu Uiso hakupokea na lilimtumia ujumbe wa maandishi kumuuliza kuhusu jambo hilo hakuujibu licha kuonyesha umemfikia na ameusoma.

Taarifa zilizolifikia Tanzania PANORAMA Blog zilieleza kuwa kampuni hiyo ulighushi leseni ya biashara na ilipata kandarasi mbalimbali kwa kutumia leseni hiyo ya kughushi.

Tuesday, December 8, 2020

TANROADS NA KISA CHA NDOTO ZA KAKAKUONA KWA WATANZANIA

 

Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Partick Mfugale

MAISHA ya wananchi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa sasa yamebadilika. Miundombinu ya barabara na madaraja ya kisasa ambayo hapo awali Watanzania waliyaona kwenye picha na sinema zilizoandaliwa katika nchi za Ulaya na Amerika, sasa ipo nchini na kwa kiwango kikubwa imekuwa msaada kwa safari zao wenyewe na pia kusafirisha mazao na bidhaa za biashara.

Mabadiliko hayo ya maisha ya wanachi wa Tanzania yameenda sambamba na mabadiliko ya mwenendo wa uchumi wa Taifa. Uchumi wa Tanzania sasa unakuwa kwa kasi kubwa na tayari umekwishachumpa kutoka kwenye uchumi wa nchi masikini hadi uchumi wa kati, miaka mitano kabla ya matarajio.

Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa kuchumpa kwa uchumi wa Tanzania kutoka ule wa nchi masikini hadi uchumi wa kati miaka mitano kabla ya matarajio kumewezeshwa pamoja na mambo mengine, ujenzi wa miondombinu imara na yenye kuvutia jambo linaloifanya nchi, kwanza kufikika sehemu zote lakini pia kuwa na mandhari ya kuvutia.

Haikuwa kazi rahisi kuyafikia mafanikio haya katika sekta ya ujenzi wa miundombinu. Wapo Watanzania waliotokwa jasho la damu na chumvi kuyawezesha na kinara wa utiririkaji jasho la kuigeza Tanzania kuwa mithili ya paradiso ni Rais John Pombe Magufuli ambaye kwa miaka mitano ya awamu ya kwanza ya utawala wake, ratiba yake ya kulala imebadilika, analala kwa saa chache na muda mwingi yupo kibaruani akichuruzikwa jasho.

Rais John Pombe Magufuli


Wa pili katika hili, ni Wakala wa Barabara, (Tanroads) ambao mabadiliko ya kiutendaji katika taasisi za serikali yaliyoasisiwa na Rais Dk. Magufuli mara tu alipoingia marakani mwaka 2015  yaliwafanya wawe kama wanajimu kwa kutafasili ndoto za mnyama mdogo anayejulikana kwa jina la Kakakuona.

Kakakuona hutembea akiota kuwa akikutana na binadamu na kufanikiwa kukimbia kwa kasi ili binadamu asimkamate kisha akajificha asionekane basi atakuwa na uwezo wa kibinadamu wa kufanya maendeleo makubwa katika maisha yake.

Binadamu nao, (baadhi ya jamii) huota kwamba wakimuona mnyama mdogo Kakakuona, basi kuna baraka mbele yao kwa sababu mnyama huyo haonekana hovyo hovyo. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Tanroads ambayo ndoto za Kakakuona kutaka kukimbia kwa kasi kisha ajifiche ili awe kama binadamu na maendeleo yake imezifanya ziwe za kweli na kwa Watanzania waliokuwa wakiota siku wakikutana na Kakakuona basi kuna baraka inayokuja mbele yao, Tanroads imezigeuza ndoto zao kuwa kweli. 

Ukweli huu umo katika kazi za kutukuka zilizofanywa na Tanroads kwenye ujenzi wa madaraja ambayo sasa yamegeuka kuwa vivutio vya utalii kwa watanzania wenyewe na hata baadhi ya wageni kutoka mataifa ya nje kutokana na muonekane wake wa kuvutia. Mbali na hilo, ndoto za watanzania katika baadhi ya maeneo ambako kulikuwa na matatizo makubwa ya kufika na hata uhai wa watu kupotea kwa sababu ya kukosa madaraja, hali hiyo sasa haipo, madaraja yamejengwa na hapa chini ni orodha fupi ya madaraja hayo.

DARAJA LA MAGUFULI

 Kwa mujibu wa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Dorothy Ntenga, Daraja la Magufuli lililojengwa katika Mto Kilombero liligharimu zaidi ya shilingi bilioni 50 ambazo zote zilitolewa na Serikali.



