Ujenzi wa Soko la Tandale ulipokuwa umefikia mwezi Agosti, mwaka huu
WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa imeelekeza nguvu
kubwa kwenye ujenzi wa miundombinu, shule, hospitali na masoko, jitihada hizo
zimeanza kuingia doa baada ya kusimama kwa ujenzi wa soko jipya la Tandale.
Katikati ya hilo, msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa
kutoa taarifa zinazohusu shughuli za maendeleo bila ukiritimba, zinazofanywa na
serikali ili kutoa fursa kwa wananchi kujua miradi inayotekelezwa kwa kodi zao,
nao unaonekana kuingia doa baada ya mkandarasi anajenga soko la Tandale, Namis
Corporate Ltd kuweka zuio la upatikanaji wa taarifa hizo.
Haya yamebainika baada ya Tanzania PANORAMA Blog kufika
eneo la ujenzi wa soko jipya la Tandale mapema wiki iliyopita kufuatilia
maendeleo ya ujenzi wa mradi huo baada ya kudokezwa na baadhi ya wafanyakazi
kuwa umesimama kutokana na ukosefu wa fedha.
Tanzania PANORAMA Blog baada ya kufika katika eneo la
mradi, lilishuhudia mafundi wakiwa wamekaa kivulini huku ujenzi ukiwa umesimama
na baada ya kuwahoji baadhi yao walisema wanasubiri kulipwa fedha zao waondoke
kwa sababu mahali hapo hakuna kazi tena.
"Bora umekuja na sijui umeingiaje huku maana
hamruhusiwi nyie kuingia humu na wakikuona watakugawana. Hapa hakuna kazi kama
unavyoona ujenzi umesimama hakuna fedha. Tunasikia bosi hajalipwa huko
serikalini ndiyo bado anafuatilia malipo lakini sisi tumeambiwa tukiulizwa
tuseme tuna tatizo la simenti ambalo ni tatizo la kitaifa kwa sasa.
" Kama unaweza twende tukupeleke kwa msimamizi wetu
ukamuhoji ila uwe unajiamini labda watatulipa. Sisi tunasubiri akipata pesa
kutoka serikalini akitulipa ndiyo basi tunatafuta kazi sehemu nyingine maana
hapa, wiki hii mnafanya kazi wiki ijayo hakuna kazi sasa tunajiuliza hiyo
serikali inatoa hela kwa wiki?" alisema mmoja wa mafundi hao.
Msimamizi wa mradi alipofikiwa na Tanzania PANORAMA Blog na
kuulizwa, kwanza alielekeza afuatwe ofisini ambako alichukua simu na
kuwasiliana na Makao Makuu ya kampuni yake kisha alisema;
"Unasema kuna wenzako kwenye gari wanakusubiri ....
Umesema hujapiga picha.... Hili ni eneo la ‘site,’ mtu yoyote haruhusiwi
kuingia humu bila kibali cha makao Makuu, awe Mkuu wa Mkoa, awe Waziri
anapotaka kuja hapa ni lazima awe na kibali kwa sababu anaweza kuangukiwa na
kitu kizito kama nondo au ubao ukaumia.
" Sasa nimeongea na Makao Makuu nadhani umeona
naongea na simu, kama una maswali nenda huko watakujibu na kama unataka
kutembelea hapa uje na kibali cha maandishi kutoka makao makuu.
"Tena tumekuheshimu sana kwa sababu umeingia eneo
ambalo haliruhusiwi ila kwa vile una wenzako nje njoo nikupitishe njia salama
usije ukajikwaa halafu mkaanza kutunga uongo, " alisema.
Tanzania PANORAMA Blog lilifika Makao Makuu ya Kampuni ya
Namis Corporate Ltd yaliyopo Mbezi Africana kwa ajili ya kupata maelezo ya
kasimama kwa ujenzi wa soko la Tandale na kuelezwa kuwa mkataba wa ujenzi una
kipengele kinachozuia kutoa taarifa yoyote ya mwenendo wa ujenzi isipokuwa kwa
kibali cha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Akizungumza kuhusu katazo hilo alilodai lipo kwenye
mkataba huo, Meneja Mradi aliyejitambulisha kwa jina la James Msumali alisema
changamoto zinazowakabili katika ujenzi huo anaweza kuzizungumzia iwapo atapata
kibali cha maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa.
"Mimi ndiyo meneja mradi na ndiye ninayeweza
kuzungumza, bosi unayetaka kuonana naye hayupo. Utaratibu upo hivi, mkataba
wetu una kipengele kinachoelekeza kuwa taarifa yoyote ya mradi haiwezi kutolewa
mpaka kwa kibali cha Mkurugenzi.
"Tena kibali cha maandishi au anipigie simu yeye
mwenyewe aseme nitoe taarifa kwako. Kwa hiyo nenda Manispaa kamtafute
Mkurugenzi muombe kibali au mwambie anipigie simu ndiyo uje nikueleze hicho
unachotafuta," alisema Msumali.
Alipofikiwa na kuelezwa hali hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa
ya Kinondoni, Aron Kagulimjuli alihoji ni kwanini Tanzania PANORAMA Blog linafuatilia
mradi wa ujenzi wa soko la Tandale wenye kelele nyingi badala ya kuandika
maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ghorofa la Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni
au ujenzi wa bwawa na kufua umeme la Mwalimu Nyerere.
"Kwanini Ujenzi wa Soko la Tandale ambalo lina kelele
nyingi saaana. Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa ghorofa hiyo hapo sasa
umefikia ghorofa ya nne, kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa bwawa la Mwalimu
Nyerere? Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa, kwanini huandiki
kuhusu stendi Mpya ya mabasi ya Dar es Salaam?
" Lakini nimeitwa mahali sasa siwezi kuwasikiliza kwa
sababu nimeitwa na wakubwa. Njooni kesho," alisema Kagurumjuli.
Alipotafutwa siku iliyofuata alisema kusimama kwa mradi
huo kunachangiwa na sababu nyingi ikiwemo ya kukosekana kwa saruji. Alipoulizwa
kuhusu zuio la kuandika habari za soko hilo alisema halitambui isipokuwa
mwananchi anapaswa kufuata utaratibu kuingia katika miradi ya aina hiyo.
"Hilo zuio silijui na nitoe barua kwa mwandishi
kwenda kuandika habari kutoka lini hiyo. Hao watakuwa na yao lakini wananchi
wanaruhusiwa kuingia kwenye miradi ya aina hiyo kwa kufuata utaratibu maalumu
ulioandaliwa na (project manager) Meneja mradi," alisema Kagurumjuli.
Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa Namis Corporate Ltd,
Thomas Uiso alikataa kuzungumza lolote na kueleza aulizwe meneja mradi,
Msumali.
Tanzania PANORAMA inaendelea kufuatilia sakata hilo.