NA MWANDISHI WETU
ASKARI Polisi wa Kituo Kidogo cha Polisi Mtongani
kilichopo Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam wameeleza kuwa
wanakabiliwa na ukata mkali unaokwamisha utekelezaji wa majukumu yao ya kulinda
usalama wa raia na mali zao.
Wameeleza hayo baada ya Tanzania PANORAMA Blog
kuhoji sababu za mafaili ya kesi zilizofunguliwa kituo kidogo cha Polisi
Mtongani kushindwa kupelekwa Kituo cha Polisi Kawe kwa zaidi ya siku tano.
Akijibu swali la mmoja wa walalamikaji jana asubuhi
lililohoji; kwanini mafaili ya kesi zilizofunguliwa hayajapelekwa Kawe kwa
zaidi ya siku tano wakati siyo mbali, mmoja wa askari aliyekuwa kituo hapo
alisema "muzee walishindwa tu kukwambia ukweli, hali ni mbaya, tuna hali
mbaya hadi usafiri wa kupeleka mafaili hapo Kawe hatuna."
Alipoambiwa kuwa mlalamikaji yupo tayari kuwasaidia
polisi usafiri wa kubeba faili hizo kuzipeleka Kituo cha Polisi Kawe kwa sababu
amesumbuka muda mrefu na anatumia gharama kuzunguka vituo vya polisi Kawe na
Mtongani, polisi huyo alisema hilo haliruhusiwi ila atajitahidi kutafuta njia
ya kuyapeleka mafaili hayo.
Dalili za kuwepo kwa ukata kwa polisi hao zilianza
kuonekana Jumamosi ya Oktoba 10, 2020 baada ya Mwandishi wa Tanzania PANORAMA
Blog kufika kituo kidogo cha Polisi Mtongani akiwa amejeruhiwa vibaya na wezi
waliokuwa wamewateka abiria kwenye daladala na kuwashambulia kwa bisibisi na
mapanga kabla ya kuwanyang'anya pesa, simu na vitu vingine vya thamani
walivyokuwa navyo kisha kuwatupa pembezoni mwa barabara.
Mwandishi wetu aliwaeleza polisi hao kuwa alipanda
daladala la wahalifu akiwa na abiria wenzake wawili katika kituo cha daladala
cha njia panda ya kwenda Hotel ya Bahari Beach ambapo mmoja wa wahalifu alikuwa
ametangaza kuwa linakwenda stendi ya Makumbusho.
"Hatukujua kama ndani ya daladala hilo kulikuwa
na wahalifu, mmoja wao alitangaza kuwa linakwenda Makumbusho hivyo mimi na
abiria wenzangu wawili tukapanda pale kituo cha kona ya kwenda Bahari Beach.
Lakini lilipoondoka tu wale wezi ambao walikuwa zaidi ya 20 mle ndani wakaanza
kupiga kelele kama washangiliaji wa mpira na dreva akawasha muziki kwa sauti ya
juu ikawa kelele tu.
" Hapo wakaanza kutushambulia, walianza na mama
tuliyepanda naye akawa anakataa kuachia pochi yake, wakamkata panga mkononi
ukabaki unaning'inia, wakachukua kila kitu wakamsogeza mwisho kabisa wa gari na
kijana mwingine niliyepanda naye yeye alikuwa amekatwa mapanga mawili kichwani
na kuwapa kila kitu akabaki analia tu.
"Mimi nilijaribu kumwambia dreva apunguze sauti
ya muziki ajabu alitoa upanga akanambia tulia kisha akaendelea kuendesha gari
kwa kasi. Kwa sababu mlango wa gari ulikuwa umefungwa na taa zilikuwa zimezimwa
niliiona hatari iliyokuwa mbele, sikuwa mbishi niliwapa pesa, simu nao
walinisachi na kuchukua kila walichoona kinafaa.