Kwamba ujenzi wa daraja hilo umezingatia viwango vilivyowekwa kwenye mkataba na mkandarasi ambaye ni kampuni ya M/S China Railway 15 Group Corporation.

 Daraja hilo linarahisisha shughuli za usafirishaji wa mazao, ufugaji na madini katika Wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero.



Ilikuwa ndoto ya muda mrefu kwa wananchi hao kupata daraja na wakati likijengwa, mmoja wa wakazi wa maeneo hayo, Zainabu Mtalanga alipata kumwambia aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa kuwa;  “Tunaishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja hili kwani limekuwa mkombozi kwetu wananchi wa Wilaya za Ulanga na Kilombero.



“Hapo nyuma vifo vingi vimetokea pasipo kutegemewa wakati tukitumia kivuko kufuata huduma za kijamii wilaya jirani ambapo kuna huduma zote za muhimu.”

DARAJA LA MAGARA

Taarifa ya Meneja wa Tanroads Mkoa wa Manyara, Mhandisi Bashiri Rwesingisa, kuhusu ujenzi wa Daraja la Magara inaeleza kuwa ujenzi wake uligharimu zaidi ya shilingi bilioni 12



Lilijengwa na Mkandarasi M/s China Railway Seventh Group likiwa na urefu wa mita 84 na barabara za maingilio KM 4 na linaunganisha Hifadhi ya Taifa ya Manyara na Tarangire kupitia Mayoka, pamoja na kuunganisha mashamba makubwa ya mpunga na miwa yaliyopo ng’ambo ya pili ya Mto na Masoko ya Babati na Arusha.



Daraja la Magara ni kichocheo cha ukuaji wa utalii na uchumi  katika Mkoa wa Manyara na Taifa kwa ujumla likiwa umbali wa KM 21 kutoka Mbuyu wa Mjerumani katika barabara kuu ya Babati – Arusha na sasa linawezesha kuvuka Mto Magara katika barabara ya Mkoa ya Mbuyu wa Mjerumani – Mbulu yenye urefu wa KM 49.

DARAJA LA MOMBA

Meneja wa Tanroads wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Ndelalutse Karoza analieleza daraja hilo kuwa ni kiunganishi cha mkoa huo na Mkoa wa Songwe kwa upande wa Bonde la Ziwa Rukwa na limejengwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania kwa 100.



Kwa mujibu wa Karoza, gharama za ujenzi wa Daraja la Momba  ni shilingi bilioni 17.7 na limejengwa na Kampuni ya ukandarasi ya Genjio Engineering Group Cooperation ya China

Karoza anasema ujenzi wa daraja hilo ni muhimu sana kwa mikoa ya Rukwa na Songwe pamoja na Tanzania kwa ujumla na kubainisha kuwa ukamilifu wa daraja hilo utawainua wananchi kiuchumi na kijamii ikiwemo kupunguza gharama za usafirishaji wa mazao.

Daraja la Mto Sibiti lipo Iramba mkoani Sindiga. Lina urefu wa mita 83 na gharama za ujenzi wake ni shilingi bilioni 19.2

 DARAJA LA NYERERE (KIGAMBONI)

Lipo Kurasini jijini Dar es Salaam na linamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na NSSF.



Ni daraja la aina ya kuning’inia lililojengwa na Mkandarasi China Railway Jiangchang Engineering (T) Ltd na China Major Bridge Engineering Company. Lina urefi wa mita 680 na upana wa mita 27.5 na gharama yake ya ujenzi ni Dola za Marekani milioni 136

Daraja la Nyerere ndilo linalovuka mkondo wa kurasini jijini Dar es Salaam likiwa na njia sita za kupitisha magari. Daraja la Nyerere ndilo kubwa kuliko yote Afrika Mashariki na linavutia sana kutokana na kujengwa kwa ustadi.  

 

 

MKURUGENZI KINONDONI AANZA KUFANYA VITUKO

 

Mkurugenzi Manispaa ya Kinondoni, Aon Kigurumjuli

NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI wa Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni, Aron Kigurumjuli, sasa ameanza kufanya vituko kwa kuwazuia waandishi wa habari kuingia na vitendea kazi vya aina yoyote ofisini kwake wanapokwenda kufanya naye mahojiano.

Kigurumjuli ameweka mlinzi katika mlango wa ofisi yake anayechagua watu wa kuingia na pia anachagua nani na yupi asiingie ambapo leo asubuhi, mlinzi huyo ameizuia Tanzania PANORAMA Blog kuonana na bosi wake kwa ajili ya kufanya mahojiano ikiwa na 'notebook' na kalamu mpaka itii sharti la kuingia mikono mitupu.

Katika hatua ya kushangaza, Kigurumjuli pia, wiki iliyopita alitoa maneno ya kashfa na kejeli kwa viongozi waandamizi wa serikali pamoja na aidha; leo hakupokea simu wala kujibu meseji kwa watu aliopanga miadi ya kukutana nao ofisini kwake.

Vituko hivi vya Kigurumjuli vimekuja siku chache baada ya yeye mwenyewe kuieleza Tanzania PANORAKA Blog kuwa amepata presha hivyo hawezi kwenda kazini baada ya kuripotiwa kwa taarifa za kukwama kwa ujenzi wa soko jipya la Tandale huku taarifa nyingine zikieleza kuwa ana hasira kwa sababu ya kuripotiwa kwa mkwamo wa ujenzi wa soko la Tandale na amejiapiza kuwashughulikia wanaofuatilia habari hiyo.

Katika tukio la leo asubuhi, Kigurumjuli alikuwa ametoa miadi ya kukutana ili azungumzie matatizo yaliyokwamisha ujenzi wa soko la Tandale. Miadi hiyo haikufanikiwa baada ya mlinzi aliyemuweka mlangoni kutaka aachiwe vitendea kazi vyote vya Tanzania PANORAMA Blog ikiwa ni pamoja na begi alilotaka apewe alishike.

"Toa vitu vyako vyote kwenye kibegi chako weka hapo kwenye kiti, hilo begi nipe hapa nilishike ukitoka utachukua vitu vyako nitakupa na begi lako," alieleza mlinzi ambaye jina lake halikufahamika.

Alipoelezwa kuwa ndani ya begi kuna kalamu, 'notebook' na nyaraka kadhaa na kufunguliwa akague na mwandishi alieleza yupo tayari kupekuliwa,  alisisitiza kuwa bosi wake ameagiza waandishi wasiingie na kitu chochote isipokuwa wao tu.

"Hii ni amri, kalamu na karatasi zako toa weka kwenye kiti, begi nipe hapa nitakushikia hatuna sababu ya kubishana," alisema kwa msisitizo.

Tanzania PANORAMA Blog haikumpatia begi mlinzi huyo kama alivyokuwa akisisitiza kwa sababu lilikuwa na taarifa za kuwepo kwa mipango miovu ya kupandikiziwa vitu visivyofaa kisha wangeitwa wana usalama kupekua begi hilo na kukuta vitu hivyo kabla ya kuwatia matatani kwa lengo la kuwazuia wasiripoti taarifa za soko la Tandale.

Unezi wa soko jipya la Tandale ulipokuwa umefikia mwezi Agosti


Kabla ya kuondoka eneo hilo, lilimpigia simu Mkurugenzi huyo kumjulisha hali halisi ilivyo hapo nje ya mlango wa ofisi yake, simu yake ilisikika ndani ikiita lakini hakuipokea na pia alitumiwa ujumbe mfupi wa maneno mara tatu ambao aliusoma lakini hakujibu.

Katika mahojiano ya wiki iliyopita kuhusu kukwama kwa ujenzi wa soko la Tandale na kuweka zuio kwa waandishi wa habari kiripoti habari za soko hilo bila ruhusa yake, Kigurumjuli alisema yeye binafsi ndiye aliyekwenda kutafuta fedha za ujenzi wa soko la Tandale, Wizara ya Fedha na Mipango na alipewa za kutosha ila tatizo lililopo sasa ni kukosekana kwa saruji.

Alipoulizwa sababu iliyomfanya yeye binafsi kwenda wizarani kushawishi kutolewa kwa fedha huku tayari aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jaffo akiwa amekwishatoa tamko kuhusu ujenzi wa masoko yaliyokuwa kwenye mpango wa kujengwa..... haraka alilikatisha swali hilo na kuanza kung'aka.

"Ni kinini hicho, Selemani Jafo ndiyo kitu gani hicho. Hapa unaongea na Mkurugenzi, upo ofisini kwa mkurugenzi usinitajie majina ya ajabu ajabu wewe. Huyo Jafo wakati nahangaika hazina alikuwepo?