" Walinishambulia kwa ngumi tu lakini
walinijeruhi vibaya usoni na mdomoni nadhani kwa sababu sikuwa mbishi na
walikwenda kunitupa Kona ya Mbuyuni wakawa wameondoka na mama ambaye wamemkata
mkono, namba ya gari nimeikariri ina mstari wa njano ya wekundu wa damu ya
mzee, tukiifukuza tunaikamata kwa sababu nimeona huko mbele kuna foleni,"
alijieleza mwandishi wetu mbele ya kaunta ya polisi.
Polisi aliyekuwa akisikiliza maelezo yake alisema hawana
uwezo wa kuifukuza daladala hiyo kwa sababu eneo hilo la kipolisi hadi Kawe
lina gari moja tu bali anamfungulia RB na atampa PF 3 akatibiwe kwa sababu
alikuwa akivuja damu nyingi.
"Hatuna jinsi ya kulifukuza mzee tuna gari moja
tu nalo muda huu linasambaza askari kwenye malindo, we acha kumzungumzia mama
aliyekatwa mkono naye watamtupa huko mbele atakwenda kutoa taarifa kituo
chochote cha polisi kama ulivyofanya wewe.
" Nakufungulia faili nakupa PF 3 nenda
Hospitali ukatibiwe angalia tisheti yote ulivyoloa damu, jihurumie umeumua sana
acha kuhurumia wengine.
"Kwa sababu umetutajia namba na rangi za mstari
wa hilo daladala Jumatatu tu tutalikamata. Hao wahalifu wamekuwa tishio
huwa wanaenda beach huko kila weekend kufanya uhalifu msiwe mnapanda daladala
zao maana ndiyo mbinu yao mpya.
"Katibiwe nenda nyumbani kasikilizie hali yako
Jumatatu asubuhi saa mbili uwe polisi Kawe utamkuta mpelelezi wa kesi yako,
kesho jumapili hakuna kazi hivyo jumatatu litakamatwa hilo daladala,"
alisema askari aliyekuwa kaunta.
Jumatatu, Oktoba 12, 2020, saa tano asubuhi
mwandishi wetu alifika Kituo cha Polisi na kuonyesha RB namba KMT/RB/2428/2020
aliyopewa kituo kidogo cha Polisi Mtongani ili aonyeshwe mpelelezi wa kesi yake
lakini polisi aliyekuwa kaunta alisema mafaili kutoka Mtongani hayajafika
kituoni hapo wala hakuna kumbukumbu zake zilizorekodiwa kwenye rejista kituoni
hapo na kuelekezwa arudi Mtongani kesi yake itashugulikiwa huko.
Alhamis, Oktoba 16, 2020 mwandishi wetu alirejea
kituo cha Polisi Mtongani ambako baada ya polisi kukagua makaratasi mengi
yaliyokuwa kaunta walisema faili lake bado lipo kituoni hapo likisuburi
utaratibu wa kupelekwa Polisi Kawe.
"Siyo peke yako mzee, faili zote hizi
hazijapelekwa hali mbaya, hakuna usafiri. Wewe uwe unapitapita pale Polisi
Kawe siku tukilipeleka utalikuta ataambiwa," alisema askari aliyekuwa
kaunta.
Alipoelezwa kuwa kwa sababu ya kupunguza usumbufu na
gharama za usafiri na pia kuokoa muda anaweza kutoa msaada wa usafiri ili
mafaili hayo yapelekwe Kawe aliambiwa hilo haliruhusiwi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni,
Camillius Wambura alipotafutwa jana kwa simu yake ya kiganjani kuzungumzia
ukata huo alipokea msaidizi wake na kueleza kuwa yupo kwenye kikao atafutwe
muda mwingine.
Alipotafutwa leo alipokea simu na kueleza kuwa
hasikii vizuri anachoulizwa pengine yupo eneo baya hivyo atumiwe ujumbe na
alipotumiwa ujumbe kwenye simu yake akiulizwa kuhusu kuwepo ukata katika eneo
lake la utawala na kukwama kwa mafaili ya kesi kituo cha Polisi Mtongani kwa
siku tano, hakujibu.