 

Kigurumjuli

“Fedha nimetafuta mimi na nimepewa mimi na nimekujibu hivyo au ulisikia kuna Jafo au huyo mkuu wenu wa mkoa? Wao kazi si kutembea tu na ..... (anasema maneno yasiyofaa) kwenye miradi tunayotafuta sisi. Hivi sasa tuna tatizo la saruji usiniletee mambo ya wanasiasa hapa. Uliza swali jingine," alisema kwa sauti ya juu Kigurumjuli.

Aidha Kigurumjuli alikana kutoa maagizo kwa mkarandasi yanayowataka waandishi wa habari kuwa na vibali vya maandishi kutoka kwake wanapotaka kuripoti habari za ujenzi wa soko la Tandale.

Taarifa ya kuwepo kwa zuio hilo kwa waandishi wa habari lilitolewa na meneja miradi wa Kampuni Namis, James Msumali ambaye baada ya kufikiwa na Tanzania PANORAMA Blog na kuombwa kuzungumzia mkwamo huo alisema mkataba wa ujenzi una kipengele kinachozuia kutolewa kwa taarifa yoyote ya ujenzi wa soko mpaka kiwepo kibali cha maandishi kutoka Kigurumjuli.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa kampuni ya Namis Thomas Uiso ambaye awali alikuwa ameitaka Tanzania PANORAMA Blog kumpelekea maswali kwa maandishi ili naye apate wasaa mzuri wa kuyajibu, ombi ambalo lilitekelezwa, alipotafutwa wiki iliyopita aliandika ujumbe wenye maneno machafu badala ya kujibu na muda mfupi baadaye aliufuta kisha alipiga simu na kueleza kuwa soko la Tandale linasimamiwa na Mkurugenzi ambaye ameagiza mwandishi yoyote anayetaka taarifa aelekezwe kwake.

"Maswali gani, wewe......(anaandika maneno ambayo hatuwezi kuyaandika). Nimepata taarifa zako mkurugenzi kanambia, hovyo sana wewe kumbe unachimba maisha ya watu. Ukimtaja Jafo au Kunenge ndiyo watu tutaogopa? Hao ni ........ (Anaandika maneno yasiyoandikika) huu ni utawala mwingine utapotea wewe na hutamuona Jafo wala Kunenge.

"Kuwa gentleman bhana, hapa ni mjini, haya ni maisha. Kwani unadhani hata nikiharibikiwa wewe ndiyo utapewa hiyo tenda? Ondoa huo uchafu ulioandika kwenye blog yako halafu kamuone mkurugenzi maisha yaendelee...., »alisema Uiso.

WIKI ILIYOPITA Tanzania PANORAMA Blog iliripoti kuwa, WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa imeelekeza nguvu kubwa kwenye ujenzi wa miundombinu, shule, hospitali na masoko, jitihada hizo zimeanza kuonyesha dalili ya kuingia doa baada ya kusimama kwa ujenzi wa soko jipya la Tandale.

Katikati ya hilo, msimamo wa serikali ya awamu ya tano wa kutoa taarifa zinazohusu shughuli za maendeleo bila ukiritimba, zinazofanywa na serikali ili kutoa fursa kwa wananchi kujua miradi inayotekelezwa kwa kodi zao, nao unaonekana kuingia doa baada ya mkandarasi anajenga soko la Tandale kuweka zuio la upatikanaji wa taarifa hizo.

Haya yamebainika baada ya Tanzania PANORAMA Blog kufika eneo la ujenzi wa soko jipya la Tandale mapema wiki iliyopita kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo baada ya kudokezwa na baadhi ya wafanyakazi kuwa umesimama kutokana na ukosefu wa fedha.

Tanzania PANORAMA baada ya kufika katika eneo la mradi lilishuhudia mafundi wakiwa wamekaa kivulini huku ujenzi ukiwa hauendelei na baada ya kuwahoji baadhi yao walisema wanasubiri kulipwa fedha zao waondoke kwa sababu mahali hapo hakuna kazi tena.

"Bora umekuja na sijui umeingiaje huku maana hamruhusiwi nyie kuingia humu na wakikuona watakugawana. Hapa hakuna kazi kama unavyoona ujenzi umesimama hakuna fedha. Tunasikia bosi hajalipwa huko serikalini ndiyo bado anafuatilia malipo lakini sisi tumeambiwa tukiulizwa tuseme tuna tatizo la simenti ambalo ni tatizo la kitaifa kwa sasa.

" Kama unaweza twende tukupeleke kwa msimamizi wetu ukamuhoji ila uwe unajiamini. Ila sisi tunasubiri akipata pesa kutoka serikalini akitulipa ndiyo basi tunatafuta kazi sehemu nyingine maana hata wiki hii mnafanya kazi wiki ijayo hakuna kazi sasa tunajiuliza hiyo serikali inatoa hela kwa wiki?" alisema mmoja wa mafundi hao.

Msimamizi wa mradi ambaye alipofikiwa na Tanzania PANORAMA na kuulizwa kwanza alielekeza afuatwe ofisini ambako alichukua simu na kuwasiliana na makao makuu ya kampuni yake kisha alisema;

"Unasema kuna wenzako kwenye gari wanakusubiri .... umesema hujapiga picha.... hili ni eneo la site, mtu yoyote haruhusiwi kuingia humu bila kibali cha makao makuu, awe mkuu wa mkoa, awe waziri anapotaka kuja hapa ni lazima awe na kibali kwa sababu anaweza kuangukiwa na kitu kizito kama nondo au ubao ukaaumia.

"Sasa nimeongea na makao makuu, nadhani umeona naongea na simu, kama una maswali nenda huko watakujibu na kama unataka kutembelea hapa uje na kibali cha maandishi kutoka makao makuu.

"Tena tumekuheshimu sana kwa sababu umeingia eneo ambalo haliruhusiwi ila kwa vile una wenzako nje njoo nikipitishe njia salama usije ukajikwaa halafu mkaanza kutunga uongo, " alisema.

Tanzania PANORAMA lilifika Makao Makuu ya Kampuni ya Namis, iliyopo Mbezi Africana ambayo ndiyo iliyopewa kandarasi ya kujenga soko la Tandale kwa ajili ya kupata maelezo ya kasimama kwa ujenzi wa soko hilo na kuelezwa kuwa mkataba wa ujenzi una kipengele kinachozuia kutoa taarifa yoyote ya mwenendo wa ujenzi isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Akizungumza kuhusu katazo hilo lililo kwenye mkataba huo, Meneja Mradi aliyejitambulisha kwa jina la James Msumali alisema changamoto zinazowakabili katika ujenzi huo anaweza kuzizungumzia iwapo atapata idhini ya maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa.

"Mimi ndiyo meneja mradi na ndiye ninayeweza kuzungumza, boss unayetaka kuonana naye hayupo. Utaratibu upo hivi, mkataba wetu una kipengele kinachoelekeza kuwa taarifa yoyote ya mradi haiwezi kutolewa mpaka kwa Kibali cha Mkurugenzi.

"Tena Kibali cha maandishi au anipigie simu yeye mwenyewe aseme nitoe taarifa kwako. Kwa hiyo nenda Manispaa kamtafute Mkurugenzi muombe kibali au mwambie anipigie simu ndiyo uje nikueleze hicho unachotafuta," alisema Msumali.

Alipofikiwa na kuelezwa hali hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kigurumjuli alihoji ni kwanini Tanzania PANORAMA linafuatilia mradi wa ujenzi wa soko la Tandale wenye kelele nyingi badala ya  kuandika maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ghorofa la ofisi ya Mkurugenzi au ujenzi wa bwawa na kufua umeme la Mwalimu Nyerere.

"Kwanini Ujenzi wa Soko la Tandale ambalo lina kelele nyingi saaana. Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa ghorofa hiyo hapo sasa umefikia ghorofa ya nne, kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere? Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa, kwanini huandiki kuhusu stendi Mpya ya mabasi ya Dad es Salaam?

" Lakini nimeitwa mahali sasa siwezi kuwasiliza kwa sababu nimeitwa na wakubwa. Njooni kesho," alisema Kagurumjuli.

Alipotafutwa siku iliyofuata alisema kusimama kwa mradi huo kunachangiwa na sababu nyingi ikiwemo ya kukosekana kwa saruji. Alipoulizwa kuhusu zuio la kuandika habari za soko hilo alisema halitambui isipokuwa mwananchi anapaswa kufuata utaratibu kuingia katika miradi ya aina hiyo.

"Hilo zuio silijui na nitoe barua kwa mwandishi kwenda kuandika habari kutok lini hiyo. Hao watakuwa na yao lakini wananchi wanaruhusiwa kuingia kwenye miradi ya aina hiyo kwa kufuata utaratibu maalumu ulioandaliwa na (project manager) Meneja mradi," alisema Kagurumjuli.

Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa Namis Corporate Ltd, Uiso alikataa kuzungumza lolote na kueleza aulizwe meneja mradi, Msumali.

Tanzania PANORAMA inaendelea kufuatilia sakata hilo.